Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano ya nchi yetu. Na nitajikita katika maeneo matatu, maji, kilimo, uvuvi na la nne elimu kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji tumeiona kwenye taarifa hapa kwenye Mpango mzima kwamba imekamilika mingi lakini mingi bado haijakamilika. Lipo tatizo kubwa, miradi mikubwa imefanywa lakini baadaye inaharibika, hali hii ni kwasababu kubwa moja tu, mradi kwa mfano wa Ziwa Victoria umegharibu karibu shilingi bilioni 617 halafu baadaye umekabidhiwa kwa CBOs wa uendeshe. Hauna fundi, hauna mtaalam yeyote na miradi mingine kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Chuo cha Ufundi wa Maji pale Dar es Salaam, lakini bahati mbaya chuo kile kimetelekezwa na ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Serikali na Wizara ya Maji, Chuo kile kifufuliwe ili kifanye kazi iliyokusudiwa. Kutengeneza mitambo ya maji, tumeshaacha mambo ya visima sana lakini miradi mikubwa ya maji haiwezi kukabidhiwa kwa watu ambao hawajui ufundi wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani tukajenga shule, tukawakabidhi watu ambao sio walimu, haiwezekani tukajenga zahanati tusiwakabidhi madaktari n.k. Hata barabara tunajenga tunawakabidhi wahandisi kuitengeneza. Miradi mikubwa ya maji iliyokamilika mingi yake haifanyi kazi kwasababu haina wataalam wakuendesha mitambo ile ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kumekuwa na matatizo makubwa sana, tunasema maji yako vijijini asilimia 85 lakini sijui wanapima pimaje kwasababu kuna sehemu nyingine maji hakuna kabisa, hakuna, wanasema asilimia 85 au 75. Nafikiri upimaji wa upatikanaji wa maji wa vijijini na mijini pia uangaliwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la kilimo ambalo nilisema nitaligusia. Tanzania nzima tunalima kilimo cha kudra ya Mwenyezi Mungu, yaani mvua inyeshe na isiponyesha hatupati; ukame ukija hatupati. tuachane na suaLa hilo la kizamani. Duniani kilimo kikubwa kinachokusudiwa kuleta tija ni kilimo cha umwagiliaji. Pale kwetu Tabora kuna mbuga kubwa na maji mengi, mvua ikinyesha tunakazana kujenga madaraja maji yapite. Hatuyazuii yale maji yakawa mabwawa ya kumwagilia, tumekazana kufungua madaraja makubwa maji yapite, yaende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hapa Dar es Salaam, tunafungua daraja lile la Magomeni pale maji yapite yaende baharini. Maji yale yangeweza kutumika kwa umwagiliaji mkubwa sana. Kwa hiyo, kilimo hiki cha kudra ya Mwenyezi Mungu hakiwezi kutuvusha. Tunataka kilimo kile ambacho kitaleta tija kwa kupima. Tuna maji haya, ekari hizi tutazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Kilimo sasa ijikite katika umwagiliaji. Mbuga kubwa kubwa zilizopo hapa zimejaa maji, baadaye maji yanakauka na jua, yanapotea wakati tungeweza kuzalishia chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uvuvi. Nchi yetu imezungukwa na mabwawa, maziwa na bahari, lakini hatupati chochote kikubwa kinachoweza kuingizwa kwenye uchumi wa nchi kutokana na samaki. Pia, ufugaji wa Samaki; nimetembea, nimeangalia huko na huko, tunajaribu hapa na pale, lakini pia hata wavuvi wenyewe wanaotakiwa kuvua samaki wanatungiwa sheria ngumu sana, wavue samaki usiku tu, wasivue samaki mchana, wavue samaki kwenye maji machache yenye mita fulani mengi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko tatizo la kuwekeza katika uvuvi wa samaki. Tulikuwa na meli na Shirika letu la TAFICO, likauzwa na bahati mbaya sana likauzwa kwa watu ambao hawakuwa na tija na nchi yetu hii na hilo Shirika likafa. Wakati linakufa lilikuwa linaingiza mabilioni. Sasa ndilo kiungo peke yake; katika bajeti hii nimeona kwamba kuna meli zinanunuliwa kwa ajili ya kufufua uvuvi. Meli tano zitakuwa Tanzania Bara na nne zitakwenda Tanzania Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, meli hizi kiungo chake kiwe Shirika la TAFICO ambalo lilikuwa na wataalam wazuri, lilikuwa na taaluma na mitambo mizuri, yaani majengo yake. Majengo yameshaoza na kadhalika. Naomba sana Serikali ionyeshe umuhimu wa uvuvi ili tupate hela kutokana na uvuvi unaoitwa uchumi wa