Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kabla sijaanza kutoa mchango wangu napenda nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mama yetu kipenzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutupia jicho kwenye Idara ya Maendeleo ya Jamii, kwa kumteua Naibu Waziri ambaye kimsingi atawajibika moja kwa moja kwenye kusimamia Idara hii ya Maendeleo ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hayo kwasababu, ni Afisa Maendeleo wa Jamii kwa hiyo nisingekuwa Mbunge leo hii Juliana Shonza ningekuwa Afisa Maendeleo ya Jamii kwa hiyo, ninajua changamoto mbalimbali ambazo zinaikumba Idara hii. Ukiangalia chanzo cha kuanzishwa Idara ya Maendeleo ya Jamii, ni zile changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kipindi kile miaka 1750 kipindi ambacho kulitokea na mapinduzi ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapinduzi hayo ya viwanda yalipelekea changamoto mbalimbali kwenye jamii ikiwepo, ukosefu wa ajira, watoto wa mitaani, lakini vile vile, migomo pamoja na maandamano ndipo walipoamua wakaona kwamba sasa kuna umuhimu wa kuja na sekta au Idara ambayo moja kwa moja ita-deal na masuala ya jamii kwa maana ile mifumo mizima ya jamii ambayo inaletwa na mabadiliko mbalimbali kwenye jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema haya yote kwasababu, leo hii kwenye halmashauri zetu tunao maafisa maendeleo ya jamii lakini katika namna ya kushangaza na kusikitisha sana, maafisa maendeleo hawa hawafanyi majukumu yao ya kimsingi, ile dhana halisi ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa Idara hii ya Maendeleo ya Jamii imeachwa na hatimaye sasa hivi, maafisa hawa wamegeuka kuwa maafisa mikopo. Kitu ambacho sio jukumu lao la kimsingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu kwamba kwenye jamii yetu sasa hivi changamoto ziko nyingi. Kuna masuala ya ubakaji kwa watoto, ulawiti na hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kesi nyingi sana ambazo zipo huko kwenye jamii zetu, nyingi zinaishia kule kule kwenye jamii, hazisikiki na haki inakuwa haitendeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Rose Tweve kuna siku alisimama hapa akazungumza kwa hisia sana kwamba kuna mtoto ambaye amebakwa na mzazi wake na mwisho wa siku akaambukizwa na UKIMWI, lakini kesi hiyo haijaenda popote, mzazi huyo yuko mtaani, anaendelea kudunda wakati mtoto huyu tayari future yake imeshaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu changamoto kama hizi ziko nyingi. Unaweza kujiuliza kwamba kesi kama hizi ziko ngapi kwenye jamii yetu? Hata hivyo, sisi kama Serikali ni nani ambaye tumemweka kule chini ambaye moja kwa moja anawajibika kwenye kushughulikia hizi kero na changamoto na mifumo hii ya kijamii ambayo inaleta athari kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia suala zima la mmomonyoko wa maadili, suala zima la miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Serikali imekuwa inapeleka fedha nyingi sana kule chini kwenye jamii yetu; lakini mwisho wa siku miradi ile imekuwa haiendelei, inakufa. Ukiangaliza chanzo ni nini? Ni kwa sababu jamii ile haijashirikishwa ipasavyo kuweza kuji-engage kwenye ule mradi ili waweze kuona kwamba nao ni sehemu ya ule mradi na kwamba Serikali imewaletea ule mradi siyo kwamba ni mradi wa Serikali peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo ni la msingi sana, nami nikaona kwa sababu sasa hivi tumepata Naibu Waziri wa kusimamia suala hili, ni vyema niweze kutoa maombi yangu kwamba jambo la msingi la kufanya kwa sasa hivi, cha kwanza kama akiona inafaa, Serikali iweze kuangalia ili tupitie upya ule mfumo wa upatikanaji wa Maafisa Maendeleo ya Jamii na majukumu yao. Warudi wakafanye kazi yao ya msingi kule kwenye jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, Serikali imekuja na Mpango mzuri sana na imetuahidi kwamba ikiwezekana ndani ya Bunge hili wataleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wote. Muswada huo ni mzuri kwa sababu upo kwenye Ilani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ila swali la msingi la kujiuliza ni je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba mradi huo unaweza kutekelezwa ipasavyo na ukaleta tija kama ambavyo Serikali imekusudia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu suala la Bima la Afya kwa wote siyo suala la Serikali peke yake, maana yake ni Serikali pamoja na wananchi wote kwa pamoja tuna jukumu la kuchangia na kushiriki kikamilifu kuhakikisha kwamba mradi huu, mkakati wa Serikali na sera hiyo inaweza kutekelezwa ipasavyo na kuweza kuleta