Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mie niweze kuchangia, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukuteuwa Profesa Mkumbo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, mimi binafsi naamini kwamba umefanya vizuri sana kwenye Wizara ya Maji, wakati ukiwa mtendaji. Imani yetu sisi wafanyabiashara kwenye kipindi chako hiki kwenye hii Wizara ya Viwanda na Biashara na kwa kuwa ni bajeti yako ya kwanza hatutakupiga mishale mikubwa sana, utegemee mwakani ndio utakutana nayo kama hutabadilisha haya mambo huko Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ningependa kumshauri Mheshimiwa Waziri afanyie kazi kwamba Serikali iongee lugha moja, shida ambayo uwa nazungumza mara nyingi kwamba yaani ukiangalia katika mfumo Wizara ya Viwanda na Biashara ni kama hauna kazi yoyote, kwa sababu watu wengi hawaoni umuhimu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sababu kila tatizo utakalokumbana nalo kwenye biashara lina Wizara yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikumbana na mazingira lina Wizara yake, ukikumbana na kodi lina Wizara yake, ukikumbana na Halmashauri lina Wizara yake. Sasa nikuombe, mnapoenda kukutana kwenye cabinet lazima ulilie power ya Wizara yako. Nakupa mfano Mheshimiwa Waziri, sasa hivi kuna mjumbe mmoja hapa amechangia, mnahamasisha watu wawekeze viwanda, lakini hivi viwanda mngekuwa mnazungumza lugha moja mngekuwa mnavipanga kiwilaya hata kimikoa. Ni kweli kwamba ni nani atakayefuata juice Geita akaiuze Dar es Salaam wakati juice hiyo hiyo inatengenezwa tena Dar es Salaam?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba mnatoa vitu ambavyo hamjapanga maeneo sahihi kwamba hiki kikae huku na hiki kikae huku. Lakini nikupe mfano tu sasa hivi kuna shida ya mnafungua refinery; nakupa biashara moja tu, refinery imejengwa Mwanza, imejengwa Geita, imejengwa hapa na ukiangalia kiuhalisia dhahabu nyingi inatoka Geita; kwa nini msingetengeza tu kama zone ya dhahabu mtalii yeyote au mnunuzi akija ukitaka dhahabu nenda Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unafungua refinery Geita, unafungua refinery Mwanza, sijui mtu wa Mwanza atatoa wapi hiyo dhahabu ya kutengeneza! Kwa sababu sisi watu Geita hatutakubali itoke dhahabu Geita ipelekwe Mwanza halafu Manispaa ya Mwanza ikakusanye levy yetu ambayo ingetengenezewa huku. Kwa hiyo ni vizuri mzungumze lugha moja na ukalilie madaraka kabisa kwenye cabinet kwamba na wewe ni waziri ambaye unaweza kujitosheleza.

