Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hotuba hizi mbili za Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, lakini leo naziite alama za Mheshimiwa Dkt. Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amechora ramani ya maendeleo ya nchi yetu na katika ramani hiyo, ameweka alama na alama hizi ndizo tunazozifuata sisi. Alama ya kwanza ni umeme wa REA. Anasema ameweka umeme katika vijiji 9,884 na vimebakia vijiji 2,000 tu. Alama ya pili pia anajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji; pia ameweka miradi ya maji 1,422 na vijijini asilimia 70 na mijini asilimia 80. Mfano huu ni Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria katika Mji wa Tabora, Igunga na Nzega na mradi huu umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alama nyingine ni elimu bure kwa Watanzania. Watoto wote wa Kitanzania, darasa la kwanza mpaka form four. Pia anajenga vituo vya VETA na hivi vinakuza uchumi. Zamani ilikuwa ukiharibikiwa na gari vijijini unamtafuta fundi kutoka mjini aje atengeneze gari, lakini anaondoka na hela, vituo hivi sasa vinajenga mafundi vijijini. Majokofu, vitu vya umeme, wanachomelea ma-grill na fedha zinabaki kule, kwa hiyo, zinazunguka badala ya kurudi mjini. Kwa hiyo, tunakuza umeme vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, alama nyingine kubwa ni ununuzi wa ndege 11 kwa ajili ya Shirika la Air Tanzania. Pia kuhusu alama ya huduma ya afya, amesema katika hotuba zake hizi, Mheshimiwa Rais amejenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887; zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 99, Hospitali za Rufaa 10, Hospitali za Kanda tatu na wagonjwa kwenda nje wamepungua na kufikia asilimia 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, Jimboni kwangu kuna changamoto. Kwa mfano, Jimbo zima lina Kituo kimoja tu cha Afya na tungependa viongezwe. Kuna vituo vile tunajenga sisi wenyewe, tunaomba vituo hivi visaidiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kitaifa liko suala la Kiswahili. Wiki hii Kiswahili kimepandishwa hadhi kabisa kwamba Wizara moja tu Tanzania ilikuwa inatumia lugha ya Kiingereza katika maandishi yake, Mahakama. Juzi umetoka Mwongozo kwamba Mahakama sasa zitumie lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kutoa hukumu zake. Naona haitoshi tu hiyo, kwa sababu Kiswahili kitaanzia juu tena. Waswahili wanasema mtaka unda haneni, lakini mimi leo nanena hata kama litaharibika, watu wenye roho mbaya, ndiyo maana methali hii ipo. Nina nia ya kuleta tena hoja ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika shule zetu za msingi na sekondari. Hili litakuwa jambo zuri kwa sababu sasa hivi tutajenga Kiswahili kuanzia shule za msingi, sekondari na matumizi yake yatadumu vizuri katika taasisi zote katika mihimili yote mitatu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitasema hayo tu, nilikuwa nimekusudia kutaja hizo alama za Mheshimiwa Rais. Nakushukuru sana kwa kuniruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)