Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kusimama na mimi kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijalia nami kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Kumi na Mbili. Vilevile namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai wa kutuwezesha Wabunge sote kwa pamoja kuja katika Bunge hili na kuwatumikia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia katika suala la afya. Tumeona ni jinsi gani Mheshimiwa Rais ameweza kutupa dira ambayo itatufanya tufikie katika malengo ambayo tumeyakusudia. Kwa mfano, kwa mwaka 2015 tumeona kwamba mpaka kufikia 2020 Zahanati zimekukwa 1,198, Vituo vya Afya 487 na Hospitali 99.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwani alipokuwa kwenye ziara Mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Kahama, aliipandisha hadhi kuwa Manispaa na Hospitali yetu ya Wilaya ya Kahama inatarajiwa kupanda daraja. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anazidi kujidhatiti katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, katika kipengele hiki cha sekta ya afya, nakumbuka kulikuwa na mpango wa MMAM. Mpango huu ulikuwa umekusudia kila Kata kuwa na Kituo cha Afya na kila kijiji au mtaa kuwa na Zahanati. Katika Mkoa wa Shinyanga kuna zahanati nyingi ambazo zimeshafika kwenye maboma. Hivyo, nadhani ni wakati muafaka sasa, ili kutimiza azma na matamanio ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba huduma za afya zinawafikia Watanzania wengi, yale maboma yaweze kumaliziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la afya, tumeona jinsi ambavyo vifo vya wamama wajawazito vilivyopungua kutoka vifo 11,000 mpaka vifo 3,000. Hili tuna sababu kubwa sana kumpongeza Mheshimiwa Rais na watendaji wote wa Wizara ya Afya na wafanyakazi wote wa sekta mtambuka ambao wanahakikisha kwamba huduma ya afya inaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo la maji, lakini tumeona dira ambayo Mheshimiwa Rais ameionyesha katika hotuba yake na vilevile kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, nawapongeza sana Wizara ya Maji, hasa Mheshimiwa Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na watendaji wote wa Wizara hiyo ya Maji kuhakikisha kwamba mwanamke anatuliwa ndoo hasa katika Mkoa wa Shinyanga, Tabora na hata Dodoma kwa kweli sasa hivi shida ya maji siyo kama ile. Tunatarajia kwamba mradi wa Ziwa Victoria utafika na Dodoma na sehemu nyingine. Kwa hiyo, ni suala la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi ambazo kwa kweli anazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, tumeona katika suala zima la uchumi. Ukiangalia katika hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais mwaka 2015 ukalinganisha na hotuba ambayo ameitoa mwaka 2020, tunaona kuna ongezeko la pato la Taifa kutoka 7% kwa mwaka. Pia tumeona makusanyo ya mapato yameongezeka toka shilingi trilioni 94.3 kwa mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139. Hivyo tuna sababu kabisa ya kuweka mipango yetu vizuri kwa sababu tunakwenda kwenye bajeti. Katika bajeti ni lazima tuzingatie dira ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa ili tuweze kutekeleza yale ambayo Chama cha Mapinduzi na sisi Wabunge kwa ujumla tuliyaahidi wakati tunaomba kura.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuzungumzia kuhusu barabara. Barabara ni changamoto sana hasa vijijini. Hata hivyo, kwa mpango madhubuti ambao upo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, naamini kwamba kuja kufikia 2025 barabara nyingi zitakuwa zinapitika na zinafunguka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema kwamba kwa kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais, sisi kama Wabunge tuna sababu ya kumpongeza na kuzidi kumwombea kwa sababu vita ya kiuchumi ni kubwa sana. Mheshimiwa Rais naamini halali akiwaza maendeleo ya Tanzania, anatamani kuacha nchi ya Tanzania katika level fulani na anatama yale anayoyafikiria yanatimia. Hivyo, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunamwombea.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, niseme kwamba tunapaswa kuendelea kumwomba Mungu hasa katika janga ambalo lipo lakini tunapaswa kuendelea kujikinga kwa sababu Mungu wetu ni mwaminifu, kama ambavyo aliweza kutushindia kipindi kile tukaweza kuepukana na janga hili, ataendelea kutushindia. Nchi za wenzetu wanatamani kuwa na Rais kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Wanasema laiti tungekuwa tunaweza kubadilishana, basi tungeweza kubadilishana mkatupa Rais Dkt. John Pombe Magufuli hata kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, tuna sababu sanasana sana ya kumshukuru Mungu kwa sababu ya kumpata Rais huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)