Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuwa mtu wa kwanza katika kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote, nisije nikasahau, naunga mkono Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hapa na hotuba alizozitoa wakati anaomba ridhaa ya kuongoza kwa mara ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Mheshimiwa Rais na zile nyingine na hasa Andiko la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inaonyesha dhahiri nia ya Mheshimiwa Rais ya kuhuisha au kujenga upya Dira ya Taifa ya 2020 – 2025. Mheshimiwa Rais nikimnukuu, anasema Taifa hili siyo maskini, lina rasilimali nyingi na anataka kwenda kwenye uchumi mkubwa. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutembea na maneno yake. Alipochukua fursa ya kuteua Baraza la Mawaziri, akachukua Wizara ya Uwekezaji akaiweka chini ya mamlaka yake, yaani yeye ndiye Waziri wa Uwekezaji na akamteua rafiki yangu awe Waziri wa Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amefanya hivyo kwa nia moja. Wawekezaji wako wa kila namna; na kuipeleka nchi hii katika uchumi mkubwa, lazima uchangamshe uwekezaji. Hata mkulima yule wa nyumbani ambaye ametuwezesha kuishi miaka mitano iliyopita bila njaa, naye ni mwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais, nashauri, ili tuweze kufikia malengo yetu, lazima vile vigezo tulivyovipitia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kugundua kwamba vinatuwekea vikwazo, basi vyote avipeleke, aviweke chini yake kama ambavyo Bunge hili liliwahi kumshauri.Namaanisha blueprint. The Blueprint of RegulatoryReform iwekwe chini ya Rais ili Wizara na Taasisi nyingine aweze kuzielekeza namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, sifungui mjadala, lakini hata ungekuwa mganga wa namna gani uliyebobea, huwezi kujifanyia operation kubwa wewe mwenyewe. Wizara yoyote yenye jukumu la kukusanya maduhuli, haitakubali haraka sana kuondoa hayo maduhuli au kodi mbalimbali mpaka Mheshimiwa Rais mwenyewe aseme wewe punguza hapa, punguza hapa, punguza hapa.

Mheshimiwa Spika, nazungumza sana suala la Wizara hii anayoisimamia Mheshimiwa Rais kwa sababu jitihada ya kufikia ule uchumi wa kati na kwenye uchumi mkubwa linahusisha uwekezaji. Nami napenda nitangaze interest; uwekezaji ninaoushabikia ni wa zile sekta za uzalishaji (the productive sectors).

Mheshimiwa Spika, tumefanya vizuri kwenye miundombinu, tumefanya vizuri kwenye elimu, sasa ni wakati wa kuhakikisha tunazidua sekta za uzalishaji, tunalima kwa tija kubwa; kama alivyoniambia Profesa Mkenda kwamba, kupungua kwa bei ya mazao siyo hoja, lakini kipato cha mkulima kisipungue, hata bei ikishuka. Sasa jibu hilo ni kuongeza tija katika shughuli na kuongeza tija katika shughuli maana yake ni uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nina falsafa, nina neno langu ninalolisema kila siku kwamba sasa tuweke flagship project katika shughuli za sekta za kiuzalishaji katika kilimo, uvuvi na katika sekta za namna hiyo. Kwa sababu gani? Hoja siyo kujenga uchumi mkubwa, hoja yetu ni kujenga uchumi mkubwa ulio jumuishi. Unaweza kuzidua mafuta, ukazidua madini ya namna mbalimbali, ukawa na GDP kubwa, ukawa na income per capita kubwa sana, lakini ukawa na watu wenye matambara, ombamba; lakini sekta hizi ni productive sectors ambazo zinahusisha watu wengi.

Mheshimiwa Spika, yote haya yapo, tumeyashughulikia, tumehangaika nayo miaka mitano, sasa ni mwendo wa kupaa. Kwa mara nyingine namuunga mkono Mheshimiwa Rais, nasi wapambanaji wake tuko tayari kupaa naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimezungumzia sekta za uzalishaji, lakini jambo moja ambalo nataka niishauri Serikali, katika maandiko iko kauli ya kwamba tuzalishe kiasi cha kutosha na ziada tuuze nje. Kwa heshima na taadhima, napenda kuishauri Serikali yangu tuondokane na falsafa hiyo. Unapokwenda kuzalisha, uende na malengo mawili makuu, ambapo lengo moja haliathiri lengo lingine. Uende kuzalisha kutosheleza soko la nchi hii na uende kuzalisha ili kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma taarifa au Hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa miaka mitano tuliweza kuuza nje dola bilioni nane na kitu mpaka dola bilioni tisa. Ni mtazamo chanya, lakini siyo namba ya kujivunia, kwa sisi waumini sehemu tulipo, locational advantage; tungetegemea nchi hii iuze sana. Kwa hiyo, zalisheni ili kuuza katika nchi hii na kuuza nje kusudi tuweze kupata fedha za kigeni na kupata uzoefu wa masoko ya nje. Ukizalisha leo kutosheleza maisha ya nchi hii au mahitaji ya nchi hii, wenzako wanaokamata soko la nje, hutakaa kuwatosheleza au kuwaingilia kwenye masoko yao wakati wewe utakapokuwa umemaliza hapa.Ninayo mifano mingi, muda siyo rafiki.

Mheshimiwa Spika, namuunga mkono tena Mheshimiwa Rais kwa kauli yake. Tunatambua kazi nzuri tuliyofanya kwa miaka mitano; watoto wengi wamekwenda shule. Mheshimiwa Rais akasema, kipindi hiki sasa ni kuongeza ubora katika sekta ya elimu. Naungana naye, tuongeze ubora katika wanafunzi ambao wameingia katika shule zetu waweze kuwa na ujuzi.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mkosefu wa fadhila na niko tayari kutoa album, siyo single tena; naishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuweka jiwe la msingi jengo ambalo limekaribia kukamilika la VETA ya Mkoa wa Kagera, jengo lenye thamani ya shilingi bilioni 22 linaloweza kupokea wanafunzi 800 kwa wakati mmoja. Ndiyo maana nilipofurahi nikakumbuka ule wimbo alionifundisha bibi kwamba senene ni tamu kuliko nyama.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Kicheko/ Makofi)