Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote ambaye ametufikisha hapa leo tukiwa na afya njema na uhai ambao ametupa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo napenda nijikite katika mambo mawili, matatu. Mojawapo nataka nizungumze juu ya watu wenye ulemavu na ajira. Katika kusoma na kufuatilia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu nimegundua kwamba ni msikivu sana, amefanya kazi nzuri sana, amefanya kazi ambayo Mungu anamtaka yeye afanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu ilishauri mambo kadhaa wa kadha lakini nashukuru moja ambalo umesema unaenda kulitekeleza ni hili la kuleta data kamili ya watu wenye ulemavu. Data kamili ya watu wenye ulemavu itatusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hiyo data kamili ya watu wenye ulemavu, kutakuwa na wasomi, wafanyakazi, watoto wadogo na wagonjwa ambao tutawatambua ili kutekeleza kwa urahisi kabisa malengo ambayo tumejiwekea kwa watu wenye ulemavu. Naomba niseme kwamba hali ya watu wenye ulemavu ni ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke msisitizo katika suala la ajira. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameendeleza yote mazuri yaliyofanywa na Awamu ya Tano. Katika kuchagua na kujali Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, amechagua watu watano katika Baraza la Makatibu Wakuu, hii pekee inaonesha dhahiri anatuamini sisi watu wenye ulemavu. Naomba Serikali iangalie suala hili kuanzia hapo, kwamba tumejaliwa watu watano wenye ulemavu basi ishuke mpaka chini kwenye watumishi ili tuweze kuonekana na kuonesha uwezo wetu ambapo tunaamini kabisa uwezo tunao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuangalie lile suala la asilimia tatu, je, limetimizwa na kwa ukubwa gani? Kwa sababu nikiangalia private sector, hata humu ndani tu kuna Wabunge wana makampuni makubwa, je, wametimiza ule wajibu wa asilimia tatu? Hili suala tulifuatilie, tusiwe tunaweka sheria ambazo hatuwezi kuzifuatilia kama zinatekelezeka. Tuweke sheria ambazo tunaweza tukazifuatilia tukajua kabisa hii idadi ya watu wenye ulemavu ya asilimia tatu inatekelezwa Serikalini pamoja na private sectors. Kwa private sector, mtu amewekeza pale akiamini mtu mwenye ulemavu hawezi, basi tuangalie namna gani ya kuwapa hawa watu motivation au kuangalia namna yoyote ile hata ya kuwapunguzia kodi fulani hivi ambayo inaweza wao kuwafanya waendelee kuajiri watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu nafahamu watu wanaoniomba kazi na wanataka ada ya shule na kadhalika. Kwa hiyo, hizi data zitatusaidia sana, nawaomba ushirikiano katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba nishukuru baadhi ya Wabunge ambao tayari wameendelea kuzungumzia watu wenye ulemavu na wale ambao wameendelea kujitoa katika majimbo yao kama kutoa miguu kwa watu wenye ulemavu wa viungo, kwa mfano, namshukuru sana Mheshimiwa Antony Mavunde. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie watu wenye ulemavu kwa jicho pana zaidi. Kwanza, tupo wachache sana na sidhani kama Serikali hii chini ya Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan itashindwa kulisimamia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nizungumze juu ya Jiji la Dodoma au Makao Makuu ya Dodoma. Sote humu ndani tunafahamu kwamba Bunge la Kumi na Moja liliazimia kuweka Sheria ya Makao Makuu, basi hii sheria isiwe tu kwenye makaratasi iendane na utekelezaji wake. Utekelezaji wake ni kuendelea kufufua vitu ambavyo vitaonyesha kweli hii ni Makao Makuu. Tuangalie Uwanja wa Msalato, ring road, upatikanaji wa maji. Hili la upatikanaji wa maji ni shida sana, kuna maeneo ambapo siku nne hakuna maji, tunaishije hapa na sasa hivi tuna kiwango kikubwa sana cha watu. Kwa hiyo, naomba sana Serikali hii itambue na iendeleze lile wazo la Mwalimu Julius Nyerere la kuhamia Dodoma ambalo lilitekelezwa Awamu ya Tano, tuendelee kutekeleza yale yote ambayo waasisi wetu wametuwekea katika mipango yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwashukuru Watanzania wote ambao wamejitokeza kwa wingi kuomboleza msiba wa kipenzi chetu. Hii imetuonesha kabisa kwamba Rais wetu alikuwa anakubalika, amefanya kazi kubwa kwa ajili wa Watanzania na kweli alikuwa ni Rais wa wanyonge. Kwa kuangalia hilo, naamini Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu mpendwa ataendeleza yote kwa sababu ni mwanamke shupavu na jasiri. Naomba wanawake wote tumsaidie kusimamia yale yote ambayo tumejiwekea katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache niliyozungumza, naunga mkono hoja hii ya Waziri Mkuu. Ahsante sana. (Makofi)