Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu hotuba mbili za Mheshimiwa Rais. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri za kuendelea kulitumikia Taifa letu, lakini pia mipango yake mizuri ambayo wananchi ilikuwa ni tarajio lao.

Mheshimiwa Spika, hotuba hizi mbili zimeligusa Taifa, lakini limegusa jimbo langu katika kila nyanja. Mheshimiwa Rais alizungumzia uboreshaji upande wa sekta ya elimu. Kwa kweli elimu inaendelea kuboreshwa na kuendelea kupunguzwa changamoto ambazo ziko katika maeneo mbalimbali kwenye shule zetu ikiwa ni pamoja na kuwaondosha watoto wetu kukalia matofali pamoja na mawe. Ametoa agizo Mheshimiwa Waziri Mkuu na tunaendelea kutekeleza kuhusu masuala ya wanafunzi wetu kukamilisha madawati pamoja na madarasa.

Mheshimiwa Spika, lakini bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinakabili sekta hiyo hususan upande wa Nyang’hwale Waziri wa Elimu alichukue hili kwamba tuna upungufu mkubwa wa walimu hasa wa sayansi. Pia bado tuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu pamoja na vitendea kazi. Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la kupunguza kero ya akinamama kufuata maji mbali, kupunguza kero hiyo vijijini pamoja na mjini. Nashukuru kwamba sekta ya maji imepiga hatua kubwa ikiwemo Jimbo la Nyang’hwale, tuna mradi mkubwa ambao tulitengewa fedha zaidi ya bilioni 15.

Mheshimiwa Spika, mradi huu Waziri wa Maji atakuwa yupo, ajue kabisa kwamba mradi huu unakwenda kwa kusuasua, umechukua muda mrefu na tarajio kubwa la wananchi wa Nyang’hwale kupate maji kutoka Ziwa Victoria ni kiu chao kikubwa sana. Leo tumekuwa tukiahidiwa kwamba mradi huu utakamilika ndani ya miezi mitatu, ndani ya miezi miwili, lakini mradi huu haufikii mwisho. Wananchi wetu wanaenda wanapoteza imani kubwa na Wizara hii Maji kwa sababu ahadi hiyo inakuwa haikamiliki.

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu wamezungumzia mtoto huyu TARURA, TARURA fedha zake inabidi ziongezwe tumekuwa na changamoto kubwa sana ya barabara kwenye halmashauri zetu, lakini TARURA amekuwa hawezi kukidhi kurekebisha barabara hizo kutokana na uchache wa fedha. Kwa hiyo, naungana na wenzangu kwamba hoja hii ya kumwongezea mtoto huyu wa TANROADS, TARURA aweze kupata fedha kuweza kukidhi shida mbalimbali zilizoko kwenye maeneo hususani kwenye halmashauri zetu ikiwemo Nyang’hwale; barabara nyingi zimeharibika TARURA hawezi kutokana na kiwango kidogo cha fedha ambacho anapewa.

Mheshimiwa Spika, hotuba hizi zimegusa maeneo mbalimbali imegusa upande wa umeme, kuboresha umeme kuongeza uzalishaji wa umeme ili sasa tuweze kuwa na viwanda na umeme wa uhakika. Nampongeza sana Waziri wa Nishati, juhudi kubwa zinafanywa huko vijijini lakini bado kuna changamaoto. Nitazungumzia upande wa Jimbo langu, ni vijiji 62 lakini mpaka sasa hivi vijiji ambavyo vimeshawashwa havijazidi hata nusu. Yeye amesema hapa nilivyomsikia kwamba bado miezi michache vijiji vyote vya Tanzania vitakuwa vimekamilishwa umeme, sasa sijui na Nyang’hwale vitakuwa vimekamilika? Kwa hiyo, changamoto ya umeme Jimboni kwangu bado ni kubwa kuna maeneo mbalimbali nguzo zimesimikwa na mashimo yamechimbwa lakini waya ndiyo tatizo kubwa. Mkandarasi wetu kila unapoongea naye anasema tatizo kubwa ni la nyaya. Kwa hiyo, namwomba Waziri wa Nishati awasiliane na huyo mkandarasi aelewe tatizo ni nini. Si changamoto tu ya umeme kwa wilaya ya Nyang’hwale, ni maeneo mengi kwa hiyo, Waziri wa Nishati ajaribu sana kuangalia wakandarasi wake ili waweze kwenda na wakati.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo kuimarisha usafiri wa anga, leo Tanzania tunajivunia usafiri wa anga, tuna ndege zetu ambazo zimeshakuja na zingine zinakuja na kwa kweli zimeleta faida kubwa, zimeleta sifa kubwa kwa nchi yetu, lakini pia Rais wetu kafanya kazi kubwa maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, muda wa hutoshi nataka nizungumzie suala la upande wa kilimo; wakulima wetu wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo pembejeo ambazo zinakuja mbovu, hazifai lakini changamoto nyingine kubwa ni soko la uhakika. Waziri wa Kilimo yupo, wananchi wetu mazao yao sasa hivi yapo hayana thamani, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, ajaribu kuliangalia sana suala hili la kuzuia upelekaji wa vyakula nje, wananchi wetu leo hii wanahangaika kupata fedha kwa sababu ya zuio hilo la kuzuia kupeleka chakula nje.

