Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Angeline Mabula kwa kazi yao nzuri sana waliyoifanya, kwenye Wizara ya Ardhi na kwa kweli wananchi wanawashukuru na mimi binafsi nawashukuru. Pia nawashukuru watendaji wote wa Wizara ya Ardhi, namshukuru Kamishna Mary Makondo na Naibu wake Nicholas Mkapa na watendaji wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kwenye Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kuchangia kuhusu ardhi yetu yetu ya Tanzania. Ardhi ya Tanzania iliyopimwa ni asilimia 25, ardhi nyingine iliyobaki haijapimwa. Ardhi ni mali, lakini ardhi hii pia ikipimwa mwananchi wa kawaida inamsaidia kupata mkopo benki. Pia ardhi hii ikipimwa inamsaidia huyo huyo mwananchi wa kawaida kwenda kulima mazao yake ya biashara, lakini pia na mazao ya chakula. Sasa basi ardhi yetu ya Tanzania na ukubwa wa eneo letu la nchi ni asilimia 25 tu ndio imepimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, iongeze nguvu kwenye kupima ardhi ili mwananchi wa kawaida aweze kufaidika na ardhi hii lakini pia ili Serikali yenyewe iweze kupata mapato. Kwa sababu ardhi inapopimwa mwananchi atapata hati anapopata ile hati anailipia kila mwaka na kuna mzunguko wa kulipia zile hati kila mwaka kwa maana hiyo Serikali itaingiza pesa, lakini pia huyu mwananchi atakuwa na uhakika wa eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, naomba kwenye bajeti ijayo Serikali kupitia Wizara ya Ardhi iongeze pesa ili maeneo mengi yaweze kupimwa nchini kwetu Tanzania. Liko tatizo ambalo ningependa kulizungumzia tatizo lenyewe ni kuhusu upungufu wa wataalam wa ardhi kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri nyingi nchini kwetu zina upungufu wa wataalam wa ardhi na wataalam hawa ni kuanzia Wapimaji, Wathamini na Warasimishaji. Hivyo basi inasababisha ucheleweshaji wa upimaji wa ardhi kwenye halmashauri zetu. Naomba tuweze kuwatumia wanafunzi wanaomaliza Chuo cha Ardhi cha Dar es salaam, wanafunzi wanaomaliza Chuo cha Mipango hapa Dodoma lakini pia wanafunzi wanaomaliza kile Chuo cha Morogoro pamoja na Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote hawa wanajua kupima hizi ardhi na wote wamesoma haya masomo ya kuthamini hizi ardhi, tungeweza kuwa-comodate hawa wanafunzi na kuwatumia ili waweze kupima ardhi yetu. Pia Serikali inawasomesha kwa mikopo, kwa hiyo wanapomaliza shule nafikiri Serikali ingewatumia hawa wanafunzi ili waweze kutusaidia tuweze kutatua hili tatizo la kutokupima ardhi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda pia halmashauri nchini kwetu Tanzania zijitambue kwamba zenyewe ndio zenye mamlaka ya kupima ardhi kwenye halmashauri zao. Hata hivyo, niliona bajeti ya halmashauri hapa wakati inapitishwa, halmashauri nyingi zilikuwa hazijatenga fedha za kupima kwenye maeneo yao. Niombe basi hizi halmashauri ziweze kujitambua na kupima maeneo yao ili wananchi waweze kufaidika na hayo maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kupima hayo maeneo niweze kutoa rai kwa halmashauri zetu kumekuwa na watendaji wengi ambao wanafanya kazi let say, mtu anafanya kazi pale kwenye Halmashauri ya Mji wa Mpanda anaweza akapima yale maeneo lakini hafikirii miaka mia ijayo hayo maeneo yatakuwaje. Naomba watendaji wa wataalam wetu wa kupima ardhi wanapopima ardhi waipime kwa kuangalia kwamba leo tupo na kesho tupo lakini tuangalie miaka 100 ile ardhi itatumikaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoharibu mji kwa sasa hivi unapima barabara ndogo, lakini labda hujaweka eneo la kuchezea watoto au eneo la kupumzika, matokeo yake tunakuwa na miji ambayo haina maeneo ya kupumzikia, lakini haina parking na wala haina maeneo ya kucheza Watoto. Tunakuwa na congested town na kurekebisha ni vigumu kwa sababu unakuta mji umeshapimwa huwezi kubomoa zile nyumba. Niombe sana wataalam wanapopima miji waliangalie hilo wasi-focus kuangalia sasa hivi waangalie hundred