Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi siku hii ya leo nina afya tele. Pia nishukuru chama changu cha CCM kwa kunipa fursa ya kugombea kwenye Jimbo lile la Vunjo ambapo wananchi wake walitupa kura kwa wingi na CCM ikashinda kwa kishindo, kwa hiyo, CCM oyee.

WABUNGE FULANI: Oyee.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, niseme hivi, mimi niliyesoma hivi vitabu vitatu nasema ni kitabu kimoja ambacho bado kinaandikwa bado hakijaisha na naamini kwamba itakapofika mwezi Juni, 2025 tutaona chapter ya nne na pengine ikimpendeza Mheshimiwa Rais tutaona na chapter ya tano itakayokuwa inatuonesha kwamba dira ya 2025 kwenda 2050 itakuwaje lakini ni kitabu kitamu na utamu wake ni kwa sababu una happy ending, unaishia pazuri.

Mheshimiwa Spika, niliposoma nimeona kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyotoa Novemba 2015 anaanza na mambo magumu sana ya kuunda utawala bora na kutafuta uongozi ambao ungeweza ukapigana na mmomonyoko wa maadili ndani ya Serikali, kurudisha nidhamu na kuhakikisha kwamba mapato ya Serikali yanakusanywa vizuri na yanatumiwa vizuri. Naamini kwamba kwa kile alichokifanya kuunda uongozi ambao aliweza kufanya nao kazi lakini pia akawa anatumbuatumbua mpaka tukaona mambo yamesimama vizuri ndiyo sababu tunasema kwamba kusema kweli ni fundisho kubwa linalosema kwamba maendeleo ya Afrika, maendeleo ya Tanzania yanatokana na uongozi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini uongozi bora siyo viongozi bora ni kiongozi mmoja ambaye anajitokeza, the leader, ana make a big difference katika mambo yote yanayofanyika kwenye nchi au kwenye kampuni inakuwa hivyo hivyo, kama ukiwa na kiongozi bora utaona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nashukuru na nasema kwamba kusema kweli ukisoma kitabu hiki ambacho kinaandikwa hakijaisha natumaini utaona wazi kwamba tumempata kiongozi ambaye anastahili sifa kwa kila Mtanzania. Hata mtiririko wa namna anavyoelezea dira na mkakati wake na malengo yake na milestone za kufikia na namna ya kutathmini utaona wazi kwamba ni kitu ambacho kinaeleweka kwa kila mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaona kitu kama hicho hata ukimuuliza bibi yangu pale mgombani kule Moshi wewe ni nani? Anakwambia mimi ni Mtanzania naenda kwenye uchumi wa kati, kipato cha kati na baadaye tutafika kwenye kipato cha juu. Kwa hiyo, kila mtu anaelewa ni kitu gani. Lengo kuu la nchi ni kuinua kipato cha Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake aliyotupa kwenye ufunguzi anasema wazi kwamba sasa amejua kutakuwa na miundombinu lakini hailiwi, lazima sasa tuweze kuwezesha wananchi wetu na wale tunaowaongoza kuongeza kipato chao, wajasiriamali kwa kuwawezesha kupata mikopo na kadhalika ili waweze kuinua kipato chao. Kwa hiyo, nasema kwamba kwa logic ya hiki kitabu kiko vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, nimsifu kwa kitu kimoja, katika nchi ambayo inaenda kwa kasi tunayoona, kasi ya ukuaji wa pato la Taifa kwa asilimia saba kwa wastani, lakini miradi mikubwa inatekelezwa. Utakuta kwamba mataifa mengi yanashangaa kwamba bado tumeweza kuendelea na utulivu wa uchumi mkubwa. Utulivu huo umetokana na umakini wa Mheshimiwa Rais, lakini pia tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wetu wa Fedha na Mipango pamoja na Gavana wa Benki Kuu kwa ushauri mzuri waliotoa. Kwa sababu wangeweza wakachukua njia rahisi ya kufanya inflation finance maana ku-print pesa na kukuza mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wao hawakufanya hivyo, wametumia njia ngumu ya kukusanya mapato kutoka kwa Watanzania, hiyo njia ngumu kuliko ku-print pesa au kukopa tu na ni kweli kwamba hii miradi mikubwa ungekuta kwamba inashawishi watu sana kuchukua mikopo ya ziada, lakini nashukuru kwamba hawakufanya vile wamefanya kitu ambacho ni kigumu, lakini tunaona matunda yake ni mazuri na ndio hapa unasema hapa tunaona kuna happy early.