Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana kwenye Kikao hiki cha Kumi na Moja cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Mbili kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe, Mheshimiwa Naibu Spika kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa mwenendo mzima wa majadiliano ya Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2021/2022. Nazipongeza na kuzishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri na michango yenye tija kwenye Hoja ya Waziri Mkuu. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa sekta ambao pia wamekuwa hapa wakisikiliza hoja hizi mbalimbali na Naibu Mawaziri lakini pia kupitia vipindi vya maswali na majibu wamekuwa wakijibu maswali na hoja kadhaa wamekuwa wakizipitia na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali. Kadhalika, nawashukuru Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu wa pamoja na ushirikiano walionipa katika kipindi chote cha mjadala wa bajeti hii yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu ambayo ni muhimu katika kuisaidia Serikali kutekeleza kikamilifu vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipokuwa nawasilisha Hoja siku ya tarehe 13 nilianza maelezo ya utangulizi mazuri ambayo sitaraji kuyarudia tena yaliyogusa maeneo mengi. Sasa tunaendelea na hoja ile ile ya kufafanua hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wote hapa wakati wa mjadala wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mjadala wa Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2021/2022 umeenda vizuri sana na umethibitisha uimara na umakini wa Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge lako Tukufu katika kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba kwa kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu. Serikali, imepokea maoni na ushauri wote uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge na wakati wote tutauzingatia katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala hapa tulikuwa na Wabunge waliochangia 121 kati yao Waheshimiwa 109 walipata nafasi ya kusema moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 12 walichangia kwa njia ya maandishi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliopata nafasi ya kuchangia kwenye hoja hii ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda naomba uridhie nisiwataje na kwamba majina yao yaingizwe moja kwa moja kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mjadala huu, Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wameendelea kujibu hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge. Kutokana na ufinyu wa muda hoja zitakazosalia zitajibiwa kwa maandishi. Vilevile, Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuwasilisha hoja zao kwenye sekta zao watatoa ufafanuzi wa yale yote yaliyogusa sekta zao. Walikuwa hapa wame-take note yale yote wanayopaswa kujibu na bajeti yao itakapokuja mbele ya Bunge lako Tukufu kila mmoja atalazimika kufafanua yale yote yanayogusa sekta yake.

