Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pili nikishukuru chama changu na wananchi wa Mbagala kwa ujumla. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri ambayo kwa kweli ukiifuatilia inaenda kujibu kero za wananchi.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikijiuliza sana wakati naisoma hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Katika kila neno kwenye hotuba hii ni dhahiri linahitaji fedha ili tuweze kuitekeleza hotuba hii sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, nimekaa nikatafakari sana pamoja na matatizo mengi yaliyokuwepo katika jimbo langu, lakini nimeona mchango wangu nijielekeze sana ni kwa namna gani ambavyo naweza kuishauri Serikali namna ya kupata mapato ambayo mwisho wa siku naamini yanaenda kutekeleza hotuba hii ya Mheshimiwa Rais pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, katika kila eneo nililolisoma nimeona tuna nafasi ya kupata mapato ambayo naona Serikali tulikuwa tunayapoteza. Nianze na suala zima la miundombinu.

Mheshimiwa Spika, hotuba yote imezungumza namna ambavyo tunaenda kutengeneza barabara na miundombinu mingine. Hata hivyo, nikija katika suala la utenengezaji wa miundombinu iliyopita na inayotaka kutengenezwa, ni dhahiri kuna baadhi ya maeneo ambayo miundombinu imepita yamelipwa fidia. Baadhi ya Wabunge hapa tumeona wakisisitiza ulipwaji wa fidia kwa baadhi ya maeneo ambayo yametwaliwa na Serikali. Pia nimemsikia Waziri wa Ardhi akisisitiza suala la ulipaji fidia maeneo ambayo yanatwaliwa na umma.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa nikaona kuna fedha za Serikali zinapotea. Tunapolipa fidia hatuangalii yule tunayemlipa fidia, hana deni la land rent au property tax? Kama jukumu la kulipa fidia ile ni la halmashauri basi linaishia kulipa fidia na badaye hamna mtu anayejali madeni haya ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi kabla sijaja hapa nilikuwa Diwani katika Manispaa ya Temeke. Tumelipa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 20 lakini baadaye nikafikiria, je, hawa tuliowalipa fidia hawakuwa na madeni ya property tax au land rent? Nikaja kugundua ni fedha nyingi sana ambazo tumezipoteza kwa kutokulipa hizi property tax na land rent. Kwa hiyo, naishauri Serikali washirikiane kati ya taasisi zinazolipa fidia na Wizara ambazo zina mapato yake katika ulipwaji ule wa fidia.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, ni katika miundombinu ya ujenzi. Hotuba ya Bunge la Kumi na Moja na hili la Kumi na Mbili tumezungumzia sekta ya maji, barabara, lakini miradi hii tunaenda kuwapa wakandarasi mbalimbali. Nikawa najiuliza, je, wakandarasi hawa wanazilipa halmashauri zetu city service levy?

Mheshimiwa Spika, mimi nilijaribu pale Temeke, tulikuwa na mradi ule wa uboreshaji wa Jiji la Dar-Es-Salaam. Makampuni yote tuliowapa tenda za ujenzi zaidi ya shilingi bilioni 600 tulihakikisha zinalipa city service levy. Pato la city service levy ndiyo lilikuja kuleta maajabu ya kuweza kujenga madarasa 120 kwa mapato yetu ya ndani. Naomba niishauri Serikali maeneo yote ambayo kuna wakandarasi wanafanya kazi za ujenzi, basi tuone namna gani halmashauri zetu nazo wanaenda kuchukua city service levy zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikaiangalia Wizara ya Ardhi. Wizara ya Ardhi kuna property tax ambayo inapatikana kutokana na majengo yanayojengwa kwenye ardhi zile lakini pia kuna land rent. Halmashauri na majiji mengi zimepima viwanja lakini vinakaa zaidi ya miaka 10 havijaendelezwa; sheria ipo kwa nini Wizara ya Ardhi viwanja vile wasiwauzie watu wengine ili majengo yale yajengwe na hatimaye tuweze kukusanya property tax katika majengo yale?

SPIKA: Sheikh Abdallah utaua hapo. Wako wengi humu hapo walishaugulia tayari, endelea Mheshimiwa. (KIcheko)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, tukitaka tulete mabadiliko ya kweli basi na sisi tunatakiwa tuwe mfano katika kusababisha hayo mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye sekta ya afya, tumemsikia Waziri hapa asubuhi akisema kuna zahanati moja ilitumia shilingi milioni 40 kununua dawa na ilivyokuja kutoa huduma ikapata zaidi ya shilingi milioni 100, lakini wakaja kununua dawa za shilingi milioni 20. Ni wajibu wetu sasa Wabunge kwenda kufuatilia vitu kama hivi. Tunapofuatilia maana yake malalamiko madogomadogo yanakuwa yanapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye elimu, Serikali yetu imejitahidi sana kuboresha miundombinu ya elimu, lakini yapo makampuni yanaendeleza maeneo kwa kujenga ma-real estate. Kwa mfano, NSSF pale Tuangoma wamejenga nyumba nyingi na wakatuletea wananchi wengi lakini hatuwaoni NSSF kusema hata tunajenga shule moja tukaiita hii ni NSSF Primary School, hawafanyi hivyo. Pia hata maeneo mengi ambayo wamekuwa wakiyamiliki hawayaendelezi kwa muda mrefu. Tukiwaomba maeneo yale basi mtupe maeneo fulani tujenge shule za msingi, sekondari na vituo vya afya, nayo imekuwa mgogoro.

Mheshimiwa Spika, niombe sana, pamoja na kuichangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais lakini vilevile tupate nafasi kubwa ya kuona ni sehemu gani mapato ya Serikali yanapotea na tuweze kuyadhibiti ili hotuba hii na utekelezaji wa Ilani uende kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, nimalizie, nimeona halmashauri nyingi zikiandika miradi ya kimkakati lakini leo kwenye hotuba ya Rais nimeona kuna mazao ya kimkakati. Nikajiuliza, je, kwa nini katika ile miradi ya kimkakati halmashauri ambazo zina uwezo wa kulima zisiandike andiko la kuomba fedha ili wakalima mazao ya kimkakati ya kihalmashauri ikawa ni moja ya vyanzo vya mapato?

Mheshimiwa Spika, nitakutolea mfano mdogo tu, Halmashauri ya Lindi. Halmashauri ya Lindi imegawa maeneo kwa ajili ya wananchi kuwekeza. Katika semina ile ilikuwa inaeleza mtu ukiwa na ekari 200 ukaweza kupanda mikorosho baada ya miaka mitatu una uwezo wa kila mwaka kupata shilingi bilioni moja. Je, halmashauri ingefanya yenyewe ikatafuta mashamba yake ikachukua ekari 100, ekari 500, ikaomba fedha serikalini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. (Makofi)