Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kutukutanisha tena hapa tuzungumzie Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2021/2022-2025/2026, uliobeba dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wetu sisi wote tumeletwa na watu humu ndani, na sisi wenyewe ni watu na mahitaji watu waliotutumia waliyonayo ni sawa na tuliyonayo. Naipongeza Serikali kwamba hatukuwa tumesimama tukipiga mark time bali toka ule mpango wa miaka mitano mitano ulipoanza mambo mengi yamefanyika; barabara zimejengwa, maji yameboreshwa, elimu imekwenda mbele, lakini kiubinadamu tu jambo likishatekelezeka halina motisha tena. Alisema guru wa management, once a need is satisfied it’s no longer a motivation. Na hilo ndiyo linatufanya kila siku tuone kwamba kuna jambo la kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naanzia pale kwenye viwanda, na ninazungumzia kwenye viwanda katika mpango wamepanga kuzuia au kulinda viwanda ambavyo vinaagiza vitu kutoka nje ili vile vya kwetu vinavyotengenezwa viweze kupata soko na pia viboreshwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitakwenda moja kwa moja kwenye viwanda vya sukari. Sukari ni bidhaa ambayo inahitajika na kila mtu, na sasa hivi ninavyozungumza ni siku chache tu wenzetu Waislam watakwenda kwenye Mfungo Mtukufu wa Ramadhani, na sukari ni bidhaa ambayo inahitajika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na sukari siku zote imekuwa mfungo huu unatokea wakati ambapo viwanda viko kwenye maintenance na vitafungwa au vimeshafungwa kwa ajili pia ya mvua. Lakini sukari hiyo mpaka mwaka jana ikifika wakati huu sukari inaadimika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tumezungumza hapa; Serikali inafanyaje sasa kuhakikisha kwamba sukari haiadimiki tena. Kumbukumbu zangu zinanikumbusha kwamba Waziri wa Kilimo alisema mwaka huu shida hiyo haitakuwepo. Na namuomba Mungu shida hiyo isiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama haitakuwepo ninachotaka kusema kuhusu viwanda vya sukari ni nini; kwa kuwa shida kubwa inayotokea ni kwamba wale wanaoagiza sukari wanasema wanaagiza sukari ya viwandani, ile sukari nyeupe nyembamba ile na siyo sukari ya kula watu, wao waagiza industrial sugar. Lakini unakuta kwamba wanachanganya humohumo na kuja kufanya repacking.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba, Serikali sasa ione kwenye mpango huu inaboresha au inawasukuma hao wenye viwanda vya sukari hiyo sukari ya viwanda itengenezewe hapa hapa nchini. Tuna viwanda vingi vya sukari vikiwemo TPC, Kilombero, Mtibwa Sugar, vingine wamesema vinakuja Bagamoyo, vingi tu. Sasa naomba kabisa kwenye mpango huu tuelezwe ni viwanda vingapi vya industrial sugar vinakwenda kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu nimeona mambo yanayohusu utawala bora lakini sikuona utawala bora kwenye ngazi ya chini; tuna watendaji wa vijiji, tuna watendaji wa kata. Watendaji hao ni watu muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku, watendaji hao ndio wanaoishi na wananchi wetu, watendaji hao ningetaka iandikwe watapewa elimu. Na wanapewa elimu gani; elimu sasa ya kuweza kujenga kanzidata kuhusu mambo yanayofanyika kwenye maeneo husika yakiwemo yale ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila aliyesimama hapa amezungumzia kilimo, nitazungumzia kilimo kivingine, ya kwamba tuwe sasa na database ya kujua ni mazao gani yanayolimwa kwenye eneo fulani na ni ukubwa wa eka ngapi yanalimwa? Na ni wakulima wangapi wanalima mazao hayo, na yanavunwa kiasi gani. Wakati huo tukiwa na rekodi hiyo, Serikali inakuwa tayari ina rekodi ya kutafuta masoko. Wanatafuta masoko na tukishapata haya mazao wanakwenda sasa kuuza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna changamoto moja; kijijini wakishavuna wanakwenda likizo. Wamevuna wanafanya