Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu. Mwaka 2012 nilipata nafasi ya kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na USAID pamoja na SAGCOT pale Ubalozi wa Marekani, wakati huo mimi nilikuwa msimamizi wa Idara ya Ukuzaji Biashara M-Pesa na nilikuwa nimekwenda pale kwa sababu ya kutaka kusaidia sekta ya kilimo ili kuona namna gani kwa kutumia mtandao tunaweza tukawasaidia kutoa taarifa mbalimbali zinazohusiana na kilimo, upatikanaji wa ardhi na pembejeo na vitu vingine kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, katika kikao kile alikuja Mkuu wa USAID duniani wa 16 kwa wakati huo, alikuwa anaitwa Rajiv Shah. Katika mazungumzo yake nilimsikia akisema: “I am not convinced with a progress of SAGCOT and I therefore consider to withdraw.” Akiwa anamaanisha kwamba hakuridhishwa na hatua ambayo SAGCOT walikuwa wameifikia wakati ule na naamini alisema statement hiyo pengine wao walikuwa ni wafadhili wa huo mradi.

Mheshimiwa Spika, Nini ambacho hakuridhishwa nacho? SAGCOT ilitakiwa iandae ardhi kubwa kwa ajili ya uwekezaji, lakini mpaka wakati ule SAGCOT ilikuwa haijafanya hivyo na wawekezaji wa Marekani inaonekana walikuwa wanataka ardhi kubwa. Unajua mwekezaji wa Marekani anaweza akawekeza Mkoa wote wa Dodoma sasa SAGCOT ilikuwa haijafanikiwa kufanya hivyo kwa hiyo, inaonekana USAID walisema wanataka kujiondoa.

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu ni nini katika chombo hiki? Hiki chombo ni muhimu na kiliundwa katika Awamu ya Nne ya Serikali yetu na nia yake ilikuwa ni kutaka kusaidia kilimo kiweze kukua, kutafuta masoko na ardhi ya uwekezaji. Sasa nataka niiombe Serikali katika chombo hiki ione uwezekano wa kukifanya chombo hiki kifanye kazi. Kama kwenye umeme kuna Mfuko wa REA, kwenye maji tumeweka RUWASA, lakini pia kwenye barabara tumeweka TARURA na kwenye kilimo tuitumie hii SAGCOT ili iweze kuwasaidia wakulima kutafuta masoko lakini kuleta wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa maendeleo tumesema hivi, kwamba tunataka tuandae mazingira wezeshi lakini pia tutafute ajira kwa ajili ya vijana pamoja na masoko, ukileta wawekezaji wakubwa huitaji kuisumbua Serikali kutafuta masoko kwa mfano ukienda pale Rungwe nilishakutana na mkulima mmoja anaitwa Robert Kruga yeye alitoka Zimbabwe analima pale anasoko lake yeye mwenyewe kwa wiki nafikiri anatakiwa kupeleka makontena 50 Ulaya ya Parachichi. Kwa hiyo, ametengeneza wakulima wengine wengi out growers hatuhitaji Serikali maana kule jamaa tayari ana soko.

Mheshimiwa Spika, ukienda Iringa pale ipo Asasi yeye anafuga na anatengeneza hizo yogurt lakini sasa hivi anapata lita 40,000 kwa siku na yeye anataka lita 100,000 kwa hiyo ametengeneza wafugaji wengi ili wamsaidie kupata maziwa na bado hayatoshelezi. Kwa hiyo, maana yake hii SAGCOT kama tunaiwezesha ikapata fedha lakini zamani nimeangalia hapa hii SAGCOT imekuwa ina guarantee ya Serikali ukiipa guarantee hii SAGCOT unaiwezesha iende ikatafute wafadhili yenyewe ili ikipata wafadhili wawekeze kwenye kilimo na hawa SAGCOT wakipata fedha hii SAGCOT catalyst fund itaweza kwenda kuwakopesha wakulima, itaenda kutoa elimu na kuweza kuwatafutia masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta kwamba hatuna haja sasa ya kuona kwamba hawa wakulima wanahangaika na soko au wahangaike kwenye mabenki kupata zile riba kubwa na za muda mfupi SAGCOT inaweza kuamua kwamba iweze kutoa riba za muda mrefu na kuwasaidia wananchi. Lakini pia ukitengeneza viwanda vidogo vidogo kwenye kilimo soko litakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe mfuko huu wa SAGCOT uwezeshwe na Serikali na mpango wake wa kwanza ulikuwa kwamba huu mfuko ushughulikie sekta zote Mifugo pamoja na Kilimo, na kwa mpango huo nilikuwa ninashauri ikiwezekana huu mfuko usikae kwenye Kilimo ukae kwa Waziri Mkuu ili aweze kuuratibu kwa sababu sasa ushughulikie sekta zote na uweze kwenda nchi nzima usiende Nyanda za Juu Kusini peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na mengi naona muda wangu hautoshi ni hilo tu moja linatosha kuchangia kwa leo pengine mengine nitaandika ili Serikali iweze kuangalia nini cha kufanya, naunga mkono hoja ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)