Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii nami niweze kuchangia rasimu ya Mpango iliyowasilishwa hapa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Ni dhahiri kwamba, Waheshimiwa Wabunge wamechangia hapa, lakini nataka tu niweke kumbukumbu sawa hasa katika masuala haya ya mipango kwa maana ya tunapopanga, maana tunasema kupanga ni kuchagua, lakini mipango yote hii ni mizuri na Serikali yetu imeendelea kuitekeleza; mingine imetekelezeka, mingine bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri katika eneo hili la Tume ya Mipango. Tunapopanga lazima tuwe na Tume ya Mipango iliyo imara sana. miaka ya nyuma kulikuwa kuna Wizara kabisa inayoshughulikia masuala haya ya mipango, sasa hivi Tume ya Mipango ni Idara ndani ya Wizara ya Fedha. Tafsiri yake ni kwamba, kama hakutakuwa kuna coordination, monitory and evaluation, tathmini na ufuatiliaji wa mipango yote tunayotaka kuipanga katika kipindi cha mwaka mmoja ama miaka mitano, itakuwa ni kazi bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Mipango ndio mpango mzima wa kutekeleza mipango hii ambayo tunategemea kuifanya. Kwa mfano mwaka 2010, mfano tu rahisi, Wizara ya Kilimo kipindi hicho pamoja na Wizara ya Maji walijenga vituo katika maeneo mengi nchini, zaidi ya vituo 200 na zaidi, hata kule jimboni kwangu kipo kimetumia zaidi ya milioni 900, hivi ninavyosema ni gofu, hakiendelezwi kiko vilevile tu. Maana yake thamani ya fedha iliyowekezwa pale haina tija kwa wananchi wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo lilikuwa zuri tu kwamba, wananchi itakuwa ni kituo cha kwenda kumwagilia pamoja na kujifunza mambo ya kilimo, lakini kimetelekezwa. Kimetelekezwa kwa sababu gani, hakuna muunganiko kati ya sekta moja na sekta nyingine ili kuishirikisha hiyo mipango na hatimaye iwe endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nichangie ni suala la elimu yetu ya Tanzania. Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa elimu yetu ya Tanzania asilimia kubwa ni theory zaidi na sio practical kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu. Naweza nikatoa mfano rahisi tu, kuna mwenzangu mmoja ambaye nilisoma naye zamani, tulikuwa tunasoma computer science, lakini computer science hiyo computer yenyewe tumekuja kuiona mwaka wa tatu, ndio computer hata kuifungua, hebu imagine. Tafsiri yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake tulikuwa tunafanya ma-intergrations mengi, ma-theory, lakini practical ile yenyewe ile hatukuwa tunafanya. Kwa hiyo, niombe Wizara ya Elimu kwamba, sasa ni wakati wa kubadilisha mitaala yetu ya elimu. Ndio maana nchi zilizoendelea kama China wamewekeza sana katika ufundi na huku na sisi tumeanza kujenga vyuo vya ufundi ni jambo jema, lakini huko technicians wale ndio wataalam hasa. Hata akiwepo engineer mmoja, lakini technicians kwa wingi zaidi ndio mpango mzima kwa maana ya kutekeleza yale ambayo tunategemea yawe. Kwa hiyo, mfumo wetu wa elimu kuna haja kubwa sana ya kufanya transformation, tusipofanya hivi hawatakuwepo watu wa kusimamia na ambaye atajituma. Maana kila mmoja ukiwa na degree unategemea atakuwa bosi wa nani juu ya nani? Sio rahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la mfumo wa elimu ndio linasababisha pia changamoto katika ajira kwa vijana. Kwa mfano South Africa wana mfumo mmoja unaitwa YES. YES tafsiri yake ni Youth Employment Service, una accommodate wanafunzi wote wanaomaliza vyuo vikuu na vyuo vya kati kwenda kwenye taasisi binafsi. Namna gani inafanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko namna hii; Rais wa nchi ile Cecil Ramaphosa alipokuwa ameuzindua lengo lake kubwa ni kwamba, badala ya vijana katika matangazo mengi ya kazi ambayo yanahitaji pengine uzoefu wa miaka mitano, uzoefu wa miaka kumi na hawa ndio wametoka ku- graduate wametoa wapi huo uzoefu; kwa hiyo, ikabidi waanzishe mfumo ambao utakuwa rahisi kuwachomeka kama vile field wanapokwenda. Wanakwenda katika kampuni, wanakwenda katika taasisi, wanakwenda katika mashirika, lakini unaratibiwa na Serikali na Serikali kazi yake ni kuwezesha hizo kampuni ama hizo taasisi ama sekta binafsi, ili sasa wale vijana ambao wanakwenda kusoma kule au wanakwenda kujifunza kazi kule baada ya muda fulani watakuwa tayari wamepata experience na kazi inapotokea Serikalini ama binafsi wao wenyewe ndio watakaokuwa wa kwanza kuajiriwa badala ya hivi tulivyo kwa sasa kwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda sio rafiki sana, lakini nitaandika kwa maandiko suala la uchumi wa kidigitali. Namna gani Tanzania tunaweza tukaneemeka na uchumi wa kidigitali. Ahsante sana. (Makofi)