bluu. La sivyo, tunakuwa tunasema, wenzetu wanafaidika. Meli kubwa kubwa zinavua tu na kule, zinaondoka nao. Sisi tumekalia; tutauza hili, tutauza hili. Naomba sana ndugu zangu, Waziri wa Uvuvi na Mifugo ajitahidi sana kuleta tija katika uvuvi ili Serikali ipate mapato ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu. Waziri wa Elimu naona atanichoka maana nimekuwa nasema. Elimu yetu iendane na Sera yetu ya Viwanda na Biashara. Tunataka kukuza viwanda; viwanda haviwezi kuendelea bila kuwa na mafundi. Mtu ananunua mashine mpya analeta hapa nchini, halafu baadaye zinakufa, hakuna mafundi. Zamani tulikuwa tukileta mafundi kutoka nje. Sasa kila mtu anashangaa, shule zote hizi, vyuo vyote hivi, kimetokea nini? Limetokea tatizo dogo tu, tumejenga gap kati ya Wahandisi ambao ni white colors na wale walioko chini ma-artisan. Wanaofanya kazi ni hawa FTC technicians. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu iandae upya sera itakayowarudisha Mafundi Sanifu au Fundi Sadifu ili waunganishwe na mafundi Artisan au Fundi Mchundo na Wahandisi. Sasa hivi nchi hii inazalisha Wahandisi wengi ambao sio Watendaji kazi, ni wafikiriaji, wanataaluma kuliko watendaji kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko kwenye sekta binafsi na ninaajiri mafundi. Ukichukua mafundi kutoka Chuo Kikuu na Vyuo vingine, wako juu, lazima umpe na Idara maana ni Mkuu wa Idara. Watu gani watafanya kazi viwandani huku chini? Utamtuma nani? Ukimtuma mtu wa chini kabisa, vitu havielewi. FTC hapa hawapo. Chuo cha Ufundi (Technical College) kilikuwa ni branch ya TFC. Rudisheni hiyo ndiyo itatupeleka kwenye viwanda. La sivyo, viwanda vitazorota vile vile. (Makofi)

(Hapa kengele ililiakuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, najua kengele ya kwanza hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya nayasema yananisumbua sana. Sisi huko, waajiri tunapata taabu kuajiri watoto wanaotoka shuleni hapa Tanzania. Unamweka wapi? Matokeo yake tumekuwa tunafungua kampuni tunaleta maombi ya kuajiri skilled people kutoka nje. Wenzetu kule nje wameendeleza polytechnic ambayo inasuka watoto wote kuanzia engineer, FTC na artisans. Sasa hili linatupa taabu sana. Nawaombeni sana, niseme namna gani sijui mnielewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri wa Elimu nifikirie. Usifikirie ulikotoka wewe, form one, form five, form six, chuo kikuu. Hiyo ni linIe moja tu. Kuna line nyingine inaanzia Technical School, Technical Secondary School, Technical College, ina-produce engineers, watendaji kazi. Mwifikirie hiyo ambayo ilifutwa, irudishwe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine muhimu sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, juzi ameligusa, anasema Kiswahili tunafundisha kama lugha. Mimi nilimwelewa sana. Lugha ya kufundishia iwe Kiswahili, kwa sababu watoto tunafundisha darasa la kwanza mpaka la saba, Kiswahili; halafu tunabadilisha kinakuwa Kiingereza, lakini kuna kitengo fulani cha Walimu wanafundishwa Kiswahili Chuoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mchanganyiko wa kufundisha watoto wetu haueleweki. Wanafika vyuoni kule wanaanza kujifunza lugha kwanza Kiingereza ndipo waanze kujifunza masomo. Tunawakata elimu mara mbili; kujifunza lugha na kujifunza taaluma. Tunapoteza muda nusu nusu, kama wamekaa miaka mitano au minne shuleni, walikuwa miaka miwili wanajifunza lugha. Wote duniani hakuna mtu aliyeendelea kwa kutumia lugha ya mwenzake. Lugha ya mama ndiyo inayomfanya mtoto aelewe. Vinginevyo watoto hawaelewi shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshatoa mifano mingi sana hapa kwamba, elimu na lugha ni vitu viwili tofauti. Tunasema, mtoto anaongea Kiingereza kama maji, kasoma sana yule! Hajui hata mbili kuongeza mbili, ila anaongea Kiingereza kama maji. Ni tofauti na mtoto ambaye hajui chochote katika lugha; anajua kujumlisha hesabu, anajua maarifa. Tutofautishe kati ya maarifa na lugha. Bado naahidi na bado nina nia ya kuleta hoja yangu binafsi Bungeni humu ya kutaka Kiswahili iwe lugha ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.