Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Pia nimshukuru Mungu sana kwa nafasi hii aliyotupatia ya kuwa mahali hapa leo. Kipekee nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi pamoja na wananchi wa Jimbo letu la Busega kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao mahali hapa.

Mheshimiwa Spika, 2015 nilibahatika kufuatilia hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge la Kumi na Moja, tarehe 20 Novemba, 2015. Aliyoyasema nilianza kufikiri kwamba yanaenda kuwezekana vipi, lakini nirudishe shukrani nyingi sana kwa mapinduzi makubwa ya maendeleo aliyotupatia Mheshimiwa Rais kwa kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita. Ni Imani yangu kubwa kwamba katika hii miaka mitano kupitia hotuba yake ya tarehe 13 Novemba, 2020 ambayo ilitoa mwelekeo wa nchi yetu yapo maeneo machache naomba nami nichangie.

Mheshimiwa Spika, kuna suala toka asubuhi linaendelea kujadiliwa; habari ya TARURA. TARURA ni pasua kichwa, TARURA ni shida mpaka sasa barabara nyingi vijijini zimekatika. Pia kutokuwepo kwa barabara hizi za vijijini kumesababisha sehemu ya uchumi wa wananchi wetu kushuka kwa sababu hawawezi sasa kupeleka hata mazao yao kwenda kutafuta sehemu ambako kuna masoko, madalali wamekuwa wengi wa bei ya chini kwa sababu ya shida ya barabara ambazo ziko kwenye vijiji ambavyo sisi tunatoka.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano ukiangalia kuna wakati hata hili zao la pamba kwetu kule Usukumani ambapo wananchi wengi wanalima, inafikia sehemu barabara ni ya shida watu wa pikipiki wanakwenda kununua pamba kwa bei ya chini sana, muda mwingine hata nusu ya bei ambayo ni halisia kwa sababu ya kutokuwepo barabara sehemu husika. Tunapotaka sasa kuendeleza uchumi wa wananchi wetu mmoja mmoja lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ili wananchi hawa sasa waweze kusafirisha mazao yao ya biashara kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kupata bei iliyo salama.

Mheshimiwa Spika, nataka pia nichangie kidogo eneo la kilimo. Mimi ni muumini sana wa uwekezaji katika sekta ambazo ni productive kwa nchi yetu. Tunapokuwa tunazungumza habari ya ajira milioni nane, ni lazima tufikiri kuelekeza baadhi ya ajira katika sehemu ambazo ni productive kwa nchi yetu ikiwemo na kilimo.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye halmashauri zetu, halmashauri zilizo nyingi zina shida ya watumishi, hasa Maafisa Ugani. Wananchi wetu wengi hawapati fursa ya kufundishwa na hawa Maafisa Ugani kwa sababu hawapo kila sehemu ni shida. Hii ni sekta ambayo tungeweza kuielekezea watumishi wengi wangeweza kuwasaidia wananchi wetu ambao wanalima kwa kutumia akili zao zilezile ambazo Mheshimiwa Mbunge wa Mbogwe alikuwa anajaribu kugusia.

Kwa hiyo, mimi niseme na niombe, tunapokuwa tunaangalia suala la ajira, lazima pia tuangalie eneo hili ili tuweze kuajiri watu wengi waende wakawasaidie wananchi wetu katika suala zima la kilimo na kilimo kiwe chenye tija na tutakapopata malighafi yetu basi itatumika kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni viwanda. Eneo hili tukitaka tufanye vizuri ni lazima tuhakikishe kwamba tunapata viwanda vyetu vya ndani ambavyo vinatengeneza bidhaa mpaka mwisho. Kama ni pamba basi tutengeneze bidhaa inayotokana na pamba mpaka mwisho tupate nguo ili tuweze ku-export nguo kwenda nje ya nchi, zao ambalo tayari limekamilika kwa kutumia bidhaa zetu za ndani.

Mheshimiwa Spika, pia nataka kuongelea habari ya uvuvi, Mbunge wa Ukerewe amezungumza kidogo. Eneo hili bado lina shida, tozo ni nyingi sana kwa wananchi wetu ambao wanashughulika katika suala zima la uvuvi. Tozo ni nyingi, kuna leseni ya mtumbwi, TASAC Sh.70,000 wananchi wetu wanalipa lakini pia kuna leseni za halmashauri, kuna leseni ya mtumbwi na kuna shilingi 20,000 leseni ya mvuvi mmoja mmoja. Haya maeneo wananchi wetu wanayalalamikia sana kwa sababu tozo zimekuwa nyingi na wanashindwa kuzimudu kutokana na hali ya uchumi ambao wanao. Kwa hiyo, niombe Wizara husika waje na mpango kuona namna ya kupunguza baadhi ya tozo kwa hawa watu wetu ambao ni wavuvi ili waweze kunufaika na kazi ya uvuvi ambayo wanafanya.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie sekta ya afya. Eneo hili asubuhi limechangiwa katika hoja mbalimbali kupitia maswali. Huduma ya bila malipo kwa akina mama wajawazito, watoto na hata wazee; ni kweli kuna baadhi ya hospitali zinatoa lakini kuna shida kubwa sana ya upatikanaji wa dawa katika sehemu ambazo wananchi hawa wanatibiwa. Ama dawa MSD hazipatikani lakini hata kama zikipatikana basi mpango mzima wa kando unafanyika na kunakuwa na shortage kubwa sana ya dawa.

Mheshimiwa Spika, tumeona hata Mheshimiwa Waziri wa Afya amejaribu kwenda na hoja ya kutaka kuangalia equation tu iliyopo kati ya uwepo wa panadol na mwananchi kukosa dawa na akasema hii siyo simultaneous. Mimi nimpongeze kwa namna ya pekee sana kwa jinsi ambavyo ameamua kuja kwa kasi na kuhakikisha kwamba sehemu zetu dawa zinaendelea kuwepo na wananchi wetu wanapata dawa.

Mheshimiwa Spika, niombe sasa, MSD bado kuna shida. Tunaweza kwenda na order kubwa ya dawa na fedha ambazo tayari ziko MSD lakini MSD inakosa dawa. Niombe sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba tunaimarisha MSD ili iweze kuwa na sehemu kubwa ya kupata dawa ili wananchi wetu sasa waweze kupata dawa katika sehemu ambazo wanakuwepo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nilitaka kuchangia ni maliasili na utalii. Kuna shida kubwa sana ya tembo kusumbua na kuharibu mazao ya wananchi wetu. Nizungumzie kwa mfano kule kwangu Jimboni Busega kuna Kata za Lamadi, Mkula kwa maana ya Kijereshi, kuna shida kubwa ya tembo. Katika mwaka uliopita 2020, zaidi ya wananchi wanne wameuawa na tembo kwa sababu ya kukaa katika kata hizo ambazo nimeweza kuzitaja.

Mheshimiwa Spika, kuna haja kubwa sana ya kuimarisha ulinzi wa wanyamapori kupitia maaskari wetu. Ninajua Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofika pale kwenye jimbo langu aliahidi kutupatia askari 26 ili waongeze kuimarisha ulinzi wa wanyamapori na hii itatusaidia sana wananchi wetu kufanya kazi zao wakiwa na amani. Sasa kwa sababu mazao yao yanaharibiwa tunawapa tena wakati mgumu wa kupata mazao ili waweze kunufaika na mazao yao.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)