Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia kufika hatua hii kama Bunge letu Tukufu. Lakini pia, kwa kutupitisha Taifa letu katika mtihani mzito tuliopita, lakini tumepita salama kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia kwenye Bunge hili, niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Kondoa kwa kuniamini tena kwa mara nyingine na kunirejesha Bungeni kwa kura za kishindo. Wale waliojaribu kuchezea jimbo lile waliona moto walioupata na naomba wasiendelee kusogelea lile jimbo niko imara na wananchi wananiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyowasilisha, wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake pamoja na Taasisi zilizo chini ya ofisi yake. Ninapompongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu natambua usaidizi mkubwa anaoupata kwa wasaidizi wake hasa dada yetu, mimi binti yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, hongera sana mwanangu unachapa kazi vizuri, unatuheshimisha wanawake hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dakika chache naomba niseme mambo machache sana nayo ni; kwa nini Tanzania tumeingia uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda tuliojipangia? Tumeingia uchumi wa kati kwasababu ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Taifa letu, chini ya uongozi makini wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu amefanya uwekezaji kwenye miradi mikubwa na ukisoma taarifa ile ya Benki ya Dunia wameeleza wazi ni kwanini Taifa letu tumeweza kupiga hatua hii kubwa? Kwa hiyo, nitoe wito kwa Serikali yetu na nitoe pongezi sana, kwa Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mwongozo sahihi kwamba, miradi yote mikubwa inakwenda kutekelezwa mpaka ikamilike, pongezi sana kwa Serikali yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usimamizi mkubwa anaoufanya kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapopongeza hili niombe sana sana, watanzania tuwe makini na tunachokiongea katika muda huu. Tunapoanza kubeza miradi iliyowekezwa na Serikali yetu ya awamu ya tano tunamuudhi Mwenyezi Mungu. Naomba tusimame kwa pamoja na tutambue kwamba wapo wenzetu ambao walifanikiwa kuvuka kutoka kwenye level ndogo ya uchumi kwenda kwenye level kubwa ya uchumi lakini walianguka na wakarudi kwenye uchumi wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Taifa letu tunapanda kuingia kwenye uchumi wa kipato cha kati, tulishuhudia dunia kuna nchi tatu zilishuka kutoka uchumi wa juu kuja uchumi wa chini, makosa yaliyofanyika ni haya tunayoyaona watanzania tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge sisi ni viongozi, tuonyeshe mshikamano dhahiri, mshikamano wa kuyaendeleza yote mazuri ambayo yalianzishwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mengi mazuri yaliyotendwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano, ni kuleta makao makuu kwa vitendo Jijini Dodoma. Niombe sana tunapokwenda sasa kuanza utekelezaji wa bajeti yetu hii, tuone miradi mikubwa iliyokuwa inaletwa Dodoma na Serikali ya Awamu ya Tano inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan ametoa muelekeo, uwanja wa ndege wa Msalato utekelezwe kwa haraka. Tumenunua ndege nyingi… (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana, dakika tano zimeisha

MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)