Mheshimiwa Spika, wakati wa majadiliano kuhusu Hoja ya Waziri Mkuu yako masuala mengi na muhimu yameibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Aidha, wakati wote wa Hoja ya Waziri Mkuu tumekuwa na mjadala wa kina na wenye msisitizo wa kiwango cha juu kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na kujenga hoja zenye ubora na umakini unaliostahili unaoifanya Serikali kuweza kuzingatia kwa umakini kwa ajili ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, nikiri kuwa hoja nyingi zilizoibuliwa zina uhusiano wa moja kwa moja na utendaji kazi wa Serikali. Aidha, masuala muhimu hususan vibali vya kazi kwa wageni na uwekezaji kwa kiasi kikubwa yamekuwa kitovu cha mjadala na michango ya Waheshimiwa Wabunge walipokuwa wakichangia hii Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Hii ni kwa sababu eneo la Uwekezaji ndiyo ambalo sasa tunaitegemea kukuza uchumi wa nchi hasa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, maliasili, maji na sekta nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, naomba uridhie japo kwa uchache nitoe ufafanuzi kuhusu baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye Hoja ya Waziri Mkuu hususan eneo la uwekezaji na vibali vya kazi pamoja na kwamba Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi wameeleza maelezo ya awali.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 6 Aprili 2021, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali aliweka msisitizo masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji na vibali vya kazi ikiwa ni maeneo ambayo yamekuwa na changamoto nyingi katika utowaji wa vibali hasa kwenye uwekezaji. Mheshimiwa Rais aliielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha Huduma za Pamoja (One Stop Centre), kushughulikia malalamiko yote kuhusu kodi, kuondoa vikwazo katika uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji kupitia mazungumzo, ushawishi, kudhibiti rushwa na kuondoa urasimu kwenye maeneo yote ya uwekezaji ikiwemo na maombi ya vibali vya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais yenye kujali maslahi mapana ya nchi hii yalikwenda sambamba na uamuzi wake wa tarehe 31 Machi 2021 wa kuunda rasmi Wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kuwa Wizara hiyo inasimamia kikamilifu masuala ya uwekezaji hapa nchini, kikanda na kimataifa. Majukumu mengine ni kuratibu majadiliano ya uwekezaji wa miradi ya kimkakati, mikutano ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ndani na nje ya nchi lakini pia kubuni na kutekeleza mikakati ya kujenga sekta binafsi ya hapa Tanzania iliyo imara na yenye ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona ushindani huu unaanza kukuwa na utatuletea manufaa makubwa. hatua hiyo, itawezesha kuvutia wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi kuja hapa nchini lakini pia hata Watanzania wenye uwezo wa kuwekeza nao sasa wanapata fursa ya wazi ya kuanza kuwekeza mitaji yao teknolojia na ujuzi ili kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kasi na upatikanaji wa ajira na maendeleo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami, napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa uamuzi wa kurejesha jukumu la uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni ishara ya wazi kuhusu imani kubwa aliyonayo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Nami napenda kumhakikishia kuwa sitamuangusha, nitasimamia sekta hii ili iweze kuleta mafanikio hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa tayari hatua mbalimbali za utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais zimeanza kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na moja kuandaa Muundo wa Wizara ambao utaainisha majukumu na mgawanyo wa Idara na Taasisi zitakazokuwa chini ya eneo hilo la uwekezaji. Mbili, kupitia upya Sera ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kubainisha maeneo yenye kuhitaji maboresho ambapo tayari tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 imekamilika. Tatu, tunaandaa sasa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ili kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji katika sekta zote hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa hatua hizo kutaiwezesha Serikali kutekeleza masuala muhimu kama yafuatayo. Moja, ni kushiriki kikamilifu katika mikutano na majadiliano ya Jumuiya za Kikanda yanayohusu masuala ya uwekezaji ikiwemo maandalizi ya Sera ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, utungaji wa Sera za Uwekezaji kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Itifaki ya Uwekezaji ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika. Mbili, ni kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji na uchumi shindani nchini kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameendelea kusisitiza kwa kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha mazingira hayo wezeshi. Tunataka biashara ishamiri na yeyote anayekuja kuwekeza nchini apate fursa hiyo ya kuwekeza kwenye sekta yoyote ile ambayo tunayo. Tuna uhakika atapata huduma zilizo sahihi.

Mheshimiwa Spika, tatu, kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wawekezaji kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Nchi alivyokuja kueleza hapa mbele yetu. Nne, kutatua changamoto za wafanyabiashara kupitia Baraza la Taifa la Biashara ambalo sasa tunaliunda kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa ambako Mheshimiwa Rais ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo la Biashara la Taifa lenye malengo ya kuratibu majadiliano ya sekta za umma na sekta binafsi. Eneo hili tutalisimamia ili sekta binafsi nayo ipate nafasi ya kuishauri Serikali kwa ajili ya utekelezaji au uwekezaji wenye tija.

Mheshimiwa Spika, tano, kutoa elimu na hamasa kuhusu huduma zitolewazo kwenye Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre), fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta mbalimbali nazo pia ziweze kuibuliwa na kuelimisha wananchi namna ya kupata wabia na kushirikia nao katika kuanzisha na kuendeleza miradi yao kupitia Taasisi yetu ya Uwekezaji Tanzania (TIC). Sita, tunataka tuimarishe mifumo ya usajili wa miradi na kutoa Cheti cha Vivutio (Certificate of Incentives), kuunganisha mifumo inayotumika TIC na makao makuu ya Taasisi na kuboresha mfumo wa kuchakata rufaa za vibali vya kazi na ukaazi kwa njia ya mtandao ambapo kila mmoja atakuwa anaweza kuufika popote alipo ndani au nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii tena kuwakumbusha watendaji wenzangu wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuhakikisha kuwa muundo na mifumo ya masuala ya uwekezaji inakamilika ndani ya muda ulioelekezwa na Mheshimiwa Rais. Natoa maelekezo kwa Wizara na taasisi zote zinazohudumia wawekezaji kuhakikisha wanawezesha uwekezaji katika maeneo yao kwa kutoa huduma stahiki na taarifa muhimu kwa wakati zipatikane lakini pia kuondoa usumbufu ukiwa unaambatana na maombi ya rushwa lakini na urasimu kama nilivyoeleza awali, hili nalo tutalisimamia.

