Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru kwa kuweza kuchangia Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo, lakini inawezekana Wabunge tukazungumza sana humu ndani, lakini bila kuelewa au kujua kwamba tunakoelekea kwenye Wizara hii ili kuleta tija ni wapi.

Mheshimiwa Spika, tunayo bajeti ya shilingi bilioni 121 bajeti hii kama itaweza kutoka kwa wakati na ikafika kwenye maeneo husika na ikaweza kufanya kazi haya mengine ambayo ni changamoto ndani ya Wizara hii inawezekana yakapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kule kwetu Mtwara tuna bandari lakini tuna bahari kubwa mno na bahari ile takribani ndani ya miaka miwili iliyopita tumeshakamata meli zaidi ya mbili na zile meli ni meli za kigeni zinakuja kuvua kwenye eneo letu. Lakini meli ya kwanza imekamatwa ikiwa ina tani zaidi ya 150,000 za samaki, meli kubwa na samaki hawa wanavuliwa kwenye bahari za kwetu lakini kikubwa zaidi ambacho tunaweza tukapiga kelele tunao wavuvi, wavuvi hawa ni wavuvi ambao tunasema ni wajasiriamali, lakini bado Wizara haijapeleka kuwatambua hawa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa mfano leo tunazungumza kwamba mvuvi anayekwenda kuvua ambaye hana boti ana mtumbwi tu tunamwambia aende akavue mita 50. Mita 50 unazizungumzia pale Nungwi na mita 50 ili aweze kuzama mita 50 lazima awe na mtungi wa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwangu pale Mtwara hawa wavuvi hakuna aliyeruhusiwa kuingia baharini na mtungi wa gesi. Sasa tukienda Dar es Salaam tunakuta kuna wavuvi ambao wanatumia mitungi ya gesi, sasa sielewi hizi sheria zinafanyaje na tunaangalia wapi watu wanahaki na wapi watu hawana haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna suala la uvuvi wa usiku, leo ukienda Dar es Salaam wako matajiri wakubwa wanavua mchana na matajiri wale wana maboti makubwa na wameruhusiwa, na kazi hii yote anafanya Katibu Mkuu ndiyo mwenye maelekezo ya kuwaelekeza kwamba matajiri waende wakavue mchana, maskini waende wakavue usiku, athari za uvuvi wa usiku kwasababu unapokwenda kuvua usiku, sisi ni watu wa baharini kuna maeneo yanakuwa na miamba, unapokwenda na jahazi au na chombo mwamba huwezi kuujua usiku, lazima ufike mahala uchemke ndiyo utakapojua kwamba hapa ninapoelekea pana mwamba.

Mheshimiwa Spika, Mtwara yenyewe ukizungumza Kilambo, Mtanga Mkuu, Kianga, Mikindani hapa ninapozungumza takribani ya watu zaidi ya 100 wamepotea baharini, wamefariki. Sasa huku tunakokwenda tunakoelekea Wizara yetu bado haiwawezeshi wavuvi wadogo, kinachofanya sasa hivi Wizara bado inakwenda kuwamaliza wavuvi wadogo.

Natoa mfano hawa wanaumoja wao wana asasi zao, lakini leo Katibu Mkuu unashindwa kuwaita viongozi hawa wa wavuvi mkakaa nao mkajadiliana. Lakini ukiangalia kwenye mijadala yao yote, katika paper zao zote ni za kiingereza, wale wamesoma darasa la nne hamna aliyefika hata darasa la saba wale viongozi wote wa uvuvi, wanakwenda kuelewa kitu gani? Lakini mnapitisha mle sheria, kwamba hatuwezi kuvua hapa na ring net. (Makofi)

Mheshimiwa Hayati Magufuli wakati akiwa kwenye Wizara hii alileta hapa waraka na mkakubaliana Bunge zilizopita kwamba ring net iwe sahihi kwenda kuvua sasa leo kwanini nyavu za ring net zinapigwa marufuku na wavuvi wanakamatwa? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Hassan.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)