Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nikushukuru sana kwa kunipa muda ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwaambia ndugu zangu Waislamu wa Jimbo la Kawe na Waislam wote wa Tanzania nzima kwamba Ramadhan Kareem na Ramadhan Mubarak. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa makusudi ya kuokoa muda, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia nampa pole kwa kuondokewa na aliyekuwa Rais wake ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba uniruhusu kwa sababu huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhan, nianze hotuba yangu kwa kunukuu andiko moja kwenye Maandiko Matakatifu. Kitabu cha Hosea 4:6 inasema hivi: “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. The English version says: “My people are destroyed for lack of knowledge”. Pia andiko hilo hilo limeandikwa kwenye Kitabu cha Methali 29:18. Kitabu hiki kiliandikwa na Suleiman Bin Daudi, Mfalme aliyewahi kuishi miaka mingi iliyopita, alisema hivi: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maono”. Kiingereza chake, anasema: “My people are destroyed for lack of vision”. Kwa hiyo, tunapata ujumla kukosa maono kunaangamiza na kukosa maarifa kunaangamiza; lack of vision destroys and lack of knowledge as well as destroys.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini sasa nimesema hayo? Kwa sababu nimekuwa nikijiuliza sana, kwa nini nchi zetu za Kiafrika na Taifa letu likiwemo, haziendi kwa speed ya maendeleo kama inavyotakikana. Ukiangalia resources ambazo zimo ndani ya Bara la Afrika na nchi yetu, hazihusiani na speed ya maendeleo ambayo Waafrika na Watanzania tuko nayo. Kwa nini? Nimekuwa nikiangalia, kwa mfano, asilimia 91 ya reserve ya almasi duniani inatokea Bara la Afrika; na asilimia 64 ya dhahabu duniani inatokea Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, haitoshi, kwenye nchi yetu tuna dhahabu, tuna almasi, ambavyo ni precious stone, pia tuna Semi-precious Stone, tuna Ruby, Emerald, Green Garnet, Aquamarine, Honey Color Opal, Black Opal, Rhodolite, Moon Stone, tuna madini ambayo unaweza kuyataja mpaka ukaimaliza dunia yote yako ndani ya nchi yetu ya Tanzania, lakini hatuendi kwa speed inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimegundua jambo moja. Jambo la kwanza, natural resources haiwezi kufanya kazi yenyewe bila human resource. Unapokuwa na madini, lazima uwe na akili ya kuyageuza madini hayo kuwa barabara, maji au umeme. Kwa hiyo, naweza kusema basi, human resource is superior to natural resources, kwa sababu unahitaji binadamu ili ageuze hizi natural resources kwenye maisha kamili ya watu ya kila siku. Nikaona hili ni tatizo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la pili ambalo nataka kuliongelea kwa dakika zangu hizi chache, Tanzania tunashindwa kuendelea mbele kwa kasi kwa sababu hatuna mwendelezo wa regime moja kutoka regime nyingine. Ni kana kwamba Mheshimiwa Nape Mbunge wa Mtama alikuwa amedukua hotuba yangu; sijui kama ni mtalaam wa IT au hapana, kwa namna nyingine nafikiri ama aliona maono ama alifanya udukuzi fulani ambao nitaufuatilia baadaye. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilichotaka kusema ni hiki, hebu tuone; Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwl. Julius Kambarage Nyerere, alitawala kwa miaka 24. Wakati anamaliza utawala wake, aliacha viwanda 411 vinafanya kazi. Unaweza kuvitaja, Kiltex, Musomatex Mwatex Sunguratex, you can name vyote, viwanda vilikuwa vinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amekuja Mheshimiwa Rais wetu wa awamu ya pili kama alivyosema Mheshimiwa Nape ali-improve baadhi ya mambo, lakini hakuendelea na wazo la viwanda, palikuwa kimya. Akaingia Rais wa tatu, viwanda vilevile vilivyoachwa na Mwalimu badala ya kuviendeleza, akaanza kuvibinafsisha vikauzwa vyote vikaondoka. Kwa hiyo, hakuna muunganiko kati ya regime ya kwanza na regime ya tatu. Tutakesha kama hakuna muunganiko huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, haikutosha, amekuja Rais nne ambaye ni Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kiwete