Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maneno machache ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kuungana na Wabunge wenzangu kutoa pongezi kwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Katavi wamenituma pia nitoe pole kwa Mheshimiwa Rais kwa kuondokewa na jembe letu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na ahadi yetu kwake yeye Mheshimiwa Rais, tutamuunga mkono, tutafanya kazi kwa bidii ili kuyaenzi yale yote ambayo yameachwa na Rais wetu Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi kwa hotuba nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, hotuba ambayo imegusa vipengele vyote vya dira iliyotolewa mwaka 2015 pamoja na dira iliyotolewa na hotuba ya Rais mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya uchache wa muda, nitoe shukrani kwa yale yote ambayo yamefanywa katika Jimbo langu, hasa katika miaka mitano hiyo iliyopita kwa kuanza na Wizara ya Ujenzi ambayo imeanza na inaendelea kujenga barabara ya kutoka Tabora kwenda Mpanda, barabara ambayo ni uti wa mgongo wa Mkoa wetu wa Katavi na hasa nipongeze kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Ugala ambalo lilikuwa linafanya Jimbo langu lisifikiwe na magari kwa muda miezi mitatu kila mwaka, lakini kuanzia mwaka huu pamoja na mvua hii, hatujapata hiyo shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba tu kwamba kuna barabara nyingine muhimu sana ambayo sasa hivi imeanza kutumika. Kuna mabasi yanatoka Mbeya yanapita Katavi yanakwenda Mwanza; na siku hiyo hiyo yatoka Mwanza pia yanaelekea kwenda Mbeya na barabara siyo nyingine, ni Inyonga - Maji ya moto kupita Mloo kwenda Kamsamba na inafika mpaka Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni potential kwa aina yake kwa sababu Ziwa Rukwa ndiyo Ziwa ambalo lina gesi ambayo ni ya muhimu sana inaitwa Helium. Ni nchi chache sana duniani ambazo zina gesi ya namna hiyo. Sasa ni muhimu sana kukumbuka kuanza kutengeneza miundombinu kwa sasa kabla hatujaanza kuchimba hiyo gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru sana Wizara ya Nishati, juzi wamesaini mikataba yote kwa ajili ya REA III. Wamekamilisha sasa vijiji vilivyokuwa vimebaki katika Jimbo langu; Kijiji cha Ilunde, Kijiji cha Isegenezya, Kijiji cha Mapili ambacho mimi mwenyewe nimezaliwa, Kijiji cha Masigo na Kamalampaka, vyote vimeingizwa. Kwa hiyo, baada ya mradi huu kukamilika, jimbo langu litakuwa na umeme kwa asilimia 100. Nawashukuru sana Wizara ya Nishati; Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru Wizara ya Kilimo. Jimbo langu kwa asilimia 100 ni wakulima. Tunalima mazao ya chakula pamoja na mazao ya biashara na zao kuu la biashara ni Tumbaku. Kule tuna vyama vitatu vinavyoshughulikia tumbaku. Tuna Chama cha Ukonongo, tuna Chama cha Ilela na tuna Chama cha Utense. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama cha Ukonongo ndiyo ambacho kimekaa muda mrefu sana, lakini kilikuwa kimetengeneza deni kwa wakulima na hivi ninavyozungumza wakulima bado wanadai shilingi milioni 400. Namshukuru sana Naibu Waziri wa Kilimo, amefanya kazi kubwa na juzi Morogoro ametoa maelekezo. Kwa sababu audit imeshafanyika, kwa hiyo, nashukuru kwamba wakulima sasa watalipwa ile shilingi milioni 400. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imefikia uchumi wa kati, lakini imefikia uchumi wa kati kwa sababu ya ushirikiano tulionao sisi Watanzania lakini hasa nin kwa sababu ya hii mihimili mitatu ambayo ilifanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza kwa mhimili wa Bunge, umewajibika kwa kuchambua bajeti na kuzipitisha. Pia wakati wa utekelezaji, tukiwa kwenye Majimbo kule tulikuwa tunaangalia yale yaliyokuwa yamepangwa na Serikali kama hayatekelezwi tunakuja kutoa taarifa katika Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza mhimili wa Serikali ukiongozwa na Waziri Mkuu, ndio wametekeleza yote yaliyofanyika. Vile vile mhimili wa Sheria wa Mahakama ambao umeleta utulivu kwa wananchi kwa kuondoa uonevu, ndiyo maana kila mtu amewajibika mpaka tumefikia sasa kwenye uchumi wa kati.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imegonga.

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)