sherehe, kwingine wanaweka kidogo akiba, hakuna kuunganisha sasa nini kinafanyika, wanakaa hivyo mpaka msimu mwingine. Na ukizingatia kwamba sisi kilimo chetu kinategemea zaidi mvua za msimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali yangu sikivu iangalie sasa baada ya kilimo – na sasa hivi kuna vijana wengi ambao wako vijijini; wako waliomaliza form six, wako waliomaliza chuo kikuu na pia wazazi wao – watu hao wanawekwa katika zoezi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda tu nitoe mfano kidogo wa kule Libya alipokuwa, Hayati sasa, Muammar Gaddafi. Yeye alikuwa vijana wakifikia rika fulani kama anakwenda kupata mwenza basi anamzawadia dola 5,000. Sisi Tanzania hatuna hizo petrol dollars lakini Mungu ametubariki kuwa na eneo kubwa, tuna ardhi kubwa na vijana hawa wangeweza kabisa wakafunguliwa maeneo wakapewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo lazima kama umezaliwa kule ulikotoka hakuna maeneo, basi watoke kule waende kwenye maeneo mazuri. Hata kama watakuja Mbeya, kule Rungwe kuna maeneo mazuri tu, au Sumbawanga, wakagawiwa maeneo mazuri wakafungua mashamba ikajulikana ni batch gani, ni mashamba yapi wakaenda wakalima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wakishalima mashamba hayo wanafungua sasa ukurasa mpya wa kilimo cha wasomi. Ninaomba sana mpango huu uweze kufikiria namna ya kuwafungulia au kuwatawanya vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliposimama kuzungumza yalikuwa yanazungumziwa mambo ya michezo. Naomba niliendee vingine, naona huku ndani Waheshimiwa wanazungumza timu zile kubwa tu za watani wale wawili. Sasa hao wachezaji mnaowajua wakishaondoka - sitaki kuwataja majina maana yake mnaweza mkacheka, japo nina timu yangu fulani – ni lini sasa sisi tulio hapa ndani na Serikali kwa ujumla, Wizara ya Habari na Utamaduni, itashuka chini kule kwenye kata tuwe na timu za kata? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na isiwe kazi ya Mbunge tu, Serikali ipeleke wataalam, tuwe na timu za wilaya, tushindanishe watu. Hapa ni mtu mmoja tu anayefahamika ikitajwa inajulikana ndiyo kule kwake, inaitwa Namungo eeh? Eeh, Namungo tu ndiyo inayofahamika hapa, labda kwa vile kiongozi huyo alikuwa refa. Sijasikia, naskia wananitajia Singida na nini lakini sijasikia Nkasi, sijasikia Mbeya. Ila nikupongeze, umewatoa Mbeya kimasomaso kuna Tulia Marathon. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nawaomba, Waheshimiwa kila wakati wanachukua jezi kupelekea wachezaji wao, lakini hatujazisikia timu zao. Mpango huu kwa kuwa michezo ni ajira basi ishuke chini, tuandae vijana wetu toka utotoni wakue wakijua michezo na waendelee kuboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kumekuwa kuna shida na ugomvi mkubwa kuhusu TARURA, na kilio, TARURA, TARURA. Lakini kwenye mpango sikusikia Mfuko wa Barabara. TARURA inajenga barabara, ikishajenga inaacha, kuna Mfuko wa Barabara ambao ndiyo unaotunza barabara, ulikuja hapa Bungeni mkautungia sheria. Tutagombana hapa na TARURA lakini tunamgusa ambaye siye. Hebu tutafute chanzo cha ugonjwa kiko wapi. Naomba mpango huu utueleze kuhusu Mfuko wa Barabara, hela zile zimegawanywa vipi au zinakwenda kwa jinsi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Mfuko wa Maji; tumesikia ujenzi miundombinu ya maji lakini hatujui ule Mfuko wa Maji unakwenda vipi. Mtandao wa maji safi na salama unakwenda kasi, lakini mtandao wa maji taka hatuusikii ukitajwa. Itakuja siku, na sasa hivi hizi mvua zikituvuruga kidogo tu ukipita kule Jiji kama Dar vinyesi vinaelea juu kwenye zile barabara za halmshauri/jiji, wanachomekea kule ile mipira inatokea. Ninaomba mpango huu uelekeze sasa mnapotaja maji mtaje maji safi/ salama na usafi wa mazingira… kengele ya ngapi?

NAIBU SPIKA: Ya pili.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)