matunda ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi ni kwamba tumejiandaa vipi? Kwa sababu hili ni suala la elimu. Tutoke kwenye ule mfumo wa kuanzisha miradi au mikakati au sera halafu tunawapa taarifa wananchi. Tuingie kwenye mfumo wa kuwaelimisha wananchi wafahamu umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu, tunaishi kwenye jamii ambayo ina misingi mbalimbali. Tunatofautiana masuala ya mila na desturi; na mapokeo juu ya mambo mbalimbali ya kijamii. Kwa mantiki hiyo, ni lazima tupate watu ambao wataenda kule chini kuelimisha jamii waone umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko dini ambazo mpaka sasa hivi wao hawaamini kabisa kuhusiana na suala la tiba za kisasa. Zipo jamii zetu ambazo zinaamini katika ugonjwa wowote, ni mtu amelogwa. Hizi ni changamoto zilizopo kwenye jamii yetu. Pia ziko jamii ambazo zinaamini sana kwenye mitishamba kuliko kwenda hospitali. Kwa hiyo, ukiangalia mabadiliko haya na suala zima la mfumo kwenye jamii; ili Serikali iweze kutekeleza azma yake hiyo ambayo ni njema sana kwa Watanzania, ni lazima tuwatumie Maafisa Maendeleo ya Jamii waende kule chini wakaelimishe jamii waweze kuona umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijikite kwenye kutoa ushauri wangu kwa Serikali. Kwanza napenda kuishauri Serikali ipitie upya mfumo mzima wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, warudi wakafanye kazi zao za kimsingi. Tunafahamu kwamba kule chini wako Maafisa Ushirika ambao kimsingi ndio ambao wanasajili VIKOBA pamoja na SACCOS. Naamini hawa wanaweza wakatumiwa vizuri na wakaleta maendeleo, wakafanya kazi ya kusajili vile vikundi vya vijana, akina mama pamoja na watu wenye ulemavu ili hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wabaki kwenye jukumu lao la msingi la kushughulika na matatizo ambayo yapo kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili kwa Serikali, kwa sababu tunatambua kwamba imekuwepo changamoto pia ya muda mrefu kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii tulionao sasa hivi hawatoshi; nikisemea tu kwenye Mkoa wangu wa Songwe tunazo wilaya nne, lakini tuna Maafisa Maendeleo ya Jamii wawili tu. Sasa huko chini kwenye vijiji na Kata bado hatuna Maafisa Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe tu ushauri kwa Serikali kwamba katika kipindi hiki ni vyema wakaangalia namna gani ya kuweza kuajiri Maafisa Maendeleo ya Jamii kama ambavyo Serikali imefanya na imefanikiwa kuajiri Watendaji wa Vijiji. Kwenye kila Kijiji Tanzania kumekuwa kuna Watendaji wa Vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini hata kwa hili la Maafisa Maendeleo ya Jamii haliwezi kushindikana kwa sababu ni Idara ambayo ni nyeti sana; na kama tukiipa kipaumbele kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha kuipa kipaumbele Idara hii, naamini hizi changamoto za kijamii za kimfumo zitapungua ikiwezekana, kumalizika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine, nataka kuishauri Serikali kwamba wanasema jambo lolote ili liweze kufanikiwa, ni lazima liandaliwe. Kwa hiyo, vile vile kwa sababu tunakwenda kwenye Bima ya Afya kwa wote, waangalie sasa namna gani ambavyo watawaita hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii baada ya kwamba wameshaajiriwa na kupatikana kwa kutosha ambao ndio tunategemea kwamba waende kule chini wakaelimishe jamii, ni vyema Serikali sasa ikaangalia na wao pia waweze kuelimishwa, waandaliwe ili vile vile waweze kutafsiri ile Sera ya Serikali kulingana na tofauti za kijamii ambazo tunazo, kulingana na mila na desturi na tamaduni zote ambazo zipo kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala la vitendea kazi. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii. Wengi wako maofisini, hawafanyi kazi yoyote ya kwenda kule chini kwenye jamii kwa sababu tu inawezekana hawana vitendea kazi, lakini kwa sababu walikuwa bado hawajajua kwamba wao wanasimamia kwenye majukumu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri pia Serikali yangu ya Awamu ya Sita kwamba ni vyema, kama ambavyo imefanya vizuri kwenye Maafisa Kilimo, sasa hivi kila Afisa Kilimo amepewa usafiri, vile vile wale Waratibu Kata wa Elimu wamepewa usafiri. Naamini hata kwa hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wakipewa vitendea kazi, wanaweza wakafanya kazi nzuri zaidi na hata miradi ya Serikali itapiga hatua mbele kwa sababu hawa ndiyo wa kwenda kuelimisha jamii na kuhakikisha kwamba Serikali inaweza kufikia yale malengo ya milenia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru kwa nafasi. (Makofi)