T A A R I F A

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Taarifa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma taarifa tusikilize ya Mheshimiwa Almas.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji wa sasa hivi kwamba ilitokea hiyo tumbaku inalimwa Tabora, Viwanda vya Tumbaku vyote viko Morogoro. Tatizo kubwa sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma unaipokea hiyo taarifa?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea ndio maana nimemwambia Profesa tunakupa mwaka mmoja ukajaribu kurekebisha haya mambo tuwe na zone, kila kitu kipatikane mkoa fulani. Na hili la Mheshimiwa Waziri najua Serikali ilikuwa na nia nzuri sana ya kutaifisha viwanda na ninashukuru sana kwa sababu pia Katibu Mkuu wa sasa alikuwa Katibu Mkuu wa Fedha na Mheshimiwa Rais amekurudisha kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara na hili ujisifu, tunahitaji viwanda vifanye kazi, hakuna Wizara inayojisifu kuua viwanda, kuua taaluma unayoisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano Mheshimiwa Waziri mimi nina maslahi na kiwanda fulani kule Tanga kiwanda cha furniture, wakati Serikali inabinafsisha kazi ya mwekezaji ni kutengeneza, kazi ya kulinda masoko ni kazi yenu Serikali msikwepe majukumu. Huwezi ukanipa mimi kiwanda nikiendeshe kinatengeneza furniture, mteja mkubwa niliyemlenga ni Serikali, ninyi wenyewe mmetukimbia mnanunua vya Kichina, sasa lazima uzalishaji uwe wa kubambanya, lakini wewe unataka nizalishe kwa asilimia 100 hii kitu haiwezekani ni kazi yenu ninyi Serikali kulinda viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mkumbo ninatamani sana kukuomba ukatembelee Kiwanda cha Play and Panel pale Tanga kimefungwa kikiwa na malighafi eti kinazalisha asilimia 20. Twende Moshi pale Kiliwood imefungwa na Kiliwood iliuzwa na Serikali na ninyi wenyewe kwenye mkataba mkasema material mtamgawia ninyi kutoka kwenye mashamba yenu. Lakini mashamba yale material mnawagawia walanguzi mwenye kiwanda mnampa asilimia moja, sio sawa ni wakati tunaona sasa Serikali inafungua akaunti ilizozifunga hii ni hatua nzuri fungueni na viwanda. Hao mliowanyang’anya viwanda wengine wana uwezo, mliwasababisha kufunga viwanda ni ninyi kutokulinda soko la ndani. Huwezi ukanishindanisha mimi mzawa ambaye ninakopa CRDB mkopo asilimia 14 ukanishindanisha na mtu wa nje ana mkopo asilimia mbili, ni hesabu za design gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kuamini sana Profesa, ninakuomba utembelee hivi viwanda niko tayari hata kesho tufuatane mimi na wewe ukaone uonevu huo uliotokea huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Kiwanda cha Moproco pale Morogoro lazima tuwaambie ukweli, sijui ni hesabu za design gani na ndio maana mimi nikisema hapa mnanilaumu kwamba nawalaumu maprofesa, sitakulenga sana profesa kwa sababu wewe ni rafiki yangu. Kiwanda cha Moproco ni kiwanda cha mafuta ya alizeti, alizeti inapatikana miezi mitatu tu, mtu anataka kuzalisha mwaka mzima unatoa wapi hiyo alizeti? Ni jukumu la Serikali kuwahamasisha watu walime alizeti ili mtu azalishe miezi 12. Sasa ninyi mkikuta amefunga kipindi ambacho hakuna material mnamnyang’anya kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri dhambi hii ya kupora vitu vya watu isikuangukie mikononi mwako, kama Serikali imeanza kufungua akaunti kaa na Katibu wako mfungue hivyo viwanda, wapeni muda kama ni mwaka mmoja, kama ni miezi sita, wakope hela mambo yaendelee tumeshambiwa kazi iendelee halafu bado umeshikilia viwanda vya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine Mheshimiwa Waziri nikuombe sisi kule kwetu jimboni kwangu tutalima mananasi yanaliwa tu shilingi 200/shilingi 300, ukiingia kwenye internet Dubai kule nanasi linauzwa mpaka dola 15; ni kazi yenu Serikali kututafutia masoko. (Makofi)

Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uje uone mananasi tunayoyauza kwa mafungu kama mafenesi, njoo uone ili uone namna wataalam wako wakazunguke huko duniani tupate masoko tuweze kuuza bidhaa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Profesa nimesema wewe ni rafiki yangu lakini nikuombe sana mimi sio kwamba nadharau maprofesa, lakini vitendo vya maprofesa wakati mwingine ndio vinatufanya tulaumu hata kama mtatusema namna gani. (Makofi)

Naomba nitoe mfano mdogo tu wakati wa Marehemu Hayati Magufuli najua Marais wetu wanatupenda sana Watanzania wote, Mheshimiwa Rais aliunda tume ya kuchunguza corona, ikachunguza ile hatoe jibu kwa Watanzania, ikaja corona ya mapapai, ya mbuzi, ya maembe, na tukaona mpaka Mabunge ya Ulaya yanamsifu Rais Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sasa watu mkaanza kuchachamaa mitandaoni Mama yetu Samia naye ameunda tume, tume ya Mama Samia miezi mitatu baadaye tuchomwe sindano mnataka kumaliza sisi ambao sio wanasayansi. Sasa niwaombe sana wasomi wetu muwe makini, lazima muwe makini hatuwezi na Profesa miezi mitatu kasema corona ya mapapai huyohuyo miezi mitatu baadaye corona ya kuchoma sindano na ninamuomba mama sana atumie busara maprofesa hawa kama watamchanganya tuko huku kitaa tumsaidie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi chanjo zinasemwa tunachanjwa tupunguze nguvu za kiume na sisi bado tunataka kuzaa, Serikali inasema tuzae maprofesa mnatuchanganya. Mama achana na hawa ma-professor wametufikisha pabaya. Wazungu wenyewe walisifu Tume ya Marehemu Magufuli akasema mapapai na mbuzi. Mbunge lilijadili Bunge la Ulaya tunaona mitandaoni miezi mitatu baadaye tunang’ang’anizwa kuvaa mabarakoa, maprofesa hao hao. Sasa niwaambie na sisi Chama cha Waganga tutakaa na sisi tutoe taarifa yetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana ahsanteni sana. (Makofi)