Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa kuandaa hotuba hii. Najua muda ni mfupi sana, mambo ni mengi lakini nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianzia kwenye ile hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna picha pale imeonyesha kwamba kuna mmoja wa wabunifu akiwa katika kiti cha walemavu ambacho alikibuni katika sherehe za kitaifa za sayansi na teknolojia mwaka 2020. Sasa napenda kufahamu hawa watoto wetu wanaonyesha ubunifu na pengine na Watanzania wengine wengi, je, baada ya ubunifu huu nini kinaendelea, ni faida gani au tija gani inayopatikana baada ya ubunifu huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu. Napenda kuzungumzia kuhusu suala la uendelezaji elimu ya msingi pamoja na sekondari. Katika ukurasa wa 7 wa hotuba hii Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba wamepeleka walimu 174 wa shule za sekondari ambao wamejengewa uwezo wa huduma za unasihi mashuleni. Mimi naishauri Serikali, tatizo la wanafunzi wetu ni kubwa yaani wana mazonge makubwa sana, kwa hiyo, wanahitaji sana kupata watu wa kwenda kuwaambia yale mambo yanayowasibu. Kwa hiyo, hii idadi ya walimu 174 kwa kweli ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba kama ikiwezekana ingewekwa programu maalum ya kuweza kuwafundisha walimu wengi zaidi hii elimu ya umahiri katika suala zima la unasihi ili kusudi walau kila shule ya msingi, sekondari na katika vyuo wawepo walimu hawa waweze kuwasikiliza hawa watoto na vijana wetu kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana. Ikiwezekana walimu hawa wa unasihi wawe wengi, wawe zaidi ya wawili au watatu ili mwanafunzi akiwa anahitaji huo unasihi aone ni mwalimu yupi ambaye anaona yeye mwenyewe anafaa kwenda kumpa ile shida yake aweze kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naipongeza sana Wizara kwa sababu mimi professionally ni mwalimu najua tulikotoka, hali kwa kweli imebadilika. Haya yote tunayazungumza tunaishauri tu Serikali ili kusudi kuweza kuboresha zaidi. Jamani, mimi nilikuwa mwalimu mwaka 1984 sasa nikiangalia hii trend Wizara you deserve all the best. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesema kwamba imetoa mafunzo kwa walimu 1,076 ili waweze kuwafundisha wanafunzi wasioona, wenye ulemavu wa akili na ambao wana matatizo mbalimbali ya ulemavu. Naomba nitoe ushauri kwa sababu watoto wenye mahitaji maalum wako wengi na sisi tunahamasisha sana hili suala la elimu jumuishi ni vizuri kama Serikali au Wizara ikaona kuna muhimu kuwe na basic knowledge yaani ianzie katika mitaala ya elimu ili kusudi kila mwalimu aweze kupata basic knowledge ya jinsi gani atakavyoweza ku-deal na hawa watoto wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kabisa sasa hivi kwa mfano hii elimu ya alama, kwa kweli elimu ya alama inahitajika sana. Kwa hiyo, kama watu wakipata zile basic skills ikawekwa kabisa kwenye mtaala ikawa compulsory ingawaje kuna wengine ambao watakuja kubobea basi ni budi Wizara ikaona kwamba at least katika mitaala kukawa kuna ulazima wa kusoma masomo hayo ili kusudi walimu wote ikiwezekana wawe wana zile basic knowledge za jinsi ya ku- deal na hawa watoto wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia kuhusu suala la mitaala, wenzangu wengi sana wamezungumzia, kwa kweli sisi tunaendelea kuishauri Wizara ijaribu kuona kwamba hii mitaala irekebishwe ili kusudi iweze kuendana na mahitaji ya sasa. Tumeona kabisa kwamba nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati na hii mitaala lazima iangaliwe upya. Tunajua kabisa kwamba kuna stadi zimewekwa kule basi ni budi sasa kuangalia stadi nyingi zaidi ili kusudi hawa watoto wetu zile stadi wazitumie kujiendeleza badala ya kusema kwamba wanategemea kazi za kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nilitamani na walimu pia ungewekwa utaratibu maalum wa refresher course za mara kwa mara. Hizi courses zitawasaidia kupata uwezo mzuri zaidi wa kuweza kuendana na hii hali halisi ya sayansi na teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hili suala la kisomo chenye manufaa. Nakumbuka miaka ya nyuma kulikuwa kuna utaratibu wa kisomo chenye manufaa kwamba kuna wale watu ambao hawakupata fursa ya kusoma basi kuwe kuna utaratibu kwamba ikifika wakati kuna masomo yale ya jioni, kulikuwa kuna walimu na Waratibu Elimu Kata wakifanikisha hilo. Nakumbuka kipindi cha Rais Marehemu Julius Kambarage Nyerere kuna baadhi ya wanafunzi waliokuwa bora walikuwa wanapelekwa kwenda kufundisha kwenye ile elimu ya Ngumbaro. Ili kupunguza watu wasiojua kusoma na kuandika ni budi basi Serikali ikaona kwamba inafufua vipi hiki kisomo chenye manufaa. Kwa hiyo, huo pia ulikuwa ni ushauri wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nataka kushauri kwenye upimaji wa umahiri katika ngazi ya chekechea. Tunajua kabisa kwamba Serikali ina lengo zuri sana la kutaka kuona kwamba tunapata msingi mzuri hasa kwenye hii elimu ya chekechea. Najua kabisa katika elimu ya chekechea kuna umahiri ambao unapimwa kwa wale watoto kwa mfano, umahiri wa kutunza afya zao, kutunza mazingira, kuwasiliana, kuhusiana na kutumia zana za hisabati na kumudu stadi za kisanii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pale natamani hapa ndiyo tuweze kujua vipaji vya wale watoto wetu tunapoanzia nao kuanzia chekechea. We build up from there kwamba akipelekwa kwa yule mwalimu wake anayemfundisha darasa la kwanza akaambiwa kwamba huyu kipaji chake ni muimbaji mzuri tunaanza kumuanzishia pale. Huyu ameonesha kukaa sana na vifaa vya magari basi tumpeleke katika trend ile. Kwa hiyo, natamani Wizara au Serikali ione umuhimu sasa wa kuwaangalia hawa watoto tunawaendelezaje kutokea pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani nitoe ushauri kuhusiana na suala la hawa wanafunzi ambao pamoja na upimaji utakuta kuna wengine hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Nafahamu kwamba Wizara imeweka utaratibu kama ikitokea hivyo mtoto wa darasa la kwanza au la pili anaweza kukaririshwa lakini kama maendeleo yake bado duni tunafanyaje? Ni vizuri sasa tuweke utaratibu au kuweka madarasa maalum ili kuweza kuwasaidia hawa watoto ambao wana uwezo duni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua muda ni mfupi sana naomba niunge mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)