Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara hii. Naomba nianze kwa kusema naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, Sera yetu ya Kilimo hapa nchini inasema kwamba Mgani Mmoja, Kijiji Kimoja. Kama tunavyofahamu, tuna vijiji takribani 12,000 lakini hadi sasa tuna wagani 7,000; kwa hiyo, tuna upungufu wa wagani kama 5,000.

Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa napenda kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, hususan Mheshimiwa Waziri, Prof. Adolf Mkenda, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Hussein Bashe, kwa jitihada kubwa walizoweka kuleta mageuzi kwenye huduma ya ugani, ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya kuwanunulia hawa Maafisa Ugani vitendeakazi kama pikipiki. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kuna changamoto ambayo naiona. Hii changamoto ni kwamba tunategemea Afisa Ugani huyu awe mtaalam wa kila kitu; ajue mazao yote, ajue masuala ya mbolea, masuala ya wadudu, masuala ya madawa, fungus, ukungu na kadhalika. Jambo ambalo siyo rahisi.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka miaka ya nyuma Serikali ilishaliona hili na ilianzisha kitu kinachoitwa Ward Agriculture Resources Centers, yaani Vituo vya Rasilimali ya Kilimo ngazi ya Kata. Kama sikosei vituo hivi vilianzishwa kwenye kata 200 hapa nchini. Pamoja na kuanzisha vituo hivi Serikali iliweka watalaam kwenye vituo hivi na iliweka vitendea kazi kama kompyuta, generator, screen za kufundishia na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Wizara kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wamesema wanaenda kuvifufua hivi vituo, lakini ningependa kushauri kwamba, ni lazima Wizara iangalie hivi vituo kweli vifanye kazi ambayo ilikusudiwa. Nasema hivi kwa sababu hivi sasa, kwa kuwa hivi vituo vipo chini ya halmashauri, kwenye halmashauri nyingi vituo hivi havifanyi kazi iliyokusudiwa ya kuendeleza kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano pale Chamwino, kituo hiki badala ya kufanya kazi ya kuendeleza kilimo kinatumika na TARURA. Kwa hiyo ningependa kuishauri Serikali ipitie upya vituo hivi na ione kama vinatumika kadri ambavyo inafaa na kama kuna changamoto basi vituo hivi virudishwe viwe chini ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo hapo kwa miaka mingi sasa halmashauri zimekuwa hazitengi bajeti ya huduma ya ugani, ambapo hii ni changamoto kubwa na hatuwezi kuendeleza kilimo wakati ni hizi halmashauri karibu asilimia 70 ya mapato yao ya ndani yanatokana na kilimo, lakini utengaji bajeti wa huduma ya ugani hawatengi. Kwa hiyo hili nalo ningependa katika kuhitimisha najua linahusu zaidi Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Mheshimiwa Waziri yupo hapa pengine atatuambia anapanga vipi kuhakikisha kwamba hizi halmashauri zinatenga bajeti ya huduma ya ugani. Naamini kwamba lengo zima la kuanzisha vituo hivi lilikuwa ni kuhakikisha tunaimarisha huduma ya ugani. Tukifanya hivyo tutaweza kuongeza tija na muhimu zaidi kuongeza pato la mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo langu la pili ambalo ningependa kuchangia ni pato la mkulima. Kwa muda mrefu sana tumekuwa tukiongelea bei ya mkulima na kabla sijaingia hapa Bungeni nilikuwa nafanya kazi kwenye Shirika ambalo lipo chini ya Wizara ya Kilimo SAGCOT yaani Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania kama Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Wezeshi kwenye Biashara, nimefurahi nimemwona bosi wangu Mr. Geofrey Kilenga yupo ndani ya ukumbi huu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kipindi kirefu tunaongelea bei ya mkulima, lakini nadhani wakati umefika sasa tuongelee pato la mkulima, kwa sababu tunapoongelea pato la mkulima lina variable mbili. Variable moja ni price, variable ya pili ni quantity and quality. Sasa tumekuwa tukiweka jitihada kubwa sana kwenye bei, tunasahau hii variable ya pili ambayo ni muhimu ya quantity and quality.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu wengi wameongelea tija yetu ya kwenye kilimo, nitatoa mfano mdogo, wenzetu wa Zambia kilo moja ya mahindi wanauza Sh.250 mpaka Sh.300 ya Tanzania na wenyewe wakiuza kwa bei hiyo wanarudisha gharama zao zote yaani wana-break even, lakini kwetu sisi Tanzania ili kufikia hiyo break even point lazima kilo moja ya mahindi tuuze Sh.500.

Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo ipo hata kwenye pamba, nchi ambazo tunashindana nazo India, Brazil, China, Egypt, wao wanazalisha kwa eka moja kilo 1,000 mpaka kilo 1,250. Kwa hiyo wao wakiingia sokoni wanaweza wakauza kwa bei ya Sh.500 na waka-break even, lakini sisi kwa sababu tija yetu ni ndogo tunazalisha wastani wa heka hiyo hiyo moja kilo 250 hatuwezi kuuza kwa ile bei ya Sh.500 mpaka ifike angalau bei ya Sh.1,000.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo, ndiyo maana napendekeza kwamba ifike mahali Wizara ya Kilimo ianze kuongelea pato la mkulima na siyo bei ya mkulima. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuongeza tija ambayo itaongeza mchango katika pato la Taifa kwa sababu tunasema kila siku asilimia 65 ya Watanzania wapo kwenye kilimo, lakini bado tunachangia asilimia 27 tu kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo inatokana na kwamba tija yetu bado ni ndogo na hiyo inatokana kwamba kila siku wimbo wa Wizara ya Kilimo ni kwamba bei ya mkulima. Kwa hiyo naomba kusisitiza tutoke kwenye bei ya mkulima twende kwenye pato la mkulima. Na na… (Makofi)

SPIKA: Bei ya mkulima ndiyo nini?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, bei ya mkulima ni ile ambayo inakuwa inapangwa, yaani unakuta mkulima akishakuwa amepata mavuno, Wizara ya Kilimo inaitisha wadau, wanakaa halafu wanapanga bei ya mkulima. Kama wanaweza wakaitisha wakulima wazao wa pamba wanakaa wanapanga kwamba bei ya kilo moja ni Sh.1000 au wanaenda kwenye mnada. Sasa ninachojaribu kusema kwa kufanya hivyo hatukuzi tija inakuwa kama vile tunafidia ule upungufu wa tija ambao tulionao. Tukijikita katika pato la mkulima ina maana zile variable zote mbili, bei maana ya price, quantity na quality tutakuwa tumezifikia

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii na naunga mkono tena hoja. Ahsante. (Makofi)