Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo kwa kweli inatekelezeka kwa asilimia 100. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naungana na Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri wengine waliochangia kupongeza kwa kweli taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu maeneo ambayo nitapita kwa kifupi sana ni matatu. Jambo la kwanza ililionekana ni kuhusiana na suala la LNG na suala la pili ni mradi wa mafuta wa ECOP wa Uganda na Tanzania na eneo la umeme vijijini.

Mheshimiwa Spika, napenda nianze na la mwisho. Katika eneo hili la kupeleka umeme vijijini, napenda niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wanaonisikiliza kwamba jambo hili limetupa sifa sana kidunia, tumefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bila kupoteza muda, labda niwapitishe Waheshimiwa Wabunge kidogo tu. Mwaka 2008 tulipoanza kutekeleza miradi ya kupeleka umeme vijijini tulikuwa kwenye nafasi ya 50 Afrika na tulifikisha asilimia 16.5 lakini Mwaka 2015 tulipofikisha sasa asilimia 39.5 tulikuwa na nafasi ya 25 Afrika. Mwaka 2017 tukiwa tunasogea sasa, wakati tunapelekea umeme vijijini tulifikia asilimia 47 tukiwa kwenye nafasi ya 18. Mwaka 2018 tulifikia nafasi ya nne Afrika tukiwa na asilimia takribani 58. Mwaka 2019 mwezi Desemba tulikuwa nafasi ya tatu, wakitupita Afrika Kusini na Nigeria. Mwaka huu mwezi wa Pili tukashika namba moja. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu, mwaka 2019 Afrika Kusini walikuwa na silimia 64 umeme vijijini; Nigeria walikuwa na asilimia 72 kwa umeme vijijini; leo sisi tunapoongea tuna asilimia 75.2 umeme vijijini. Kwa nini nimelazimika kuyasema haya?

Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa kipindi chote hiki kuwapelekea umeme Watanzania. Takribani shilingi trilioni 2.8 zimetumika kuwapelekea umeme wananchi kwenye maeneo haya. Hongera sana Mheshimiwa Spika, hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, nampongeza sana Mheshimiwa Rais katika jukumu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwezi ukazungumza uchumi wa viwanda kama umeme vijijini haupo. Viwanda vinajengwa na raw materials kutoka vijijini, kwa hiyo msitari wa kwanza kupeleka viwanda ni kuanzia vijijini. Serikali yetu imejipambanua vizuri; huwezi leo ukazungumza kujenga kiwanda Dar es Salaam, eneo liko wapi? Huwezi kuzungumza kujenga kiwanda kizuri Dodoma Mjini, eneo liko wapi? Maeneo ya viwanda yako vijijini, ndiyo maana umeme tumepeleka huko. Kwa hiyo, jambo hili tumelitekeleza vizuri sana, naipongeza sana Serikali. Katika hili, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge. Wametupa ushirikiano mzuri sana katika kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona niseme machache katika eneo hili kwa sababu ya muda. Najua tutawasilisha taarifa yetu mwezi ujao tarehe 26, nitaeleza kwa upana zaidi katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi, tunapoongea hapa, zipo Wilaya 35 ambazo Kata zake zote zimefikiwa na umeme, vijiji vyake vyote vimefikiwa na umeme. Kwa hiyo, mradi unaokuja hatutapeleka umeme kwenye vijiji, bali kwenye Vitongoji tu. Ni jambo kubwa sana limefanyika kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, katika eneo hilo, ni-reserve muda tu kwa ajili ya taarifa nyingine ambazo nimetakiwa nizieleze mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la mradi wa LNG kumekuwa na concern kubwa sana kwamba inawezekana mradi huu hautekelezeki. Naomba nitoe taarifa mbele ya Bunge lako tukufu; mradi wa LNG uko pale pale. Utatekelezwa na kazi za kufanya zinafanyika na Serikali imetenga fedha na harakati za kutekeleza zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, labda nitoe taarifa kidogo. Ni kweli takriban miaka miwili iliyopita speed imekuwa siyo nzuri na zipo sababu za msingi. Sababu ya kwanza, kwanza nilipongeze Bunge lako, mwaka 2018 uliunda Tume Maalum ya Wabunge Kupitia Mikataba ya Kugawana Mapato. Katika mapendekezo ya Tume ya Wabunge, ilipendekeza mikataba yote 11 (PSA’s) zifanyiwe mapitio na taratibu nyingine ziendelee baada ya mapitio hayo kukamilika. Sasa hili ni letu sisi kama Serikali. Tulifanya hivyo kwa nia njema ili kuhakikisha kwamba tunapokwenda huko mbele ya safari hatuangukii shimoni.

Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, baada ya mapendekezo ya Tume ya Bunge, Serikali imefanyia kazi mapendekezo hayo. Pamoja na kazi iliyofanyika ni kufanyia mapitio. Mwanasheria Mkuu wa Serikali amefanya kazi hiyo, nampongeza sana na kazi imekamilika. Hivi karibuni taarifa imewasilishwa Serikalini. Kinachofanyika sasa, Serikali inatafakari taarifa hiyo ili mapendekezo yatakayotokana na mapitio hayo sasa tuendelee na hatua ya utekelezaji wa mradi wa LNG.

Mheshimiwa Spika, kwa hatua tu tuliyofikia, jambo la kwanza tumetenga gesi asilia tani milioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, commitment ya Serikali iko pale pale. Jambo la pili, tumetenga fedha kuwalipa wafidiwa 693 ambao watafidiwa takribani ekari 2,071; na hivyo pesa zipo. Najua Waziri wa Fedha amejiandaa kuwalipa taratibu zikikamilika, nadhani ni mwisho wa kipindi cha fedha cha mwaka huu. Kwa hiyo, ambao wamepitiwa na mradi huu wawe na imani na Serikali, watalipwa fidia zao ilimradi uhakiki utafanyika. Nimeona nitoe taarifa kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni mradi wa mafuta wa Hoima na Tanzania. Kwanza naipongeza Serikali mradi huu unatekelezwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, nieleze tu kidogo yapo mambo mawili ambayo tumeyafikia kwa sasa. Jambo la kwanza ni wenzetu Waganda walianza majadiliano na wazalishaji wa mafuta kwenye mkondo wa juu, imetuchukuwa muda mrefu lakini napenda kutoa taarifa kwamba wametuletea taarifa majadiliano wamekamilisha kwa hiyo sasa kuanzia hapo tunaweza kuendelea na mradi.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili tumekamilisha kwa upande wetu tadhimini ya watakao fidiwa ambao wanafika watu takribani watu elfu tisa kwa upande wa korido, lakini takribani watu elfu 3,420 kwenye maeneo yatakapo jengwa camp fedha zipo takribani bilioni 50 zimetengwa na Serikali yetu tukufu na Bunge lilipitisha tunashukuru sana kwa kazi hii. Kwa hiyo, niseme tu kwamba miradi itatekelezeka bila wasiwasi wote isipokuwa haya mambo mawili tunayakamilisha.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwenye mradi huu ni suala la corona tunachofanya kwa sasa kwa sababu wataalam wetu hawawezi kwenda Uganda na waganda kuja Tanzania tunafanya mikutano kwa video conference ili kuonyesha kwamba Serikali tumekusudia kutekeleza mradi huu, kwa sababu ya muda nimeona nichangie haya machache sasa naunga hoja asilimia mia moja.