Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Rose Vicent Busiga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuzungumza kwenye Bunge hili Tukufu. Naomba kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameendelea kutulinda, lakini pia kulitetea Taifa la Tanzania kutokana na msiba mkubwa wa baba yetu, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Baada ya kupata msiba huo nilikuwa na huzuni kubwa sana na nililia kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu baba yetu alitupenda kutoka moyoni. Baba yule alikuwa na upendo usiokuwa na kifani, alikuwa na upendo ambao hauwezi kulinganishwa na mtu yoyote hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumejifunza mambo mengi kutoka kwa baba yetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Moja ambalo nililojifunza kubwa sana, nimejifunza kwa namna alivyoweza kusimama na kutusaidia sisi wanawake kupata nafasi katika Serikali hii ya Tanzania. Nitaendelea kumuenzi baba yetu kwa upendo mkubwa na ndio maana akaamua kumteua mama yetu Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wake kwa mara kwanza Tanzania ikapata Makamu wa Rais mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, safari yake ya miaka mitano ilikuwa ni safari yenye mafanikio sana na hatimaye tukauona uwezo wa mama yetu Samia Suluhu Hassan na mara tu baada ya matatizo kutokea mimi kama Mbunge wa Mkoa wa Geita, nilivyopata tatizo hilo nililia kwa huzuni sana, lakini nikajitia moyo nikasema, Wana wa Israel walipokuwa wakienda wakisafiri kwenye Nchi ya Kanaani, walikuwa na Mussa lakini hawakuweza kuifikia ile Nchi ya Kanaani, hatimaye Joshua ndiye aliyeweza kuwafikisha katika Nchi ya Kanaani. Hivyo nikaamini kabisa kwa matumaini yangu makubwa kuwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan atatufikisha kwenye Nchi ya Kanaani, nchi ya asali na maziwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze hili kwa uchungu mkubwa sana. Nasikitika na maumivu makali sana ambapo ninapoona wanambeza baba yetu aliyetusaidia mpaka leo sisi wanawake tunachangia hotuba nikiwa nina imani kabisa ya kuwa ninaweza kutoa mchango wangu na wananchi wangu wakanisikiliza.

Mheshimiwa Spika, naomba niingie kwenye hoja moja kwa moja katika Wizara ya Afya. Tumeona Serikali imeweza kufanya vizuri kwa kujenga Hospitali za Wilaya 99 lakini pia, tumeona imejenga Hospitali za Rufaa 10 na za Kanda tatu sambamba na hivyo imejenga zahanati 1,198 na Vituo vya Afya 487. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kufanya vizuri lakini pia, ninaiomba Serikali yangu kwasababu ni sikivu kuna maboma ambayo yapo ambayo wananchi wamechangia fedha zao za mfukoni wakajenga maboma yale na wanaisubiri Serikali iweze kumalizia. Nikitoa mfano, katika Wilaya ya Mbogwe kuna Kituo cha Afya kinaitwa Nghomolwa wananchi wamekijenga kwa muda mrefu sana kituo kile cha afya kimeshafikia hatua ya ukamilishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunao watendaji wetu wa kata, ndio wanaosimamia miradi hii ya ujenzi wa zahanati, ya ujenzi wa vituo vya afya, lakini watendaji hawa wa kata wanafanya kazi katika mazingira magumu ya kazi. Lakini, watendaji hawa hawa wa kata hata sisi Wabunge tukienda kwenye shughuli zetu za Kibunge, hawa hawa tunafika kwenye ofisi zao, ofisi zao hazifai, ofisi zao haziendani na yale ambayo wanatutendea sisi kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali sasa, waone haja ya kuwasaidia watendaji wa kata waweze kupata usafiri wa kufanyia kazi zao ili kuleta maendeleo kwenye kata zao. Lakini pia, niiombe Serikali yangu kwa sababu ni sikivu iweze kuwasaidia watendaji hawa wa kata hata motisha tu inatosha… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Rose Busiga, caucus imeamua iwe dakika tano tano kwa hiyo, sio uamuzi wangu nakushukuru. Imeamua hivyo kwasababu dakika ni chache ili… (Makofi/Kicheko)

MHE. ROSE VICENT BUSIGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja lakini naomba watendaji wa kata wafikiriwe kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi kwa wakati mgumu. (Makofi)