Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kwanza nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Hii imeonyesha jinsi gani migogoro ya ardhi ilivyopungua hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi tunajua ni asilimia 25 tu ya ardhi yetu ambayo imepangwa na kupimwa. Kati ya hizo, kuna viwanja 2,337,938 ambavyo vimepangwa. Tuna miliki zilizotolewa 1,557,819; tuna vijiji vilivyopimwa 11,743,000 ambavyo vimepimwa na kuandaliwa hati ya ardhi; na pia tuna hati zilizosajiliwa 868,474. Hii ni dalili tosha kuonyesha kwamba kazi ndani ya Wizara hii inafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 75 iliyobaki, nasema, kama Wizara imejipanga vizuri, lakini kuna watu au taasisi ambazo zinawarudisha nyuma. Kama wameweza kufanya kazi hii, naona kila mtu abebe mzigo wake mwenyewe, kwa sababu inafika sehemu mtu anafanya kazi lakini mwenzie anamrudisha nyuma. Yeye anashindwa kufanya kazi zake anamsababisha na mwingine ashindwe kufanya kazi. Hii ipo kwa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri. Wamepokea shilingi milioni 400 ili wapime hivi viwanja na kuvipanga vizuri, matokeo yake wamefanya vitu vitatu tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo kundi la kwanza ambao wamefanya vizuri, tunawapongeza. Kuna kundi la pili wamekwenda wamebadilisha matumizi kwa kuwasingizia Madiwani. Kuna kundi la tatu wamekamilisha ule mradi halafu wameanzisha mradi mwingine na pesa hawajarusdisha wakati wanajua kuna Halmashauri nyingine zinahitaji fedha hizi ili wapange miji yao vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakurugenzi hawa ambao wamekiri, mimi nasema kwa sababu niko kwenye Kamati ya TAMISEMI, tumewaita na kuwahoji, wamekiri lakini wanatoa kisingizio cha Madiwani. Sasa naomba wasiwasingizie Madiwani. Wao ndio Watendaji Wakuu na ndio wataalam, kwa nini wasingizie Madiwani wamebadilisha matumizi? Kama kweli wanafuata utaratibu wa Madiwani, mbona Madiwani wakisema tunawafukuza Wakurugenzi, wanaanza kusoma kanuni, sheria na taratibu ili mradi wabaki? Kwa nini na huku wasitoe utaratibu? Kwa nini wasiwaongoze Madiwani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafika sehemu agenda nyingi zinapokuja pale, mimi najua; kuna baadhi ya ajenda ambazo zinaletwa moja kwa moja na Madiwani, lakini kuna ajenda nyingine zinatoka kwenye Kamati ya Fedha na Utawala, wanakuja nazo pale kujadili; na wale ni wataalam tunategemea kwamba wataongea na Madiwani, watawaelimisha halafu Madiwani watafanya maamuzi. Ila wakishaona hii hoja ina maslahi kwao, basi wanawadanganya wale Madiwani ili mradi tu waseme ndiyo halafu waje waharibu. Katika hili Mkurugenzi mmoja, sina haja ya kumtaja jina au Halmashauri yake, anasema kabisa nimewasomesha Madiwani wakakubali, tumebadilisha matumizi; kwa sifa tu, wala hana wasiwasi wowote. Sasa kwa nini mwasingizie Madiwani?

Mheshimiwa Naibu Spika, itafika kipindi hapa akija Mkurugenzi tunamwambia njoo na Meya wako ili tuone ukweli uko wapi? Kwa sababu wale Mameya na wale Madiwani wenyewe hawapo huko ndiyo maana Wakurugenzi wengine wanasema sivyo. Kinachotakiwa sasa hivi, wale waliochukua shilingi milioni 400 za mkopo bila riba, warudishe ili wenzao waweze kufanya kazi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mnasema Serikali na Serikali mnashindwa kushitakiana, mimi nasema kwenye hili Waziri amtafute Waziri mwenzake wa TAMISEMI awabane Wakurugenzi wake fedha zirudi. Kuna miji mizuri sasa hivi inashindwa kuendelea kwa sababu haijapangwa. Watu wanapewa fedha wanabadilisha matumizi. Kama hamzitaki, kwa nini mlizichukua? Nasema kabisa mpango huu ni kumvuta shati Waziri wa Ardhi na Naibu wake ili kazi isiendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hii ardhi ni mali ya Halmashauri. Hawa Halmashauri ndiyo wanatakiwa wapange hapa kuna shule, hapa kuna zahanati, hapa kuna kiwanja cha michezo, hapa kuna soko, ni kazi ya Halmashauri. Cha ajabu wanapokaa kwenye bajeti zao hawapangi kwamba tunatenga kiasi hiki kwa ajili ya kupanga miji na kupima, wanasubiri mikopo ambayo hawataki kurudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili naomba Wakurugenzi ambao wamechukua fedha na hawajarudisha na pia wengine wamebadilisha matumizi, hatua za nidhamu zichukuliwe dhidi yao. Kwa sababu utawala bora ni pamoja na kuheshimu matumizi ya fedha na kuwa na nidhamu ya fedha na matumizi yake. Hatuwezi tukawa tunapitisha fedha halafu watu wanabadilisha matumizi, wengine wanakosa, yeye amekaa tu ame-relax anasingizia Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na taarifa hiyo, bado kuna suala lingine la ardhi ambalo wote mara nyingi tunalalamikia. Ndani ya Halmashauri mpangilio uko mzuri, kuanzia ngazi ya Halmashauri kwenye Kata, kwenye Vijiji mpaka kwenye Mitaa. Mtu anaanza kujenga wanamwona, anachimba msingi, anaweka tofali wanamwangalia, anapiga plasta wanamwona, anapiga bati wanamwona; akishahamia anaambiwa bomoa, hapa kuna barabara inapima. Hiyo mipango miji hamuioni? Kwa nini tuwatia hasara wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama utendaji upo na Maafisa Mipango Miji wapo, wakiona msingi umechimbwa, basi waende wakamwambie mapema hapa usijenge kuna barabara inapita, lakini siyo anamwacha amejenga mpaka mwisho, anamaliza, unamwambia abomoe, hela yenyewe ya kuungaunga, utabomoa mara ngapi? Sisi tunawajua Watanzania wenzetu. Pesa hatuna, kujenga kwenyewe kwa kudunduliza, kwa nini uningoje nipige bati ndiyo uniambie nibomoe? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hawa watu wa Mipango Miji huko wazunguke kwenye mitaa yao, maeneo ambayo wanaona haya kuna kitu kingine kinakuja wasiruhusu watu kujenga, wawaondoe kabisa. Hii inatokana na huo uzembe wa hizo fedha, badala ya kwenda kuwapangia watu wapate viwanja halali wanawaacha wanazagaazagaa tu wanajenga popote. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi ya kuongea kuhusu Wizara hii lakini kwa leo naomba niishie hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)