Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niungane na Wabunge wenzangu kuchangia katika bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Napenda kwanza kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa sana aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano. Sina wasiwasi kabisa miaka mitano mingine ijayo tutaona mapinduzi makubwa sana ya kimaendeleo katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze kuchangia katika sekta ya afya na kabla sijaanza kuchangia sekta ya afya nimpongeze Makamu wa Rais, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na nimpongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Manaibu wake Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Mwita pamoja na Katibu Mkuu na Manaibu wake kwa kazi kubwa sana wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa upande wa sekta ya afya ndani ya kipindi cha miaka mine, tayari Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano imeanza kujenga na kukarabati hospitali za halmashauri 98, kati ya hizo 77 zimekamilika. Zitakapokamilika zote mwezi Juni, 2020 tutakuwa na hospitali za Halmashauri za Wilaya 175, ndio kusema tutabakiwa na Halmashauri tisa tu kujenga hospitali za wilaya ambazo nina uhakika kwa speed ambayo tunayo ndani ya mwaka mmoja wa mwaka 2020/2021 tutakuwa tumemaliza kabisa zoezi la kujenga hospitali za wilaya na hivyo kuifanya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuhamia kwenye ujenzi wa vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu ambaye anasema tangu tumepata Uhuru mpaka sasa hivi tumejenga vituo vya afya 900. Tanzania tuna kata 3,956 mpaka sasa hivi tumeshajenga vituo vya afya zaidi ya 900, ndiyo kusema kwamba tunahitaji chini ya miaka 10 kukamilisha ujenzi huu. Kwa sababu kama tumeweza kujenga vituo vya afya 433 ndani ya kipindi cha miaka 5, tunahitaji chini ya miaka 10 kukamilisha vituo vya afya 3,956. Kwa hiyo, yule aliyekuwa anasema tutahitaji zaidi ya miaka 20, hebu arudi kwa mwalimu wake wa hesabu na akazipitie tena zile hesabu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Ghasia, kuna taarifa, Mheshimiwa Mwakagenda.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa, nimkumbushe tu kwamba tunamshukuru Jafo angalau kajitahidi, yeye alikuwa Waziri wa Wizara hii na alikuwa ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, labda kama anatuambia anaomba msamaha kwa kwenda taratibu, hakufikia malengo. Nakupongeza Mheshimiwa Jafo kwa kufanya kazi nzuri. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunapotaka kutoa taarifa tutumie zile Kanuni zetu vizuri. Hii siyo taarifa, Mheshimiwa Hawa Ghasia, endelea na mchango wako.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, anajifurahisha kwa sababu nimesema tumeongeza kutoka vituo vya afya 535 kwenda 968. Ndiyo kusema kuna kazi iliyofanyika siku za nyuma na tunaendeleza. Ndiyo maana nikasema tukikamilisha Hospitali za Halmashauri 98 tutakuwa na Hospitali za Halmashauri 175. Maana yake kuna kazi imefanyika siku za nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokisema speed imeongezeka na ndiyo maana nikasema kwa speed ambayo Mheshimiwa Jafo anayo, kwa speed ambayo Mheshimiwa Magufuli anayo…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. HAWA A. GHASIA: … tunahitaji chini ya miaka 10 kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya katika nchi yetu. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, ungempa muda azungumze maana umeingia sasa hivi, umeshamsikia na mchango na taarifa unayo?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa. Hadi nimesimama maana yake nimemsikia kuna kitu nataka nimpe taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Ghasia, endelea na mchango wako. (Makofi)

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, wataelewa tu, naona wanaelewa kidogo kidogo na wanachangamka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiacha hospitali za wilaya, Serikali ya Awamu ya Tano iko katika mchakato mpaka kufikia Juni, 2020 itakuwa kwa zaidi ya asilimia 60 imekamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini. Hata anayezungumza anafahamu kwamba katika Mkoa wake wa Mara kuna Hospitali ya Rufaa inajengwa na Chato pia inajengwa na zikikamilika hizo ndiyo kusema kwa maana ya Kanda tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa Hopsitali za Rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokea kule juu kwenye rufaa tunakuja kwenye hospitali za halmashauri, hospitali za mikoa, katika sekta ya afya, Mheshimiwa Magufuli akiingia awamu ya pili ana-deal na vituo vya afya na zahanati tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale ambao wanasema kwamba hakuna kilichofanyika, hebu warudi waangalie tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Watakubaliana na mimi kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza Ilani yake kwa speed kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kumpongeza Mheshimiwa Jafo kwa kusimamia vizuri elimu bila ada. Kama ambavyo tumesema, hili ni wazo la Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli la kuhakikisha kwamba watoto wote wa maskini wanakwenda shule na kuondoa ada katika shule zetu. Jambo hili limeongeza watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza na hata wanaokwenda sekondari na imesaidia sana wazazi kujikita katika kuwapatia wanafunzi mahitaji mengine ambayo zamani ilikuwa wachangie ada na pia watafute na sare na vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongeza ujenzi wa vyumba za madarasa na ujenzi wa mabweni. Mimi ninayezungumza katika halmashauri yangu tunayo mabweni mawili ambayo yanaendelea kujengwa, tumepata pesa za kukamilisha maboma katika halmashauri yangu na miundombinu katika elimu ya sekondari na msingi imeboreshwa kwa kiasi kikubwa. Nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mkuu wangu wa Mkoa Mheshimiwa Blasius Byakanwa kwa ubunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Serikali Kuu ilipojikita katika kukamilisha vyumba vya madarasa, kujenga nyumba za walimu yeye akaja na wazo la shule ni choo na akahamasisha wananchi, viongozi mbalimbali katika mkoa wetu na sasa hivi tunafanya vizuri sana katika kuhakikisha kwamba tunasaidiana na Serikali Kuu. Si kila kitu kuiachia Serikali, tunakuja tunasimama hapa tunasema kitu fulani hakijakamilika, sisi kama sisi na wananchi wetu tumefanya nini?

Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kuja na wazo la shule ni choo pamoja na mengine yale ambayo yako katika mchakato mzuri sana, nina imani kabisa tutamsaidia katika kupitisha sheria ili gongo sasa ikawe sanitizer. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha Mamlaka ya Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA). TARURA imefanya kazi nyingi sana na kubwa sana. Nachoiomba Serikali ni kuiongezea vyanzo vya mapato. Pesa wanayopewa TARURA na kazi waliyonayo ni tofauti. Tunaomba tuwaongezee na tuwatafutie vyanzo vya uhakika vya mapato ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Jafo pamoja na Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu, ahsante sana. (Makofi)