Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango uliopo mbele yetu. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wenyewe kwa sababu ni dakika tano, nijikite sana kwenye ushauri na napenda Waziri wa Fedha ajaribu sana kusikiliza ushauri wangu. Mheshimiwa Rais alituita pale Ikulu sisi kama wafanyabiashara na wadau mbalimbali kutaka kujua changamoto tulizonazo kwenye upande wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimwelezea changamoto zetu ikiwemo tatizo kubwa lililoko bandarini kuhusu TRA. TRA kule bandarini wana usiri mkubwa. Usiri huu unasababisha watu kukwepa kulipa kodi na tozo mbalimbali, lakini pia unasababisha kupoteza mapato makubwa ya Serikali. Mfano, leo hii utakwenda China ama mtakwenda China watu watatu ama wanne mnaofanya biashara ya aina moja, mnakwenda kununua mabegi kila mmoja container moja, lakini mnapofika bandarini kila mmoja analipa kodi tofauti na mwenzake, hii ni kwa nini? Wajaribu kuangalia usiri uliopo bandarini, kuna usiri mkubwa sana. Kama alivyosema yule mchangiaji mwingine, leo hii Mtanzania anaona bora kufuata mzigo Uganda na kuuleta Tanzania kuliko kufuata mzingo Dubai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Uganda mzigo unakuwa na bei ya chini kuliko Tanzania, wakati tumetumia bandari yetu, barabara yetu kusafirisha mzigo kwenda Uganda. Inakuwa hivyo kwa sababu hapa kuna utitiri wa mambo mengi, TRA wajaribu kuangalia tatizo hili lililoko bandarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine nitautoa kwa pale bandarini. Leo hii unaingia dukani ama madukani, unaingia duka moja unakwenda duka linguine, unaingia kwenye duka hili mtu anakupa bei anakwambia hii ni ya risiti ya VAT; bei hii haina risiti haya yametokana na nini? Mwanzo wa kule bandarini. Biashara nyingi leo zimekufa kwa sababu kuna double standard ya kulipa kodi, nina Ushahidi, nimeingia duka moja nikaenda nikanunua mzigo wenye thamani ya milioni 35, nikapewa risiti ya milioni 1,500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikamwambia yule mama wewe hujipendi nipe risiti iliyo kamili, sheria gani inakulinda wewe ya kutoa risiti nusu, lakini cha ajabu ni kwamba mpaka leo hii mchezo huo upo na TRA walitangaza kwamba anayenunua ahakikishe anapewa risiti na anaomba risiti, cha ajabu leo hii mtindo huu wa kununua na kuuza hakuna anayetoa risiti. Fedha nyingi za mapato ya Serikali yanapotea, lakini cha ajabu, sheria hii hatujawahi kuipitisha Bungeni ya kwamba mtu akikamatwa hajatoa risiti ama amekamatwa amenunua na hakuomba risiti atatozwa faini ya kuanzia 30,000 mpaka 1,500,000, mambo haya yamepitishwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu leo hii kuna hawa Machinga (wafanyabiashara wadogo wadogo) wanauza bidhaa zenye thamani kubwa na hawatowi risiti, TRA hawaoni kama wanapoteza mapato? Nina ushahidi nimenunua brenda ya juisi ya shilingi 120,000 kwa mfanyabiashara huyu anayeitwa Machinga hajatoa risiti, lakini leo hii ukiingia supermarket hata ukinunua pipi unapewa risiti, wajaribu kuangalia sana TRA kuna maeneo wanapoteza mapato. Ushauri wangu wahakikishe wafanyabiashara kuanzia hao wadogo, wa kati na wakubwa waunganishwe kwenye mfumo wa ulipaji kodi EFD yaani wahakikishe kila mmoja anagawiwa hiyo mashine hata bure ili aweze kutoa risiti, tuna mapato mengi ambayo tunapoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia Mheshimiwa Waziri anasema tumevuka malengo, sasa hivi tunakusanya trilioni mbili kwa mwezi. Kwa uzoefu nilionao kuna trilioni zaidi ya tano ziko kule nje, zinapotea hivi hivi. Namwomba Mheshimiwa Rais kama itampendeza, sisi wafanyabiasha ambao tunaitwa wa darasa la saba elimu, yetu ya msingi tumo wengi humu ndani, tunamiliki uchumi wetu, kama itampendeza achague angalau hata watu wawili hao wenye elimu ya darasa la saba wakawe Manaibu Waziri, upande wa Wizara ya Fedha ama Viwanda tuweze kuwashauri vizuri, haya tunayoyazungumza, kwa sababu tuko ndani ya field tunayaelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Musukuma alitoa ushauri na namuunga mkono kwamba TRA watengeneze vijarida ama vitabu vya kuonyesha uhalisi na uhalali wa kulipa kodi. Waende wakajifunze Uganda, kwa nini ukienda Uganda unataka kufuata gari, unataka kufuata TV unaambiwa na Mamlaka ya Mapato yao, ukileta TV yako utalipa bei hii. Mtu anakwenda kununua bidhaa yake kule nje anajua nikifika hapa nitalipa kiasi fulani lakini kwa TRA ya Tanzania kuna usiri mkubwa. Nasema TRA kuna usiri mkubwa lakini ni wachache siyo wote, nawapongeza wanafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba watangulize uzalendo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja, lakini na sisi wa darasa la saba muwe mnasikiliza michango yetu. (Makofi)