Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kipekee namshukuru Mungu sana kutuweka hapa ili tuongee masuala muhimu haya kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, amani, amani, amani, nikiuliza hapa mna amani? Wote mtasema ndiyo na ndiyo maana mko chini ya jengo hili mkisikiliza na mkitafakari na mkifanya kazi nzuri hizi kwa wananchi wenu. Amani ni kitu muhimu sana kwa mtu mwenyewe kwenye nafsi yake na kwa mtu na watu wake na Taifa na viongozi wa juu na wananchi wao.

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kuzungumza machache. Mimi ni mjumbe wa Kamati hii na mashahidi ninaowazungumzia ni wajumbe wenzangu. Kwa heshima na taadhima, naomba niseme kwamba matamko yaliyotoka kutoka kwa wenzetu hawa yalileta mtafaruku kwenye nchi yetu. Naanzia na Mheshimiwa Josephat Mathias Gwajima, yeye ni Mbunge mwenzetu, ni mtu tunayemsikiliza, ni mtu tunayeishi naye lakini pia alituambia yeye ni Mchungaji au ni kile cheo kingine hapa nchini na kwa mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, aliposema mataifa mengine na akaleta ushahidi pale kwetu akisema kwamba anapozungumzia chanjo anazungumzia hapa na anaikataza hapa, nikajiuliza na bado najiuliza kama waumini wake wako nchini hapa na nchi nyingine haya mambo yalivyoanza nchi nyingine kwa nini hakuzungumzia nchi hizo? Kwa nini linakuja kuzungumziwa hapa leo? Kweli yeye Kanisa lake ni kubwa lakini chanjo zimeanzia nje ndiyo zikaja hapa, kwa nini hakukataza kule kwa nini anakuja kukataza hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili la chanjo katika nchi yetu ni hiari mtu uamue uchanje au usichanje lakini anapolitamka yeye na analitamka kwenye nyumba yake ya ibada au kwingineko anakataza, anapokataza anakwaza, anapokwaza ni kwamba anamnyima mtu uhuru wake. Unaposema imani ni kitu very sensitive, imani yako ndiyo inakupa wewe ujisikie unajiamini na unakuwa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kujadili jambo hili kwenye Kamati mengi yamezungumzwa na Mwenyekiti wangu na mimi ni sehemu ya yale yaliyozungumzwa. Jambo gani limenifanya nisimame na kuomba kuchangia ni kwamba mtu mmoja au watu wachache wasiingilie uhuru wa mtu. Wahenga walisema hiari yashinda utumwa ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipotuambia tuchanje alisema hiyo ni hiari yenu hatukulazimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa inatia uchungu, inakera na unajua kwamba mimi nimesimama hapa kama kiongozi wa wanawake nikijua jinsi gani wanawake wanaimani na wanapenda kusikiliza viongozi wao, tutakavyobweteka tukasema ameongea kiongozi yule tusijilinde, tusilinde wengine tunakwenda kuhatarisha familia zetu. Naunga mkono adhabu zilizotolewa kuhusu shahidi huyu kwa sababu yeye alitukwaza alipokuwa akisema kwamba anazungumza kwa kuoteshwa au kwa kufuata Roho Mtakatifu. Mimi ni Mkristo Roho Mtakatifu ndiyo tunavyobatizwa, tunabatizwa kwa maji na Roho Mtakatibu. Huyu Roho Mtakatifu asiyetaka utakatifu anataka vitu basi huyu siyo Roho Mtakatifu bali Roho Mtakavitu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni suala la Shahidi Mheshimiwa Jerry Silaa, haihitaji rocket science kuzungumza na kusema kwamba mshahara unakatwa kodi. Kodi ni kitu ambacho kiko kwa mujibu wa sheria na kuna kodi nyingi sana katika nchi hii na hii kodi ya mshahara ipo. Wabunge wanalipwa mshahara kama public servants na Pay As You Earn inakatwa, sasa sioni ni kwa jinsi gani mtu mwelewa kama Mbunge anakwenda kwenye mikutano yake ya hadhara anapigiwa makofi, anapata mihemko na anazungumza zaidi ambavyo angetakiwa.

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana kwamba Mheshimiwa mwanangu huyu alisema hatukatwi kodi na aliulizwa, je, wewe ulikuwa unakatwa kodi ulipokuwa Mstahiki Meya? Akasema yeye alikuwa anapata posho na alikuwa hakatwi kodi. Sasa kama hivyo ndivyo kwa nini wakati ule hakuliona ni tatizo amekuja kuona ni tatizo leo hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu unakaa unajiuliza Bunge hili lilianzishwa miaka mingi nyuma toka enzi za mkoloni na yanayofanyika hapa yalikuwa yanafanyika, kwa nini hao wote waliopita miaka hiyo hawakuona, inakuja kuonekana leo, unajiuliza hapa kuna jambo gani? Kwa nini limeleta simanzi na taharuki? Unajiuliza hivi hii ni sawa, tunyamaze? Hatukuweza kunyamaza, naunga mkono adhabu zilizotolewa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)