Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili kuchangia leo Mpango wa Tatu. Kwanza kabisa nianze kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Msalala. Lakini pia leo nitachangia katika maeneo matatu; eneo la kwanza nitachangia eneo la kilimo, na eneo la pili nitachangia eneo la madini na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Taifa hili. Kila mmoja ni shahidi wa mambo ambayo kimsingi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ametufanyia sisi Watanzania. Tuna haja kubwa ya kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Msalala limegawanyika katika maeneo mawili; eneo la kwanza ni kilimo. Asilimia 50 ya jimbo langu ni kata ambazo kimsingi zinafanya shughuli za kilimo, lakini kumekuwa na tatizo katika suala zima la utoaji wa vibali ambacho kitawaruhusu wakulima hawa baada ya kupata mazao mengi waweze kusafirisha kwenda kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliowekwa na Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanaweza kuomba kibali kwa kutumia njia ya mtandao. Ni ukweli usiopingika kwamba katika maeneo yetu, hasa ukizingatia maeneo ya Kata za Mwaluguru na Mwanase, ni maeneo ambayo hayana mawasiliano. Nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Waziri wa Kilimo waweze kuona namna gani wanakwenda kushirikiana na Waziri wa Mawasiliano ili kuweza kuhamisha mawasiliano ambayo yatawafanya basi sasa wananchi hawa, wakulima hawa, waweze kupata huduma ya mtandao ili waweze ku-apply kibali hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe sasa Wizara iweze kubadilisha utaratibu huu wa wananchi kuomba kibali kwa kupitia njia ya mtandao, kwani tunaamini kuwa wananchi wengi hawawezi kuingia kwenye mtandao na kujaza taarifa za kuomba kibali hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba kwa sasa kumeibuka tabia ya kwamba kila maeneo wanaweza kuanzisha mazao mbalimbali ikiwemo korosho na mengine. Niseme tu kwamba sisi wananchi wa Shinyanga ni wakulima wa zao la pamba, lakini kumeibuka tabia ya sasa hawa Maafisa Kilimo kuanza kutuletea mazao mapya. Niombe Waziri wa Kilimo yuko hapo, Naibu Waziri wa Kilimo yuko hapo, waone namna gani sasa wanaweza wakahakikisha kwamba wanatu-support ili tuweze kwenda kwenye kilimo cha pamba kwa kutupatia fedha na mitaji na matrekta yetu yaingie kwenye zao la kilimo cha pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la madini. Jimbo langu la Msalala ni jimbo ambalo kimsingi lina Mgodi mkubwa wa Bulyanhulu. Nimwombe Waziri wa Madini yuko hapo, Mheshimiwa Doto Biteko, kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha ya kwamba wameweka makubaliano na Kampuni ya Twiga. Ni ukweli usiopingika kwamba wanasimamia vizuri shughuli hizi za madini na usimamiaji wa utoroshaji wa madini. Hata hivyo, nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba kampuni hii kwa sasa nadhani imeanza kuja na mfumo mwingine ambao kimsingi kama Taifa tunakosa mapato lakini kama halmashauri tunapoteza fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hii imeanzisha kampuni mbili ambayo moja iko Marekani inaitwa TSL. Uwepo wa kampuni hii Marekani kama Taifa tunapoteza mapato. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kampuni hii ipo USA maana yake kazi kubwa ya kampuni hii ni kutangaza tenda tu na zabuni mbalimbali katika makampuni makubwa makubwa. Kwa nini kampuni hii isweze kurudi hapa nchini, Makao Makuu yake yakawa Dar es Salaam ili kama nchi tuweze kupata mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Kampuni hii imeanzisha mtoto wa kampuni ambayo inaitwa TSR Service, iko Dar es Salaam. Uwepo wa Kampuni hii Dar es Salaam inatufanya Halmashauri kupoteza zaidi ya shilingi bilioni 20 fedha za Service Levy. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kushirikiana yeye na Waziri wa Viwanda waone ni namna gani sasa wanaweza kuzishauri kampuni hizi ziweze kuja kuwekeza na kuanzisha ofisi zao katika maeneo ya kazi hususan Bulyanhulu. Uwepo wa kampuni hii Dar es Salaam unasababisha ukosefu wa ajira kwa wananchi wetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)