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme hivi tumeona kuna utulivu wa uchumi wa ujumla ndio, exchange rate imekuwa stable, mfumuko wa bei uko chini, riba zimetulia lakini hazijatulia mahali pake kwa sababu ziko juu bado watu wanalalamika riba asilimia 15 inflation asilimia tatu, really interest rate ni kubwa sana. Kwa hiyo, kinachohitajika sasa ni pengine tuhakikishe kwamba tunaendeleza sera hizo za kuhakikisha kwamba riba nazo zinashuka kwenye mabenki yetu. Utaona mabenki yanarekodi faida kubwa sana, mwaka huu kwa mfano, faida za mabenki ni kubwa sana kwa sababu wanatoza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoke hapo niseme hivi, kwa kuona kwamba miundombinu inaboreshwa vizuri, sasa njia ya peke ni kuongeza uwekezaji na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusema kwamba ameunda Wizara ndani ya ofisi yake ambayo inashughulika na uwekezaji. Niseme hivi kwamba private sekta haitaweza kunufaika sana kama blue print aliyoizungumza Mheshimiwa Mwijage haitatekelezwa kwa umakini na kwa haraka zaidi. Inatekelezwa kwa speed tofauti tofauti kwenye kila Wizara, lakini ingetekelezwa kwa speed ile wanayotekeleza kwa mfano Wizara ya Viwanda naamini ungekuta vitu vinabadilika na pengine private sector ingeweza ikaanza kushika hatamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba tatizo kubwa katika sekta binafsi ni kusema kwamba uwekezaji lazima uwe mkubwa sana, kumbe sasa hivi uwekezaji hata kwenye nyumba yako unaweza kwa sababu kuna umeme. Ukishakuwa na umeme unaweza ukawa na kiwanda kidogo cha kuchakata hata ndizi na hiyo ndio njia peke kusema kweli ya kuinua kipato kule kwetu mashambani kwa kuunda viwanda vidogo kwa vikundi au kwa mtu mmoja mmoja ambaye ataweza kuchakata mazao akayaongezea thamani na yale mazao yakauzwa sehemu nyingine ambapo hayapatikani au ambapo yanahitajika kwa wakati ule.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba pengine tuangalie namna gani ya kuwawezesha vijana wetu au wajasiriamali wanawake na wengine na hata akinababa kwa kuwapa exposure. Nikasema exposure haiwezi kutolewa kwa kumpeleka mtu China kuangalia maonesho China hapana, exposure ni kwamba pengine Shirika letu la SIDO lingekuwa karibu zaidi kule kwenye vijiji sasa linashughulika kwa kuona kwamba kweli linaonesha watu kwamba kuna kiwanda kidogo cha shilingi milioni moja au laki tano na hiki kiwanda unaweza ukakitumia mkiwa vijana watano, mkakitumia mkaongeza thamani mkapeleka mkauza. Naamini kwamba hicho lazima kifanyike na naamini kwamba Wizara inayohusika itafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunazungumza mambo ya mikopo, kupeleka watu vyuo vikuu, hii nataka kusema katika uchumi tunaojenga sasa hivi uchumi wa kati, tatizo kubwa ni skills study zile za watu kufanya vitu kwa mkono sio kuwa na degree sio kuwa na ma-Ph.D hayatasaidia sana. Utakuta kwamba unemployment kati ya watu waliomaliza chuo kikuu ni kubwa sana lakini mtu anayetengeneza simu, simu hizi tunazotembea nazo hizi mfukoni ukimtafuta mtaani humpati na wana kazi, mechanic wote wana kazi lakini tatizo moja tunasema tu kwamba elimu yetu inalenga chuo kikuu, hapana! Huko ni kwa zamani, elimu ilenge daraja…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: …baada ya kumaliza form six watu wengi waende kujifunza kazi za mikono, study za mikono. Kwa hiyo, vyuo vya ufundi viongezeke…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Lakini na vyenyewe vibadilishe mwelekeo sio kuangalia zile study zilizokuwa zinahitajika zamani tuangalie study za kisasa, electronic base na ambazo…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kimei pokea taarifa, jitambulishe Mheshimiwa nani.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naitwa Mheshimiwa Musukuma, ningependa kumpa taarifa tu Mheshimiwa Dkt. Kimei kwamba anavyochangia anasema tuache kuamini ma-degree na ma-PhD. Nampa taarifa tu kwamba duniani kote matajiri wengi hawana degree. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa!

