Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kwa kunipa fursa niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametufanya leo tuwepo asubuhi hii, na kipekee nikushukuru wewe namna ambavyo unaongoza Bunge lako zuri na zaidi pia niishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Waziri Mheshimiwa Mashimba Ndaki, pamoja na Naibu Waziri - Mheshimiwa Ulega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nichangie katika maeneo mawili ya uvuvi pamoja na ufugaji hususan katika Jimbo la Busokelo, lakini kabla sijafika huko ningeanza kwanza kwa kuishukuru Wizara mmetujengea majosho, mmetununulia majokofu ya chanjo, mmeanzisha mfumo ambao utatumika kwa wafugaji wote kwa ajili ya kuripoti maradhi yote ya wanyama kupitia mfumo huu najua Serikali itakuwa inapata taarifa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko na kilio cha wavuvi kwa muda mrefu hususan suala la nyavu. Siku za nyuma Serikali ilikuwa ikichoma nyavu ambazo hazijakidhi vigezo, lakini kwa bahati mbaya sana kulikuwa hamna uhalali ama uhalisia kwa nini wanachoma nyavu ambazo kimsingi kulikuwa kuna contradiction ama muingiliano wa kati ya Wizara pamoja na TBS. TBS wao wanatambua nyavu za milimita sita, lakini Wizara inatambua nyavu za milimita nane. Kwa hiyo, hawa watu wa Wizara wakienda kukamata nyavu kwa wavuvi wanaona hazijakidhi vigezo, lakini wakati huo yule anayetengeneza ama kutoka kiwandani China kwa nje ya box anaandika milimita nane, lakini kiuhalisia ndani ya box hizo nyavu inakuwa ni milimita sita. Kwa hiyo, ni hasara kubwa ambayo imetokana na kutokuwa na mahusiano kati ya Wizara pamoja na TBS ambavyo vyote viko chini ya Serikali. Nafikiri kuna haja ya jambo hili kuliweka vizuri ili tusiwatie hasara wavuvi wetu wakati ni makosa yetu sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka pia nichangie suala la uvuvi wa bahari kuu; kwenye Mpango wa Serikali mwezi wa pili nilichangia namna ambavyo bahari kuu (blue zone) inaweza ikaleta fedha nyingi sana katika pato la Taifa na niipongeze sana Serikali kwa kuchukua hatua madhubuti na wewe mwenyewe mwaka 2018 Bunge lako lilipounda Tume Maalum ya Masuala ya Uvuvi ilikuja na ripoti nzuri na ndiyo maana matokeo yake hivi leo Serikali imeamua kwenda kununua meli za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana katika jambo hili sina sababu ya kurudia tena takwimu hizo kwa sababu tayari ninaamini Serikali mnakwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichangie kwenye ng’ombe wa maziwa; Jimbo langu la Busokelo tunazalisha maziwa mengi sana na maziwa mengi sana yanapotea na kwa bahati mbaya sana nchi tunaagiza tena maziwa kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nataka nikupe taarifa takwimu zifuatazo; kwanza tuna ng’ombe 31,079; lakini kwa siku tunazalisha lita 124,320; kwa mwezi tunazalisha lita 3,729,600 ambapo kwa mwaka sawa na lita 44,755,200. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bei ya maziwa yanayozalishwa Busokelo kwa lita ni shilingi 600 na kwa bahati mbaya sana maziwa ambayo yanaingia sokoni kwa ajili ya kununuliwa kwa siku ni lita 5,000 kutoka lita 124,320 yanayonunuliwa pekee ni lita 5000 wakati kwa mwezi yananunuliwa pekee ni lita 150,000 kutoka lita 3,729,600 na kwa mwaka maziwa yanayonunuliwa ni lita 1,800,000 kutoka lita 44,755,200 sawa sawa na kusema tunapoteza kwa mwaka fedha za Kitanzania shilingi 25,773,120,000 ni fedha nyingi sana hizi.

Sasa swali ambalo Waziri uje uwaambie wananchi wa Busokelo na Watanzania; kwa nini tunaagiza maziwa kutoka nje ya Tanzania angali maziwa lita zaidi ya 42,955,200 zinazalishwa Busokelo kupitia njia ya zero grazing? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini Waziri utakuja na majawabu sawasawa ili tusiendelee kuagiza maziwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)