Mheshimiwa Spika, najaribu kuangalia leo hii jimboni kwangu debe la mahindi mpaka sasa hivi linauzwa shilingi 7,000, mkulima huyu atatoka vipi hapo alipo debe la mahindi shilingi 7,000 lakini kama kungekuwa soko la nje naamini kabisa asingeweza kuuza debe la mahindi shilingi 7,000. Kwa hiyo, Waziri wa Kilimo ajaribu kuliangalia hilo zuio, sawa lina wakati wake hilo zuio, kama hali ya hewa ya chakula si nzuri, waweke hilo zuio, lakini kwa sasa hivi hali ya hewa ni nzuri na wakulima wetu wanapata vyakula kwa wingi ili waweze kutoka hapo, basi tunaomba soko hilo liweze kufunguliwa kuweza kupeleka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu Mheshimiwa Rais alivyokaa na wachimbaji wa madini mbalimbali, kwa kweli hamasa imekuwa ni kubwa na pato la nchi limeongezeka, lakini bado kuna changamoto ziko kwa wachimbaji wetu wadogo wadogo. Nitazungumzia wachimbaji wadogo wadogo walioko Wilaya ya Nyang’hwale, wana maeneo ambao wameyavumbua lakini inakuwa ni tatizo kubwa la kuweza kuwapatia leseni. Kuna maombi mbalimbali ambayo yameombwa kwa wachimbaji wetu wadogo ili waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji lakini leseni zenyewe kutoka inakuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Madini kwa sababu yupo hapa namwomba sasa, wachimbaji wadogo wa Wilaya ya Nyang’hwale wamekuwa na changamoto ya kupata huduma za Ofisi ya Madini kwa sababu Ofisi ya Madini inakuwa iko mbali, zaidi ya kilomita 90. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Madini aweze kuangalia namna gani ya kufungua Ofisi ya Madini pale Makao Mkuu ya Wilaya ya Nyang’hwale Kharumwa ili hawa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini waweze kupata huduma hiyo karibu hapo na kuweza kusababisha kuzuia mianya saa nyingine ya kuweza kutorosha madini haya. Mtu anapotoka eneo moja kwenda eneo lingine inawezekana kuna jambo liko pale katikati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Madini naomba ulichukuwe hili ili uweze kuwasaidia wachimbaji wa Nyangh’wale kwa kuwasogezea huduma. Nimeshalizungumza sana suala hilo.

Mheshimiwa Spika, bila kukuficha Mheshimiwa Waziri wa Madini, Nyangwale wamemuunga mkono sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, sasa hivi utoroshaji wa madini asilimia 98 nakuhakikishia haupo tena. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Madini hakikisha basi unaifungua hiyo ofisi ili kuweza kukamilisha zile asilimia 2 za wasiwasi unaweza kutorosha madini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya ardhi, Mheshimiwa Waziri wa ardhi yupo, wananchi wangu hususani wa Wilaya ya Nyang’wale wamekuwa wakienda kuomba kupimiwa ardhi zao pamekuwa na usumbufu mkubwa, njoo kesho, njoo kesho kutwa. Waziri wa Ardhi ajaribu kuwasiliana na Maafisa Ardhi wa Wilaya ya Nyang’wale ajue kwa nini wamekuwa wakiwasumbua wananchi kuhusu suala la kupima ardhi zao.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja iliyoko mbele yetu ya hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)