Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Daniel Awack Tlemai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa nafasi kuweza kuchangia wizara hii ya kilimo. Katika Jimbo la Karatu tunalima mazao kama aina takribani nne hivi, tunalima mbaazi, tunalima ngano, tunalima vitunguu na tunalima mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kilimo hiki cha kitunguu kipo Tarafa ya Eyasi na ni tarafa ambayo ina-history kubwa kwa sababu ni tarafa inayolima vitunguu Afrika Mashariki inasambaza kwa mwaka mzima. Na kama alivyoeleza mzungumzaji aliyeongea kwamba vitunguu vyetu vinaenda Kenya kwa asilimia kubwa sana, na soko letu kubwa lipo Kenya kwa asilimia kama 90 hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika eneo hili la kitunguu pale Bonde la Eyasi Serikali ina skimu ambayo imegharimu zaidi ya bilioni moja na andiko tumeandika wizarani mara nyingi kwamba sasa ile miundombinu ya zaidi ya bilioni moja naa katika Kata ya Baray imeweza kufukiwa na mafuriko kwa mbele sasa miundombinu ile kwa takribani sasa miaka mitano haiwezi kufanya kazi na tumetuma andiko wizarani kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini ukienda katika eneo hili la mbaazi kwa mwaka 2014/2015 mbaazi iliweza kufika shilingi 300,000 gunia moja mpaka shilingi 400,000 lakini kwa muda huu mbaazi inauzwa kwa gunia moja shilingi 25,000 mpaka shilingi 30,000, shilingi 35,000. Sasa nilikuwa nafikiri wizara wajiulize wale waliokuwa wanakula mbaazi 2014/2015 wamekwenda wapi au sasa kwenye nchi hizo nini kilichotokea kwamba mbaazi yetu sasa imeshuka kutoka shilingi 300,000 mpaka shilingi 400,000 kuja shilingi 30,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo la ngano, sisi ni wakulima wa ngano na kubwa sana wanalima katika Tarafa ya Bulumburu katika eneo hili la wakulima wa ngano watu wa TBL wanatoa vifaa vyote, lakini wameweka limit ukiivisha kwa heka moja wanasema usiivishe zaidi ya gunia saba, sasa wakulima wangu wao wanaivisha gunia saba mpaka gunia 10 mpaka gunia 12, lakini ukiivisha zaidi ya gunia saba, zile zingine zinazozidi hawataki kabisa na itakuwa ni mgogoro mkubwa katika Tarafa ile ya Bulumburu katika eneo hili la wakulima wa ngano.

Mheshimiwa Spika, sasa wenzangu watu wa wizarani wanatakiwa hilo waliangalie kwamba wanaweka limit kwamba heka yako ikitoa zaidi ya gunia saba ina maana hiyo utajua mahala pa kwenda kuuza, kwa maana watu wa wizarani waangalie sana hilo katika Tarafa ya Bulumburu na imetokea mara nyingi sana na mwaka jana ilitokea na kukatokea mgogoro mkubwa mpaka wananchi wale wakashindwa kulima zao hili la ngano kutokana na kwamba mgogoro unaotokea kwenye kampuni ya TBL. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo lingine la mahindi wizara sasa hivi bei ikiwa 20,000, 25,000 watasema mipaka ipo wazi, lakini ikatokea bei ikaenda kwenye 60,000, 70,000 wanafunga mipaka wakidhani kwamba ndani ya nchi hii kuna njaa ya chakula. Lakini, nashauri wizara kwa muda mrefu kama ilivyokuwa mpaka sasa uko wazi uweze kuwa wazi kwa muda wote wa miaka ijayo, ili wananchi hawa waweze kupata masoko yao maeneo mengine. Kwa wale wanaotokea Kanda ya Kaskazini na imetokea mara nyingi Mkuu wa Mkoa anaweza akatokea akasema kwenye ndani ya mkoa wake kuna njaa, wakati kuna maeneo mengine mahindi yanalimwa mengi yanatakiwa yatolewe kwenye hiyo mikoa mingine ziende kwenye mkoa huo ambao Mkuu wa Mkoa anajidai kwamba Mkoa wake una njaa.

Mheshimiwa Spika, sasa imeshatokea mara nyingi kwamba Wakuu wa Mikoa kusema mikoa yao ina njaa na kwamba watu wa mikoa mingine wanashindwa kuuza mazao yao iwe fursa kwenda kuuza mazao haya kwenye mikoa mingine ambayo ina shida ya chakula. Wenzangu wa Kanda ya kule Ruvuma watu jana waliongelea kwamba kule kwao mahindi yanakosa soko sasa kama kuna mkoa mwingine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawezi kufunga na imetokea mara kwa mara katika Mkoa wa Kilimanjaro, katika Mkoa wa Arusha, Tanga wakisema kwamba kwenye ukanda ule kuna njaa na mimi nadhani hakuna siku itatokea sisi watanzania tukaagize mahindi Kenya sisi tutaendelea kuuza mahindi Kenya na maeneo mengine kwa nchi zilizotuzunguka ndani ya Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana wenzangu wa wizara wasifunge mipaka hii kwa muda muda wafungue mipaka hii kwa muda wote wa miaka yote ambayo sasa wakulima wa Tanzania ili waendelee kupata fursa ya kuweza kuuza mazao yao maeneo mengine ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina mengi sana ya kuongea lakini wenzangu wa wizarani nilikuwa nafikiri kwamba sasa ni muda, lakini leo wametuletea makaratasi haya wakidai kwamba tuweze kuandika maeneo yenye skimu. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba, ina maana hii wizara haina watalaamu mpaka sisi wabunge watuletee ndiyo tuwaletee hapa kwenye Bunge hili tuwaandikie kwamba kuna skimu sehemu fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna vitu vingine vya kushangaza katika wizara hii ya Kilimo, leo Mbunge nilete skimu ina maana hakuna mtaalam kwenye Ukanda huu wa Jimbo la Karatu wa kuleta taarifa kwenye wizara hii kusema kwamba kuna skimu iliyolala, kunaskimu inayoendelea kufanya kazi, leo tunaletewa sisi Wabunge tujaze hizo nafasi kwa taaluma ipi tulizonazo sisi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wizara hii inatakiwa ijitafakari sana katika maeneo haya na naamini kwamba inaonekana uwajibikaji kwa watumishi wa eneo hili la kilimo wapo nyuma mno hawaendi na nchi hii ya Tanzania jinsi inavyokwenda. Watu wa wizara waangalie sana hili suala lakini vile vile ni….

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Daniel Awack.

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)