years to come huu mji utakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la vile vijiji ambavyo vinakua kwenda mji. Unakuta kata inaanza kukua, kuna majumba mazuri yamejengwa pale, unakuta kuna umeme na maji yamewekwa, lakini unakuta lile eneo halijapimwa, matokeo yake tunajaza squatter kwenye miji squatter nyingi na tunapokuja kuzirasimisha kunakuwa na matatizo ya upungufu wa pesa, lakini pia uthamini utakuta mtu amejenga nyumba yake nzuri lakini inathaminiwa kwa pesa ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba zile vijiji ambavyo vinaanza kukua kwenda kuwa miji hizi halmashauri ziwe zinaviangalia na kuvipima ili kupunguza ukaaji holela na kupunguza migogoro ya ardhi kwenye maeneo yetu na kwenye hiyo miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumizia hapa ni suala la hizi halmashauri ambazo zilikopeshwa pesa lakini hazijarudisha. Kwa sababu tunataka halmashauri nyingine zipate zile pesa ili ziweze kupima ardhi zao, tunaziomba zile halmashauri ambazo zilipewa pesa na Ofisi ya Ardhi ziweze kurudisha hizo pesa ili halmashauri nyingine ziweze kupewa hizo pesa na hizo halmashauri ziweze kupima maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuupongeza sana Mkoa wa Mbeya kwa sababu wao walipewa pesa, wamezitumia vizuri, wamepima na wamerejesha na walipata faida. Nawapongeza sana, lakini sipongezi mikoa kama ya Iringa na mingine ambayo Mheshimiwa Waziri aliiorodhesha hapo. Kwa hiyo niombe tu zile halmashauri zilizingatie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kutoa ushauri wa jumla kwa akinamama wa Tanzania. Napenda kutoa ushauri kwamba akinamama wa Tanzania, waume zetu wanapokwenda kununua ardhi basi tuhakikishe na sisi majina yetu yanakuwepo pale pembeni. Natoa ushauri huu kwa sababu akinamama wengi wamekuwa wakidhulumiwa nyumba, lakini wakidhulumiwa pia mashamba, lakini unakuta huyu mama aliolewa na huyu mtu akiwa kijana, wakaanza Maisha, wakanunua kiwanja kwa pamoja, lakini sisi kina mama kwa sababu huwa tunakuwa na tabia ile ya uvuvi wa kutaka kuweka majina yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nitoe wito, mume wako kama anataka kwenda kununua kiwanja basi mwambie na yeye aweke jina lako pale ili iondoe matatizo pale mmoja wenu anapoondoka duniani ili usiweze kufukuzwa. Naomba nitoe wito kwa akinamama wa kule Mkoani kwangu Katavi lakini pia kwa akinamama wa Tanzania na pia tusiwe wavivu wa kwenda kutafuta ardhi kwa sababu sheria haimkatazi mwanamke kununua ardhi wala kununua kiwanja, tusipende sana kuwatumatuma akinababa kaninunulie kiwanja halafu akifika pale haweki jina lako, matokeo yake unakaa pale after 40 years unaonekana kama wewe ni mpangaji kwenye nyumba ambayo mmejenga pamoja.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Sofia Mwakagenda.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa taarifa kwa mzungumzaji kwamba ni kweli anachosema kwamba sisi akinamama tujitahidi kuwaambia waume zetu watuandike majina. Hata hivyo, waume hawa Mheshimiwa Taska Mbogo wanapoenda kununua viwanja hawatuagi na wakati mwingine wananunua akiwa bahati mbaya amefariki unashangaa kumbe mko sita wakati wewe unajua uko peke yako. (Makofi/ Kicheko)

NAIBU SPIKA: Sasa Waheshimiwa Wabunge huu mchango, hakuna akinamama wanaotumwa na waume zao kwenda kununua ardhi. Mheshimiwa Taska Mbogo sekunde kumi kwa sababu kengele ya pili ilikuwa imeshagonga.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda nipende kusema tu kwamba naupokea vizuri sana mchango wa Mheshimiwa Mwakagenda, ni mchango wenye tija lakini na mimi pia niendelee kutoa wito kwa akinababa ili kuondoa matatizo unapotoka duniani na mke wako kupata shida kutoka kwa ndugu zako kumfukuza kwenye nyumba basi muweke mke wako kwenye hati ya nyumba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia, wito wangu kwa akina mama ni huu.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.