Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili name niweze kuchangia katika hotuba hii muhimu na ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na ninaomba uniruhusu pia nimfikishie salamu za Watanzania walio wengi, kila mahali tulipotembelea miradi, tumekuwa tukipokea pongezi na salamu za wananchi wakisema kufikishe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, pongezi kwa Mheshimiwa Rais. Nami nitumie nafasi hii niziwasilishe salamu na pongezi kutoka kwa wananchi, kwa sababu wanatambua kwamba Serikali yao ya Awamu ya Tano kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ndiyo kiunganishi muhimu cha sekta za uchumi katika nchi hii na kwamba ni kichocheo katika kukua kwa uchumi na maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nizungumze tu kama ufafanuzi kwa Waheshimiwa Wabunge. Kwanza nianze kwa kuwapongeza kwa michango mizuri na utashuhudia kwamba uchangiaji wa bajeti una mabadiliko makubwa sana. Kwa hiyo, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa sababu kwa sehemu kubwa tumepokea ushauri na sehemu kubwa tumepokea maelekezo ya Waheshimiwa Wabunge katika kutekeleza majukumu yetu, wanafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, nami nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla na yale yote ambayo wameyatoa kama ushauri, nasi kama Serikali na kama Wizara pia tutaendelea kuyatekeleza.

Mheshimiwa Spika, nifafanue tu mambo mawili ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi walizungumza hasa hoja ya kuimarisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua katika kipindi hiki ambacho tumepokea mvua nyingi. Niseme tu kwamba Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu hasa ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini kuanzia kipindi cha Oktoba, 2019 mpaka mwezi Machi.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba tumejipanga kwa maana ya kuendelea kurejeshea miundombinu. Ukiangalia kwa ujumla wake, ukubwa wake kwa kipindi hiki kulikuwa kuna makadirio kama ya shilingi bilioni 34.3 ambapo upande wa TARURA ilikuwa kama shilingi bilioni 40 na upande wa TANROAD shilingi bilioni 34. Kwa hiyo, utaona athari hizi zimetuchota mafungu makubwa sana kuendelea kuimarisha.

Mheshimiwa Spika, kubwa niseme tu kwamba tumejipanga vizuri kuhakikisha Serikali inaendelea kurejesha miundombinu ili ile sera ya kuhakikisha wananchi wanapita na kwenda kwenye shughuli zao za maendeleo, ziendelee bila kupata kikwazo chochote.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie barabara hii muhimu ambayo Mheshimiwa Lubeleje alikuwa ameizungumzia. Hii barabara utakubaliana nami kwamba ni barabara muhimu. Ni barabara inayotuunganisha kutoka Mbande kwenda Kongwa - Mpwapwa mpaka kule Kibakwe. Hii barabara tulishaifanyia usanifu kwa ajili ya kufanya matengenezo. Kwa sasa shughuli za ujenzi zinaendelea, Mkandarasi aliyeko kwenye site amekamilisha kilometa tano na zile kilometa nyingine 11.7 kukamilisha kilometa 16.5 kwenda mpaka Kongwa ikifika mwezi wa Tano natumaini kwamba tutakamilisha barabara hii.

Mheshimiwa Spika, vile vile uko ujenzi wa kilometa mbili ukitoka Mpwapwa kuja Kongwa unaendelea vizuri na tumeshasaini mkataba na Mkandarasi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje na wananchi wa maeneo hayo tuliyoyataja wasiwe na wasiwasi, tumejipanga vizuri kuona kwamba tunaendelea kupeleka huduma hii muhimu ya barabara kuelekea Mpwapwa na siyo Mpwapwa peke yake, kwenda mpaka maeneo mengine ambayo tunajua yanayo uzalishaji mkubwa na huduma hii ni muhimu sana kwa Wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Lubeleje pia alizungumza juu ya madaraja muhimu sana haya; kule Godegode, Mpwapwa, Nyasungwi na Mbande. Niseme tu, katika mwaka wa fedha huu ambao tunaokwenda nao tulitenga fedha na kazi ya usanifu wa madaraja hayo ulishakamilika. Tunaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba tunarejesha madaraja haya muhimu ambayo Mheshimiwa Lubeleje ameyataja, nasi tunayaangalia kwa macho mawili.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa ujumla wake, Dodoma ni kati ya Mikoa ambayo imeshambuliwa sana na hizi mvua nyingi tulizozipata. Kwa hiyo, utaona Dodoma ni kubwa, maeneo mengi yalikuwa yamepata athari za mvua. Niwahakikishie tu wakazi wa Dodoma na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba tumejipanga kuhakikisha tunaenda kufanya maboresho makubwa kwenye maeneo haya ambayo yameharibiwa; siyo hapa Dodoma tu, lakini na maeneo mengine ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka nichangie hayo kwa sababu ya muda, lakini niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tutakwenda kufanya maboresho ya miundombinu hii. Yumkini katika bajeti inayokuja pia tutaonyesha namna tulivyojipanga ili maeneo yote haya yaliyopata athari za mvua tutakavyoyafanyia urejeshaji kupitia bajeti.

Mheshimiwa Spika, naamini Bunge lako litatupitishia fedha ili tuende kufanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanarudishiwa huduma muhimu za miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, narudia tena kusema naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ni hotuba nzuri na bajeti nzuri ili tuende tukafanye kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)