Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, nianze kutoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambazo anazifanya. Pili nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Waziri Mkuu lakini kwa pamoja niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao wameniwezesha kufika kwenye Bunge hili kwa mara ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze kwenye maeneo mawili. Kabla sijaanza kuzungumza ni vema nikatoa shukrani kubwa sana, Jimbo la Mtwara Mjini tumepata miradi mingi sana. Tuna mradi wa Hospitali ya Rufaa ambayo itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 122, tuna barabara ya kiwango cha lami ambayo inatoka Mtwara - Masasi na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi nataka tuzungumze kuhusu Mtwara Corridor. Hii Mtwara Corridor inawezekana hatuielewi vizuri na italeta maendeleo gani. Mheshimiwa Rais amewekeza fedha kwenye bandari ya Mtwara takriban shilingi bilioni 157, lengo na madhumuni ni bandari ya Mtwara iweze kufanya kazi na ilete tija kwenye uchumi wa taifa. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais ameamua kutengeneza barabara ya kutoka Mtwara - Newala ambapo itakuwa ni kiunganisho kikubwa sana kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu umefanyika juu ya reli ya kutoka Mtwara hadi Mbambabay. Kama upembuzi yakinifu umefanyika na tunapozungumza upembuzi yakinifu ni kwamba tayari mamilioni ya shilingi yametumika kwenye kuangalia dhana nzima ya awali. Niishauri Serikali muda sasa umefika wa kutoa maamuzi ambayo yako sahihi ya kuanza kuijenga reli hii ambayo itaweza kutuletea uchumi kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi wa nchi, yako mambo matatu tunatakiwa tuyaangalie. Tunazungumzia barabara ambayo ni kiunganisho, viwanda ambacho ndiyo kiunganisho namba moja lakini lazima tuwe na watu kama hatutakuwa na watu hatutakuwa na mashamba na hatutakuwa walimaji. Kama hakuna barabara ambazo ziko sahihi hatutaweza kupitisha mazao yetu kwenye barabara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu niiombe tena Serikali, tuna barabara ya kutoka Mtwara - Dar es Salaam, kwa muda mrefu sasa imekuwa inafanyiwa service za mara kwa mara na kutengeneza barabara ya lami kilometa moja inatugharimu fedha nyingi sana. Barabara hii imekuwa inaharibika mara kwa mara kwa sababu malori yanayopita ni makubwa na yenye uzito mkubwa. Tuna kiwanda cha Dangote, cement yote zinasafirishwa kwa njia ya gari. Tuna zao la korosho ambapo zote zinasafirishwa kwa njia ya barabara. Tumejenga bandari na tumewekeza pale shilingi milioni 157 ni kitu gani kinashindikana bandari ya Mtwara isifanye kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la elimu ni vema nikampongeza sana Mheshimiwa Rais. Tunapozungumzia elimu bure kwenye shule za msingi na sekondari suala hili limeleta chachu kubwa kwa wananchi kwa ujumla wake. Hata hivyo, ni vema nikasema kuna mgawanyiko katika fedha ambazo tunazipeleka kwenye shule za sekondari na msingi. Mwanafunzi mmoja shule ya msingi anapelekewa Sh.6,000 na mwanafunzi mmoja kwenye shule ya sekondari anapata Sh.10,000…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga

MHE. HASSAN S. MTENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dooh, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)