Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya na majukumu mengi ambayo wanayabeba kwa umahiri na weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika kabisa kwamba timu hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ikiendana sasa na kauli mbiu mpya ya kazi iendelee chini ya mama yetu mama Samia Suluhu Hassan ambaye tunamuombea sana Mungu amjaalie hekima na maisha marefu, nina hakika tutakwenda vizuri watatufikisha salama tunapotakiwa kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitachangia maeneo matatu. Eneo la kwanza ni juu ya suala zima la hifadhi ya jamii. Niipongeze Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii kwa muda mrefu imetufanyia kazi nzuri hasa maeneo ambayo wamekuwa mabingwa zaidi wa kuwekeza la real estate. Eneo hili ni eneo ambalo ni stable kwenye uchumi, huwa haliyumbi sana, hata likiyumba huwa linarudi sawasawa, kwa hiyo nawapongeza wamefanya kazi nzuri, wamesaidia sana suala la kuongeza makazi bora. Tunafahamu kwamba nadhani mwaka 2018 urbanization rate ilikuwa asilimia 32.6 bila kuwa na juhudi za kupata makazi bora tunaweza kuishia kukaa kwenye slums. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na-declare interest kwamba niko kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, kwa hiyo tulipata fursa ya kutembelea miradi ya ujenzi ya NSSF ya Dungu, Toangoma na Mtoni Kijichi. Miradi ile ni mizuri na ilibeba maono makubwa. Hata hivyo, tukiangalia hatua ambazo ile miradi mbalimbali imefikia, mbele bado ni parefu na nadhani iko haja ya Serikali kufanya intervention kusaidia ile miradi. Ushauri wangu ni kwamba kwa vile ziko fedha nyingi za kukopesha watu katika mambo ya mortgages hasa kupitia TMRC na benki zinazo hiyo fursa ya kukopesha lakini zinashindwa kwa kukosa wateja kwa sababu ya masharti kuwa makali. Ningeshauri katika hatua hii Serikali iandae stimulus package kwa ajili ya mabenki ambayo yako tayari kuwakopesha watu kununua zile nyumba. Tusipoweza kukopesha watu wakanunua zile nyumba nadhani ile miradi haitakwenda vizuri, haitatimiza makusudi yale ambayo yalikuwa yamelengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la stimulus package ni la kawaida kabisa kwenye uchumi mahali popote pale kunapokuwa na kamgogoro/kamyumbo fulani. Kwa hali hii iliyotokea tunahitaji kuziwezesha benki zetu zikopeshe watu kwa chini ya asilimia 10 ya riba ili waweze kunua zile nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ningependa kuchangia ni juu ya suala la Mahakama. Tumezunguka kama Kamati tumeona maboresho kwenye Idara ya Mahakama kwakweli upande wa majengo na TEHAMA wanafanya vizuri sana, lakini liko eneo moja ambalo labda hapo kabla sijaenda nishukuru kwamba hata katika Jimbo langu la Mwanga pia tumepata jengo la Mahakama zuri, mkandarasi anasubiriwa tu kuingia site, lakini tayari mkataba umeshasainiwa. Hata hivyo kiko kipande kimoja ambacho naona kimeachwa pembeni kwa sababu tu ya sheria na pengine kitakuja kutusumbua mbele ya safari.

Mheshimiwa Naibu Spika, iliamuliwa hapo awali kwamba, Mabaraza ya Ardhi yatolewe nje ya Mfumo wa mahakama. Kwa kweli, uamuzi huu pamoja na kwamba, umefanyika lakini haujawa na tija sana. Kwanza mabaraza haya yako machache, kuna wilaya nyingi ambazo hazina mabaraza ya ardhi ikiwa ni pamoja na wilaya yangu ya Mwanga. Ushauri wangu ni kwamba, Mabaraza ya Ardhi haya yarudishwe chini ya mahakama, ili yasiachwe nje ya haya maboresho ambayo yanafanyika yakaja kuachwa nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati hayo yanaendelea ni jambo ambalo linawezekana kabisa tu kwa kutumia circular la Mheshimiwa Jaji Mkuu, mahakimu wale wa mahakama za wilaya wakapewa mamlaka ya kuendelea kusikiliza masuala ya ardhi. Kama mahakama kuu imewezekana hilo hata hizi mahakama za chini inawezekana, migogoro ya ardhi ni moja ya sehemu kubwa sana inayozisumbua jamii zetu na hasa kwangu. Sisi ni wapare tunapenda na tunaweza kesi, tunahitaji baraza la ardhi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho limeshazungumziwa na baadhi ya watu hapa, ni eneo la maafa. Yako maeneo ambayo kila mwaka yanakumbwa na maafa. Mojawapo ya maeneo hayo ni kata ambayo ipo kwenye Jimbo langu la Mwanga, Kata ya Kileo. Yako mafuriko ambayo huwa yanaanzia Mto Hona, kila mwaka wananchi wale wanapata mafuriko wanakuwa ni watu wa kusaidiwa nguo na chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu tulifanya jitihada za kwenda kutembea mguu kwa mguu na viongozi wale madiwani wa kata ile ya Kileo pamoja na viongozi wa kata ya Jirani kwa Mheshimiwa Dkt. Kimei, Kata ya Kahe Mashariki. Tukatembea mguu kwa mguu pamoja na wataalamu kutoka Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Pangani ambayo nayo ni Mamlaka inayofanya vizuri sana, tunaipongeza. Tulibaini kwamba, eneo linalohitaji kudabuliwa pale ili tuondokane na shida hii ni kilometa 1.72 ili mto ule uweze kupitisha maji mafuriko yale yakome.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunavyozungumza hatujaweza bado kupata grader la kufanya hiyo kazi. Wako wafadhili binafsi ambao wametusaidia tukadabua sehemu kubwa ndio ambayo mpaka sasa hivi inafanya mvua zilizonyesha tusipate mafuriko. Lakini nilikuwa naongea na Mheshimiwa diwani wa pale anasema Mheshimiwa Mbunge tuko kwenye dilemma, tuombe Mungu alete mvua au aache kwasababu, ikija tutapata mafuriko ikikosa tutakosa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe mwito kwamba, maeneo kama haya yatazamwe ili maafa haya yasiwe ni suala la kila mwaka kwamba, ikifika mvua zikikaribia watu wanajijua kabisa kwamba, wanakaribia kulala nje na kupoteza vyakula. Kwa hiyo, huo ndio wito wangu kwa eneo hili ambalo liko ndani, maafa haya ambayo yanatokea kwenye Jimbo la Mwanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia zote. (Makofi)