SPIKA: Kabla Mheshimiwa Dkt. Kimei hujapokea taarifa hiyo, nisisitize tu Waheshimiwa Wabunge mumsikilize Mheshimiwa Dkt. Kimei hoja yake, ni hoja ya msingi sana. Hii habari kila mwanafunzi anaenda chuo kikuu anasoma vitu vya ajabu ambavyo tumezoea traditionally, sitaki kuyataja masomo, yako masomo yaani ni kama kumpotezea mtoto tu direction. Yalikuwa na maana enzi hizo, lakini leo hii dunia ya sasa, dunia ya uchumi wa kati, ndio hii anayopendekeza Mheshimiwa Dkt. Kimei. Skills na kwa hiyo hata mfuko wa mikopo uelekeze zaidi mikopo yake huko. Mheshimiwa Dkt. Kimei hebu rudia hiyo hoja yako bwana, nakupa dakika tatu. Katibu hebu iweke vizuri. (Makofi)

Waziri wa Elimu amekaa vizuri anakusikiliza sasa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ndio nasema hivyo kwamba, kusema kweli mahitaji ya uchumi wetu wa sasa hivi ni watu wanaoweza kutenda na mahitaji ni kwamba watu wana magari lakini hawawezi kutengeneza, ukitafuta fundi hakuna kwa sababu hakuna mtu anayefundisha vitu hivyo na siyo tena kutengeneza magari ambayo ni ya ajabu, sasa hivi tengenezeni magari ambayo lazima zile shule zetu za ufundi na zenyewe zi-adopt mahitaji ya sasa hivi. Ukienda uka-register wanafunzi utapata wanafunzi utapata wengi sana ukitafuta kwenye electronic base industry na nini utapata, lakini ukienda kwa ile ya zamani kwamba sijui unataka mtu wa kuranda. Tuna chuo cha ufundi pale kwetu Mamba pale lakini hakuna mtu anaenda kwa sababu wana mashine za kuranda wanafundisha kuranda au cherehani za kushona lakini ni zile za zamani sasa hivi kuna cherehani za kisasa.

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema hivi kwa kule kwetu kama anavyosema Mheshimiwa Saashisha, kusema kweli zao la kahawa limedorola sana na nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais aliweka hilo pia katika zao la kimkakati. Hata hivyo, niseme hivi kule Kilimanjaro ile ardhi imeshadidimia haifai tena hata kulima kahawa, utatumia madawa mengi na watu hawajui kutengeneza composite, kwa hiyo unakuta kwamba ile kahawa ukiipeleka kuuza nje tena hupati hata wanunuzi. Halafu bahati mbaya pia vile vihamba vyetu, yale mashamba yetu yamekuwa tragmented mtu mmoja ana robo heka, atalima wapi.

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi, sisi Wachaga wengine tunataka tuhamie mahali ambapo kuna ardhi, tukalime huko, mambo ya kusongamana kule haifai na wameniomba wananchi wangu wa Vunjo kwamba jamani ukienda tafuta mahali utakakoweza kutupeleka tukalime tupate eneo tulime na sisi tuwe na tija, tuwe na mabilionea na sisi, lakini kusema kweli kule Uchagani huwezi kuwa bilionea kwa sababu hakuna ardhi. Watu wa kule Vunjo tuna shida hiyo na nitakuja kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, atusaidie.

Mheshimiwa Spika, mwisho, niseme hivi katika rasilimali tuliyonayo sisi kule Kilimanjaro, ni mlima Kilimanjaro na ni kweli wana Vunjo na wengine wote wanaozunguka ule mlima wanapata shida sana. Shida kubwa ni kwamba ajira haipatikani, vijana wengine wanaokuja kupata ajira kule ni kutoka maeneo mengine, lakini hata wale wanavijiji wanaozunguka ule mlima, ile nusu maili hawaruhusiwi kutumia, siku hizi wanapigwa, walikuwa wanasema ni wanawake tu waende huko, sasa wanawake wakaenda wenyewe, baadaye na wenyewe wakanyimwa kwenda huko kutafuta kuni, kutafuta majani ya ng’ombe na mbuzi na kadhalika. Sasa tunamwomba Waziri wa hifadhi naye atuangalizie hilo na ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Spika, mambo ya barabara yameshazungumza sana. Naunga mkono hoja ya kuongeza Mfuko wa TARURA, kusema kweli barabara zetu zina matatizo japokuwa hata zile ambazo zinatakiwa ziwekwe lami zimeahidiwa lami tunazo hizo kama tatu hivi ambazo Mheshimiwa Rais naye alituruhusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Naona kengele imelia.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kimei, tunakushuru sana…

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa moyo moja na sisi tutatekeleza kila jambo ambalo liko kwenye hotuba hii. (Makofi)