Mheshimiwa Spika, aidha, nasisitiza kuwa watendaji wajiepushe na haya ambayo nimeyaeleza ya uombaji wa rushwa na urasimu usiokuwa wa lazima katika kuhudumia wawekezaji ili kujenga imani baina ya sekta ya umma na sekta binafsi ili tuweze kuzungumza lugha moja. Mwaka ujao wa fedha 2021/2022, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ikiwemo kuainisha ardhi ya uwekezaji (land bank) na kuendeleza miundombinu muhimu ya uwekezaji katika mikoa yote ili kuvutia uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limeibua mjadala mkubwa wakati uchangiaji wa hoja ya bajeti ya Waziri Mkuu ni vibali vyenyewe vya kazi. Mheshimiwa Waziri wa Nchi hapa ameeleza lakini changamoto kubwa iliyozungumziwa ni kuhusu kubanwa na masharti mbalimbali dhidi ya ajira za wageni ikiwemo la kwanza ukomo wa mwombaji kuishi nchini kwa muda usiozidi miaka mitano. Huu nao umekuwa kikwazo pale anapowekeza mradi mkubwa unaohitaji kuusimamia zaidi ya miaka 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mahitaji ya elimu, uzoefu au ujuzi wake wa mwombaji ili aweze kupewa kibali. Hapa pia kuna mgogoro mkubwa. Tunadai mtu awe na degree lakini pia degree hiyo aweze kuifanyia kazi kwenye sekta hiyo. Kwa hiyo, tutaangalia zaidi uzoefu na ujuzi alionao, elimu itakuwa ni kitu ambacho kinasaidia ujuzi na uzoefu alionao katika kufanya kazi. Hili nalo tutaliangalia ili kurahisisha kupata watu ambao wanaweza kufanya kazi hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tatu kigezo cha mwombaji kupata uthibitisho wa cheti chake kutoka NECTA. Mtu kasoma Norway tunataka alete cheti ili aweze kuajiriwa hapa nchini kwa kupeleka cheti hicho NECTA, NACTE au TCU. Nalo hili tutaliangalia tena vizuri kwa sababu limekuwa likikwaza kupata wawekezaji wanapokuja kuwekeza hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo hayo ndiyo yenye mgogoro zaidi katika suala la utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni. Hivyo basi, Serikali inafanyia kazi changamoto hizo kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais. Aidha, tayari nimetoa maelekezo kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kushirikiana na Wizara zote za kisekta pamoja na watendaji wa Wizara zote za kisekta katika kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinafanyiwa kazi kwa haraka zaidi ili kuweza kuuweka uwekezaji katika sura inayotuletea watu wengi zaidi na kujenga imani ya uwekezaji hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali ya uwekezaji, kwa mujibu wa Kanuni ya 118(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo ya Mwaka 2020, naomba nitumie nafasi hii pia kuendelea kufafanua hoja nyingine ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wote wa mjadala kama ifuatavyo. Tulikuwa na hoja ya kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu ihakikishe kwamba utekelezaji wa vipaumbele ulenge zaidi katika kuwatengenezea wananchi wa kawaida fursa za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu inalo jukumu la kuratibu, kufuatilia na kutekeleza vipaumbele vya Sera na miongozo mbalimbali ya Serikali ili kumletea maendeleo mwananchi kulingana na fursa zilizopo katika maeneo husika miongoni mwa maeneo ya kimkakati ya utekelezaji wa jukumu hilo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja ni kuwajengea wananchi uwezo kwa kutambua fursa zinazowazunguka na kuzitumia kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Kwa mfano, utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali, uanagenzi, urasimishaji ujuzi, kurahisisha upatikanaji mitaji na taarifa za masoko, ni miongoni mwa mkakati wa Serikali kuwafanya Watanzania wajue fursa zinazowazunguka.

Mheshimiwa Spika, pili, kuratibu ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya kiuchumi ili kuwawezesha Watanzania kunufaika na fursa zilizopo katika maeneo yao, mathalani ujenzi wa njia za usafirishaji kama vile njia ya anga, njia za maji, barabara, pia ujenzi wa madaraja makubwa, masoko, vituo vya mabasi, miundombinu ya umwagiliaji kwenye Sekta ya Kilimo, usambazaji wa umeme na pia kuimarisha mawasiliano ndani ya nchi. Hayo yote ni yale ambayo tunayasimamia.

Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea kuratibu na kufuatilia ushiriki wa Watanzania katika utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati kupitia mpango wa local content. Lengo ni kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na utekelezaji wa miradi hiyo sambamba na uwekezaji mkubwa ulifanywa na Serikali kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano wa miradi hiyo ni ujenzi wa reli ambao sasa unaendelea ambayo ni SGR, ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambao pia unaendelea, bomba la kusafirisha mafuta litakaloanza hivi karibuni linalotoka Uganda mpaka hapa Tanzania, kuna suala la uchimbaji wa madini hususan uchimbaji mdogo mdogo nao tumeimarisha, ujenzi wa barabara za vijijini na barabara kuu pamoja na madaraja makubwa ambayo pia yanaunganisha eneo moja na eneo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja ya Wizara ya Fedha inayotaka ihakikishe inatoa fedha kwa wakati ili kuwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuteleza majukumu yake ya kusimamia changuzi ndogo zinazoendelea kujitokeza kwa mujibu wa sheria. Haya yote yanaendelea kutekelezwa na tunazingatia sana sheria, Kifungu cha 122 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura 343) na Kifungu kidogo cha (120) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura 292).

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatekeleza hili kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha kwamba chaguzi hizi zinaendelea kufanyika kama ambavyo zinaendelea. Kwa sasa tunayo maeneo mawili ya yanayoendesha uchaguzi mdogo kule Buhigwe pamoja na Kibondo ambapo pia uratibu wake umeshanza kuratibiwa.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu iwe na mfumo mzuri utakaohakikisha Makao Makuu ya Nchi Dodoma yanaendelezwa. Hili nataka nilileleze vizuri kwa kuwaondolea mashaka au wasiwasi Watanzania wakifikiri kwamba mkakati wa Makao Makuu ya Nchi Dodoma kuwa sasa hautaweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mfumo mzuri sana wa kuhakikisha kwamba Makao Makuu ya Nchi yanaendelezwa kwa kujenga na kuendendelea na mipango ya maendeleo ya Jiji la Dodoma. Mfumo huo unahusisha kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia hapa Dodoma ambacho kinajumuisha Wajumbe kutoka Wizara na Taasisi zote za Serikali.

Mheshimiwa Spika, leo hii watumishi wote wapo hapa Dodoma, shughuli zote za Serikali zinafanywa hapa Dodoma na ujenzi wa miundombinu mbalimbali unaendelea hapa Dodoma. Natumia nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji, wale wote ambao wanaotamani kufanya kazi hapa Dodoma, waje. Nataka niendelee kurudia kusema kwamba Makao Makuu ya Dodoma bado itaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki kikozi kazi kina jukumu la kushauri namna moja ya kupanga na kuendeleza Mji wetu wa Dodoma na utekelezaji huo unahusisha zaidi miradi mbalimbali ikiwemo na kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa miradi ya maji, tupate maji ya kutosha, tunajenga kiwanja cha ndege kikubwa zaidi ya hiki tulichonacho, barabara na utoaji wa huduma za jamii nao unaimarishwa na kujenga kituo cha reli kikubwa kuliko vituo vyote nchini kitajengwa hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Watanzania wote kuwa Dodoma inaendelea vizuri na wale wote wanaotamani kuja, waje, fursa zipo na njia za usafiri zote zipo za barabara na anga.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine inasema Serikali iendeleze miradi yote ya awamu zilizopita ambayo inaendelea kutekelezwa na utekelezaji wake uweze kusimamiwa. Serikali tumeahidi kutekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni ya Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, miradi yote ya kipaumbele iliyoainishwa kwenye Ilani ambayo imeanza kutekelezwa na ile ambayo bado haijatekelezwa, yote itatekelezwa ili kuhakikisha kwamba tunafikia malengo ya Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali yake kwa kutelekeza na kusimamia miradi yote hii ya kimkakati.tuna Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umeweka kipaumbele cha kuendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hilo halina matatizo.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ipo mbele yetu na imejadiliwa sana ni ile ya Ofisi ya Waziri Mkuu ishirikiane na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuboresha utaratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuwepo na mfumo mmoja wa vyanzo vya fedha. Hatua hiyo iweze kuandamana na kuongeza usimamizi wa udhibiti wa marejesho ya fedha hizo za mikopo ambazo zinatolewa na hiyo mifuko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyofafanua katika hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itathimini kwa kina utendaji na ufanisi wa mifuko yote ya uwezeshaji kwa wananchi kiuchumi ikiwemo Mfuko huu wa Maendeleo ya Vijana ili kuona kuwa kuna umuhimu wa kufuta baadhi ya mifuko kuunganisha au kuanzisha mifuko mipya kwa kuzingatia mahitaji ya sheria za nchi.