ambaye hatukumwona akishughulika na viwanda hata kidogo, tulimwona akishughulika na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukamwona Rais anayefuata, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, tena anasema, “Tanzania ya Viwanda.” Viwanda vilevile ambavyo Mzee Mkapa alivibinafisha na kuviuza, huyu tena anasema Tanzania ya Viwanda. Hapo ndipo tunaanza kupambana tena kuanza viwanda wakati viwanda vimebinafsisha, vimeingia mikononi mwa watu binafsi, nao awajajenga viwanda bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikagundua jambo moja ambalo napenda niliseme. Kila Rais aliyeingia madarakani ali-perform vizuri colorful kwa namna yake; Mwalimu Nyerere ali-perform vizuri sana kwa namna yake; Mwinyi ali-perform vizuri sana kwa namna yake; Mkapa ali- perform vizuri sana kwa namna yake; Mheshimiwa Jakaya Kikwete ali-perform vizuri sana kwa namna yake; Mheshimiwa Magufuli aka-perform vizuri sana kwa namna yake; naamini na Mheshimiwa Samia ata-perform vizuri sana kwa namna yake pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, namna zao hizi, kama kila mtu ana namna yake, unategemea nchi itaendeleaje? Kwa sababu kila mtu ana namna yake; na namna ya mmoja ni kinyume cha namna ya aliyetoka. Tutaendaje kama namna hizi hazifanani? Hii inanipelekea kusema, ili tuendelee, tunahitaji agenda ya pamoja ya Taifa lote. Kwa namna gani tu-define maono ya Tanzania ya miaka 30 ijayo. Inaweza ikawa miaka 30 au miaka 50, tuwe na vitu ambavyo sisi Watanzania tutaviita maendeleo. Siyo lazima vitu hivyo viitwe maendeleo Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ujenzi wa maghorof siyo maendeleo kwetu. Tunaweza kusema maendeleo kwetu ni kila Mtanzania awe na maji safi na salama. Tunaweza kusema maendeleo kwetu; kila Mtanzania mwenye uwezo wa kusoma shule, asome Chuo Kikuu na amalize, asiwepo asiyesoma Chuo Kikuu. Tunaweza kusema maendeleo kwetu sisi, wafanyabiashara wafanye biashara vizuri, tuwe na export. Tunaweza kutafsiri maendeleo tunayoyaita maendeleo katika nchi ya Tanzania na tukaacha kutafsiri maendeleo kutumia jukwaa la Wamarekani au watu wa Ulaya, tukaamua kuwa na miaka 50 ya kile ambacho sisi tunaamua kuki-achieve kama maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila Rais anayeingia madarakani, aingie kutimiza kwa namna yake na kwa sarakasi yake vile vitu ambavyo sisi tumevitafsiri kama maendeleo kututimizia kwa namna yake. Kama hatutafanya hivi, tuna hatari. Kwa sababu Katiba yetu inampa nafasi kila Rais anayeingia madarakani kwa namna yake, kwa hekima yake na kwa namna anavyotafasiri yeye maendeleo awaletee maendeleo Watanzania. Siku moja tutakapopata Rais ambaye hayuko sawasawa, tutaishia kulia. (Makofi)

Mheshimiswa Naibu Spika, ni ombi langu sasa kwa dakika chache hizi, naomba ikiwa ni nia yetu tuendelee, tuwe na vision ya miaka 50 ya Taifa na hii vision tuitafsiri, tuseme vision yetu ni kila mmoja apate maji, kila nyumba iwe na umeme, asipatikane Mtanzania anayekaa kwenye nyumba ya majani; tu-define vision yetu. Halafu tunasema, inapoingia regime, anapoingia Rais, lazima ilani ya chama chake izungumze mambo ambayo sisi tumejiwekea kama maono ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano. Patakapotokea Rais akaanza kufanya mambo yake ambayo hayako ndani ya ilani, kuna mtu wa kumwuliza hapa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Amirijeshi Mkuu kwamba hutakiwi kufanya hayo? Hayupo! Tutakapokuwa na vision ambayo imewekwa kwamba tunahitaji ku-achieve mambo kadha wa kadha na kila regime inapoingia, iwe ya kijani, ya blue au ya namna yoyote, itatimiza yale ambayo tumejiwekea kama maendeleo kwetu na maono ya Taifa letu. Tafuta sarakasi zako ama kwa ukali, ama kwa nguvu, ama kwa namna yoyote, ilimradi yale maono tuliyojiwekea kama Taifa yatokee kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ahsante sana. Nasema tena, katika jina la Mwenyezi Mungu Subhan- huwa-taallah na katika jina la Yesu Kristo na katika jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi iendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)