Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia leo hii kuhudhuria kwenye Bunge lako Tukufu salama usalimini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sina budi pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri wa Fedha kwa uandaaji mzuri wa mapendekezo haya ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi pia kipekee kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa mno aliyoifanya kwa ajili ya kulisimamia Taifa hili la Tanzania kusonga mbele kimaendeleo. Ingawa wapo watu wachache ambao ndiyo wanaomrejesha nyuma Mheshimiwa Rais, lakini bado anaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Waziri wa Fedha, uchambuzi na ushauri wangu utajikita katika maeneo makuu matatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza nitajikita zaidi kuhusiana na kupanda bei kwa vifaa vya ujenzi. Sasa hivi tumeshuhudia upandaji bei wa holela. Tokea kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2020, bei ya cement imepanda mno. Kwenye hili halijaathiri tu sekta binafsi, lakini hata sekta ya umma pia imeathiriwa mno. Sasa hivi tumeshuhudia cement inauzwa kwa shilingi 17,000/= mpaka shilingi 20,000/=. Kwa kweli Watanzania wanaumia sana. Haiumizi tu kwa huku Mainland, lakini hata kwa upande wa Zanzibar pia wanaumia. Wapo wafanyabiashara ambao wanachukua cement kutoka Bara kupeleka Zanzibar; kwa bei hii ya shilingi 17,000/= ikifika Zanzibar ni bei kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika kuja kufanya majumuisho atupe majibu, amechukua hatua gani, au atachukua hatua gani kwa ajili ya kudhibiti upandaji holela wa bei ya cement? Siyo cement tu, nondo nazo zimepanda sana; gypsum powder nayo pia imepanda sana; misumari na bati, halikadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana atakapokuja Mheshimiwa Waziri atupe majibu na mikakati ambayo ipo kwa ajili ya kudhibiti huu upandaji holela wa hii cement ambayo imemuathiri sana Mtanzania katika pato lake la kawaida. Siyo kuathiri tu katika sekta binafsi, hata sekta ya umma, kwa maana ya Serikali. Sasa hivi Serikali inapoendesha miradi yake ya kimaendeleo, hununua cement kwa bei ghali sana, inasababisha kukwamisha utendaji mzuri wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo la pili ambalo ni muhimu sana kwa sasa hivi katika nchi yetu ambayo tayari tunaendelea kwenye uchumi wa kati. Bado hatujajipanga na hatuna mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba Serikali inakusanya mapato kupitia digital economy. Kwa sasa hivi, nadhani sote ni mashuhuda, Waheshimiwa Wabunge tunatumia mitandao ya kijamii. Wapo wafanyabiashara wengi sasa hivi hawanunui bidhaa zao kuingiza madukani, wananunua bidhaa ile kuweka kwenye stoo na wakauza biashara yao kupitia mitandao ya kijamii. Wanatumia WhatsApp, Instagram, Facebook na mitandao tofauti tofauti. Hata hivyo, bado sijaona wazi kabisa Serikali kusimamia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wafanyabiashara wanawasiliana na mteja moja kwa moja kwa maana kwamba seller na customer wanashirikishwa kwa pamoja wanawasiliana wapi nikuletee mzigo, nikikutumia mzigo Dodoma utatoa pesa ya usafiri shilingi 1,000, lakini Serikali bado haijatambua hizi technic ambazo sasa hivi zinatumiwa na wafanyabiashara. Hii inasababisha Serikali kupoteza gharama kubwa sana kwa ajili ya kuwachaji hawa wafanyabiashara. Hivyo, naiomba sana Wizara hii pamoja na wataalam wetu wa Serikali kuhakikisha sasa wanaweka mipango madhubuti na mikakati ili mradi fedha za Serikali zisipotee kupitia uchumi huu wa digital economy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa hivi tuna wasanii, tuna watu mashuhuri kwenye nchi hii ya Tanzania na wanatumia mitandao ya kijamii, kwa mfano, tunao wasanii wakubwa wanapata fedha kupitia you tube; msanii analipwa pale ambapo ana watazamaji wengi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Usonge.

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)