Mheshimiwa Spika, aidha, wakati wote mchakato huu ukiendelea, taratibu za kuratibu marejesho ya fedha za mikopo hiyo zitakuwa zinaendelea kuratibiwa ili fedha hizi zinazokopeshwa ziweze kurudi halafu ziwe endelevu kuwakopesha vijana wengine.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilikuwa imezungumzwa kwenye mijadala hapa, ni mfuko wa uwezeshaji wa vijana wa Halmashauri kwamba uongezewe fedha kutoka 4% mpaka asilimia 10. Kama nilivyotangulia kueleza, Serikali inafanyia tathmini mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa lengo la kutaka kujua kiwango cha mikopo chenyewe kinachotolewa ikilinganishwa na mahitaji, riba za mikopo yenyewe na ufanisi wa mifuko hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini hiyo, taarifa rasmi itatolewa na maombi haya yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na ushauri wao tutauzingatia kulingana na uwezo wa mfuko wenyewe kadiri tunavyoendesha ndani ya Serikali. Mfuko huu wa Halmashauri kwa sasa unaendelea kutoa 4% ya vijana, asilimia 4% kwa wanawake na 2% kwa wenye mahitaji maalum au walemavu.

Mheshimiwa Spika, yako maeneo muhimu yaliyojadiliwa kama hoja ikiwemo uboreshaji wa huduma za maji, elimu, lakini pia suala TARURA limezungumzwa sana, Sekta ya Mafuta nayo imejadiliwa sana, uimarishaji wa bandari umeungumzwa na suala la madini hasa kule Mererani imepata nafasi kubwa ya kuzungumzwa. Masuala haya yote yataratibiwa vizuri sana kupitia Wizara husika kama ambavyo nimeeleza na watafika mbele ya Bunge lako Tukufu ili kutoa ufafanuzi wa kila hoja ambayo pia imeweza kuchangiwa hapa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, hoja za Muungano zimejadiliwa sana, nazo pia zitapata ufafanuzi kupitia bajeti ya hotuba ya Makamu wa Rais. Hoja ya mfumo kununua mazao (TMX) imezungumzwa pia na Wizara ya Kilimo itazingatia hili, kwa sababu mkakati wetu sasa ni kukuza ushirika.

Mheshimiwa Spika, ushirika ni wana ushirika, tutaendelea kuwapa nafasi wanaushirika kusimamia ushirika ili tuufanye ushirika huu uweze kuwa endelevu. Mifumo mingine yote itabuniwa na kuanzishwa na Wizara yenyewe ya Kilimo inayosimamia ushirika ambayo pia inajua mwenendo wa uanzishaji wa ushirika mwenendo wa uanzishaji wa mifumo mingine inayotakiwa kusimamiwa hapo. TMX kwa sasa ni ya Wizara ya Fedha na tunaisihi Wizara ya Fedha ijiimarishe na mfumo huu, itutafutie masoko ya nje zaidi kwa mazao yaliyoko hapa ndani ili tuweze kuyauza na wanunuzi kutoka nje huko waweze kununua kwa mfumo huo wa TMX.

