Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya katika wizara hii pia na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia naomba nimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya. Tunao ushahidi mkubwa kwamba nchi yetu ilikuwa na giza, lakini sasa mwanga unaonekana, pamoja na kwamba zipo changamoto. Lakini nipongeze Serikali kwa kazi nzuri ambayo imefanywa ya kuhakikisha kwamba tunapata megawatt 2115 katika bwawa lile la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli huo utakuwa ni ufumbuzi wa kudumu kuondokana na giza tuliokuwa nalo katika nchi yetu, lakini pia ni kwamba kutokana na umeme ni mwingi ambao utakwenda kuuzwa katika nchi jirani maana yake bwawa lile litakwenda kuongeza pato la Taifa pale ambapo tutakwenda kuuza umeme katika nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo la kupongeza sana Awamu ya Tano ambayo iliingia mkataba na ilifanya maamuzi magumu kwa kuhakikisha kwamba bwawa lile linajengwa pamoja na kwamba mipango ile ilikuwepo kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia niipongeze Serikali kwa kuingia mkataba wa kuona namna ya kujenga ile eneo la Malagarasi pale Igamba ambayo kwa kweli ni katika Jimbo langu la Kigoma Kusini huu mradi unakwenda kutekelezwa kulingana na hotuba ya Waziri wa Nishati naomba Mheshimiwa Waziri mradi huu unaonekana utaanza Septemba mwaka huu na utakwenda kuisha Septemba tena 2024, maana yake ni miaka minne.

Mheshimiwa Spika, naomba Mkoa wa Kigoma umekuwa ukitumia mafuta, umeme wa mafuta kwa muda mrefu sana na ndiyo maana unaweza kuona kwamba kimkoa hatuna viwanda, isingewezekana kupata kiwanda au viwanda katika eneo ambalo tunatumia umeme wa mafuta. Ambao umeme wa mafuta una gharama kubwa sana katika uendeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo imani, kwamba mradi huu ambao una megawatt 49.5 utakwenda kuwa ufumbuzi na wa Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, lakini ninayo imani kutokana na bajeti yako na ulivyoonyesha, umeonyesha kabisa kwamba umeme wa grid ya Taifa utawahi kuingia Kigoma kabla ya mradi huu ambao utajengwa pale, pale Igamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona ulitakiwa kufanya ziara kwenye Mkoa wa Kigoma pale Nguruka ambapo tayari kumeshaandaliwa na palishajengwa kwa ajili ya kupokelea umeme ambao ndiyo utakuwa unapoozewa pale. Lakini ninayofuraha kuona kwamba mpango wako Mheshimiwa Waziri kuingiza umeme wa grid ya Taifa Kigoma maana yake upande mmoja wa Tabora unaingilia Nguruka ambapo ni kwenye Jimbo langu pale katika Kijiji cha Mgaza pameshajengwa tayari, compound imeshakamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini pia umeme mwingine wa grid ya Taifa unaingilia Kankoko kutokea Nyakanazi hii mipango miwili ikikamilika Mheshimiwa Waziri kwa kweli na sisi Kigoma tutakuwa tumepata ukombozi kutoka kwenye giza. Na ninayo imani sasa wawekezaji watakuja kwa ajili ya kuwekeza viwanda katika mkoa wetu ili na sisi mkoa wetu uweze kuinuka kiuchumi na wananchi wetu wa Kigoma waweze kupata ajira, kwa sababu bila viwanda ni vigumu sana kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo hili la Ujenzi wa Igamba nimefurahi kuona kwamba tayari fedha zimekwisha patikana kwa ajili ya fidia, wananchi katika eneo hili walitwaliwa maeneo yao kwa muda mrefu na walizuiliwa wasiendelee kwa hiyo walikuwa hawawezi kufanya chochote kwa sababu ya mradi huo, lakini naona kabisa kwamba sasa fedha ya fidia nayo pia imepatikana. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili uende kulifanyia kazi ili wananchi wale waweze kupata fidia katika maeneo ambayo waliyaachia kwa ajili ya mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu kuna vijiji 61 ni kweli vipo vijiji 17 tayari vimekwishapata umeme na maana yake kuna vijiji 14 bado havijapata umeme kabisa, lakini kwamba hata hivi vijiji 17 ambavyo vimekwishapata umeme ni katika maeneo tu kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu wanavyoongea. Na hii imetuletea malalamiko makubwa sana sisi Wabunge, tunalalamikiwa sana kwamba kwanini umeme unakuja hapa na baadaye kwenye vitongoji vingine umeme haufiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapata wakati mgumu katika kujibu maswali tunaomba Mheshimiwa Waziri hili jambo lifanyie kazi. Nafurahi kuona kwamba unao mpango mzuri kwamba tayari makandarasi wameshapatikana na nimekuwa nikikusumbua sana, lakini mpango wa Serikali ni kwamba umeme utapatikana 2022 kwa maana ya nchi nzima, kwa maana ya vijiji vyote.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba wakandarasi hawa ambao sasa wameteuliwa waweze kwenda kuondoa hizi kero pamoja na kwamba tunatakiwa tuendelee kumaliza vile vijiji 14, lakini pia huku kwenye vijiji 17 ambavyo tayari vina umeme lakini kuna maeneo mbalimbali hayana umeme katika vijiji hivi kwenye vitongoji na hiyo kazi pia iendelee kupunguza malalamiko.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Kigoma Kusini zipo Kata nne, Sigunga, Mgambo, Kalya na Igalula, kata hizi zinatumia umeme wa jua, wananchi hawa wamekuwa wakilalamika sana kila siku napigiwa simu kwamba kwanini mkandarasi huyu ambaye ni Jumeme kwanini anawauzia umeme unit moja shilingi 4000. Shilingi 4000 tunakuwa na bei mbili kwenye nchi moja hivi hawa wananchi tunawaonaje, tunawasaidiaje Mheshimiwa Waziri, nimekwisha kuja kwako mara nyingi sana, lakini ulionyesha kutatua tatizo hili na leo pia umetoa tamko, lakini pia bado nakuomba ziara yako ya kwenda Kigoma kutokea Tabora iendelee kuwepo na nitaomba nishirikiane na wewe unipe taarifa lini utakwenda nione uende kutoa tamko ili kusudi hawa watu wakome, wakome kabisa. (Makofi)

SPIKA: Ahsante, Ahsante Mheshimiwa Bidyanguze.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naoamba basi niweze kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)