Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia rasimu ya Mpango. Wizara hii imeweka mambo mengi sana ambayo ni mazuri na naamini kabisa ni mwendelezo wa mafanikio ya miaka mitano iliyopita ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye rasimu hii nimeona wakizungumzia viwanja vya ndege, kikiwemo kiwanja cha Mkoa wa Mara. Kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Mara ningeishauri Serikali katika Mpango wake kipewe kipaumbele na ikiwezekana wakiangalie kwa macho ya ziada kwa sababu, kule kwetu Mkoa wa Mara ndipo alipotoka muasisi wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa hiyo, ni sehemu nzuri ambayo ingelikuwa ni ya mfano na hasa ukizingatia Mkoa wa Mara tunachangia Taifa hili pato kubwa sana kutokana na madini, lakini pia utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara tuna kiwanda ambacho kiko Musoma Mjini, Kiwanda cha MUTEX. Kiwanda cha MUTEX kimekufa muda mrefu sana. Kiwanda hiki kilikuwa kinatengeneza kanga nzuri sana na kubwa ambazo ukiangalia watu wa kule Mkoa wa Mara tumejaliwa zile kanga zilikuwa zinatutosha vizuri tu. Kwa hiyo, niseme na sasa hivi pia ni vizuri zaidi kile kiwanda kikiangaliwa kwa jicho la ziada ili kifunguliwe kwa manufaa ya kuongeza ajira kwa vijana na watu mbalimbali ambao wanaweza kupata ajira na kupunguza upungufu wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wazee wetu wa muda mrefu sana ambao wanaitwa wastaafu walifanya kazi kipindi hicho kiwanda kile kikiwa Serikalini. Wana madai yao ya muda mrefu sana ni miaka sasa, kila wanapoenda mahakamani wanakata rufaa, wanashinda, wanakata rufaa wanashinda, nimwombe sana baba yangu, Mheshimiwa mpendwa wetu sana Rais, naamini kabisa ataiangalia siku ya leo; akawaangalie wale wazee wetu wa Kiwanda cha MUTEX kwa jicho la huruma, walipwe mafao yao ya muda mrefu kwa sababu, kuna wengine wao wameshafariki, kuna wengine wamepata ulemavu, lakini hata wale waliopo hali zao sio nzuri sana. Naamini anajali wanyonge na wale ni kati ya wanyonge ambao naamini kabisa daddy atanisikiliza leo na ataenda kuwaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la maji; Mkoa wa Mara wilaya zetu zote zimezungukwa na Ziwa Victoria, lakini baadhi ya wananchi wetu wanalia sana shida ya maji kutokana na miradi mikubwa ambayo Serikali imeshaiandaa kwa ajili ya Mkoa wa Mara. Pia, kwenye rasimu nimesikia wakiitaja, kwa kweli nawapongeza sana wako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Mkoa wa Mara ni mkoa aliotoka muasisi ulitakiwa uwe mkoa wa mfano, asiwepo mwananchi hata mmoja analalamika shida ya maji. Hivyo basi, ningeomba miradi hiyo mikubwa inapopita; upite Bunda, upite Serengeti, upite Tarime, upite Rorya, upite Musoma Vijijini, upite Musoma Mjini, lakini upite maeneo yote lengo ni kwamba, kutoa haki sawa na hasa kwa wale ambao wamekaa karibu na uaridi. Wanasema unapokuwa karibu na uaridi unanukia. Sisi wenyewe Mkoa wa Mara ndio wenye uaridi ambalo ndio maji ya ziwa, pamoja na kuwa Taifa zima ni haki yetu na ni haki yao, lakini sisi hasa Mkoa wa Mara tuwe wa mfano tusikose maji nyumba hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la miradi mikubwa ya umeme. Huu mradi wa umeme umekuwa kwa wananchi na hasa wananchi wa vijijini umekuwa changamoto sana huu mradi wa umeme wa shilingi elfu 27. Wananchi kila wanapoenda kwenye ofisi zao, wanaambiwa kwamba, bajeti bado haijaandaliwa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana, pamoja na kazi nzuri anazozifanya, nimwombe aangalie hili suala kama ni bajeti sisi Wabunge tutampitishia harakaharaka ili hili suala liende kwa wananchi wakapate huu umeme wa shilingi elfu 27 kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja tu.

MWENYEKITI: Muda wetu umeisha.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)