Mheshimiwa Spika, hoja ya mahusiano ya Vyama vya Siasa au Chama Kimoja na Serikali, imefafanuliwa vizuri na Waziri wa Nchi. Jambo hili litaangaliwa na linaendelea kuangaliwa, lakini mahusiano yetu bado ni mazuri kwa sababu tunashirikiana kwa pamojo, licha ya kuwa kuna kasoro mbalimbali ambazo pia nazo huwa zinapata ufumbuzi kupitia Baraza la Vyama vya Siasa ambapo pia huwa tunakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni migogoro ya ardhi na mipaka ya utawala kwenye maeneo mbalimbali nchini. Tuna migogoro kati ya vijiji na vijiji, migogoro kati ya Wilaya na Wilaya, hata Mkoa na Mkoa, ukiwemo ule mgogoro wa Wilaya ya Kiteto na Kilindi ambao pia tulishautafutia ufumbuzi. Nilitoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya, nitoe wito tena kwa Wakuu wa Mikoa ya Manyara na Tanga; na Wilaya za Kiteto na Kilindi, wamalize huo mgogoro kabla sijarudi tena huko ili ufumbuzi upatikane na wananchi waweze kufanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiwa nahitimisha, nimesikiliza na kufuatilia kwa umakini sana mjadala huu kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 mpaka 2025 itatatekelezwa vyema chini ya Jemedari wetu, Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Saluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wakati wote tunakuwa katika Vikao vya Bunge, tutakuwa tunaendelea kushauriana na pia kuona namna nzuri ya kutekeleza maeneo haya kupitia ushauri wenu na namna ambavyo mnaweza kuisimamia Serikali yetu kupitia Kamati zetu.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanayo imani kubwa sana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana na mwanzo mzuri aliouonyesha Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, imani hiyo ya wananchi haina budi kuwa chachu kwetu katika kuwatumikia kwa ubora zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine mwelekeo wetu ni mzuri, suala la msingi lililo mbele yetu ni kuongeza umakini na kasi ili malengo yote tuliyojiwekea ambayo dhamira yake ni kuwaletea maendeleoo wananchi na Taifa kwa ujumla yaweze kufikiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 7 Aprili, mwaka huu 2021 tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 47 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na tarehe 12 Aprili mwaka huu, 2021 tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 37 ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Watanzania tunaendelea kuwakumbuka viongozi hawa kwa mchango wao mkubwa katika kutetea wanyonge na kudumisha misingi ya Imani, mshikamano na umoja wa Kitaifa ambao tunao. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, turejee kauli ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa wakati huu tuendelee kushikamana, kusimama na kuwa wamoja katika Taifa, kuonyesha upendo wa undugu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu, Utanzania wetu na kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu siyo wakati wa kuonyesheana vidole, bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele. Kwa msingi huo, tuendelee kudumisha na kuilinda amani ya nchi yetu ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za waasisi wa Taifa hili. Tutumie muda mwingi kwa kazi zaidi na kujipatia kipato na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja kuliko vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, nawakumbusha Waheshimiwa Mawaziri, Viongozi na Watendaji wote waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, mnalo jukumu kubwa sana kuwahudumia wananchi na kuhakikisha mnasimamia ipasavyo miradi iliyoanzishwa kwenye maeneo yenu na kushughulikia changamoto zote katika maeneo yenu na pia kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yenu.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo yanayoendana na thamani ya fedha za walipa kodi. Ndiyo namna bora ya kurudisha shukrani kwa wananchi waliotupa ridhaa ya kuwatumikia.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kusisitiza kuwa tukiwa watumishi wa Umma, tunao wajibu wa kuwapokea, kuwasiliza na kuwahudumia wananchi waliotupa dhamana hii ya uongozi. Kwa hiyo, tufanye kazi, tena kwa bidii zaidi, tuache mazoea ya kiurasimu ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kutumia nafasi hii kuwatakia Waislamu wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ulioanza katikati ya wiki hii. Natoa rai kwamba tutumie kipindi hiki kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu, aendelee kuwalinda viongozi wetu na Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, kadhalika, tumwombe Mwenyezi Mungu awajaalie wote kwa hekima na busara ili tuendelee kuliongoza Taifa letu kwa haki kujenga umoja na mshikamano kudumisha amani katika nchi yetu pamoja na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nihitimishe kwa kutoa tena shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, timu yote ya Bunge ikiongozwa na Katibu wa Bunge, Watanzania kwa ujumla, ndugu Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, napenda mtambue kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu muda wote ipo wazi, iko tayari, kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia. Tunaendelea kushirikiana na kila mmoja kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, kwa unyenyekevu mkubwa kabisa naliomba sasa Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili tuweze kuchapa kazi, taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge letu Tukufu kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 13 mwezi huu wa Nne 2021ili tuchape kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.