Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Assa Nelson Makanika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kunipa nafasi niweze kuchangia wizara hii muhimu sana ambayo hakika ni injini ya uchumi ambao tunatarajia kuuendea kama Taifa, Uchumi wa Viwanda yaani Industry Economy.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naanza kwa kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi kwa ajili ya kuchangia katika wizara hii. Lakini jambo la pili naishukuru Serikali kwa jinsi inavyofanya kazi kwa mambo makuu mawili katika mkoa wetu wa Kigoma. Kigoma ilikuwa ipo gizani lakini mpaka dakika ya sasa Serikali imeweza kuchukua juhudi kubwa sana tunaunganishwa na umeme wa grid ya Taifa na hatua zinaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili kabisa ambalo ninaishukuru Serikali inayoongozwa na Jemedari Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kusaini mkataba wa kufua umeme katika chanzo cha Mto Malagarasi. Sisi Kigoma na location tuliyonayo tunaitegemea hii wizara sana kuliko kitu kingine, kwa sababu ukiangalia katika eneo lile tulilonalo la Kigoma na majirani tulionao bila hii wizara kututazama hatuwezi tukatoka mahala tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia tupo tumepakana na nchi jirani zile nchi zote ku-survive zinaitegemea Kigoma na haziwezi zika-survive bila Kigoma bila kuja kula Kigoma, lakini Kigoma haiwezi ikawalisha wale watu bila hii Wizara muhimu sana wizara ya Nishati. Nakumbuka nimejaribu kupitia sana hapo nyuma Mzee wangu Mwijage aliweza kuwa na wawekezaji kipindi yupo ni Waziri wa Viwanda alipata wawekezaji ambao walipaswa waje kuwekeza katika mkoa wetu wa Kigoma kwa ajili ya kuzalisha sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wale wawekezaji hawakufanikiwa kuzalisha sukari katika mkoa wetu wa Kigoma ukifuatilia vitu ambavyo vilivyo wakwamisha cha kwanza ilikuwa ni ukiritimba wa sheria za uwekezaji. Lakini jambo la pili ilikuwa ni kukosekana kwa nishati ya kuweza kusimika kiwanda cha kuzalisha sukari pale Kigoma, walishindwa lakini mpaka sasa kuna watu wanakuja kuchukua sukari Rwanda wanapeleka mpaka Zambia na wakati ilihali tungezalisha pale Kigoma, lakini hiyo yote ilishindikana ni kwa sababu hatukuwa na nishati ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo naomba nielezee hali halisi ya nishati katika mkoa wetu wa Kigoma. Katika mkoa wetu wa Kigoma tunatumia umeme unaotokana na ma-generator tuna vituo vitatu katika Mkoa wetu wa Kigoma, kituo cha kwanza ni Kigoma Mji na kituo cha pili ni Kasulu na kituo cha tatu ni Kibondo. Vituo hivi vyote vitatu vinauwezo wa kuzalisha megawatt 11.25, lakini na sisi mahitaji yetu kama mkoa tunahitaji kuwa na megawatt 10.57, pamoja na hayo yote bado watumiaji wameongezeka kwa kasi sana kutokana na kwamba Serikali imeleta kuwaunganisha wananchi wengi na watumiaji wengi wameongezeka kupitia mfumo huu wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na baada ya kutokana na hiyo ukija ukaangalia hiki kituo cha Kigoma Mji kinahudumia maeneo ya Kigoma Ujiji, kinahudumia na maeneo ya Wilaya ya Uvinza kinakwenda na sehemu ya maeneo ya Wilaya ya Buhigwe, lakini hiki kituo kina uwezo wa kuzalisha megawatt 6.25 tu, ili kiweze kuhudumia hizi wilaya tatu. Pamoja na hayo yote bado kinazidiwa, kinazidiwa kwa sababu hizi wilaya tatu zinazidi hizo megawatt zinazozalishwa na kituo hiki cha Kigoma Mji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kituo cha Kasulu kina mashine mbili nacho kinalisha Kasulu na kinalisha na sehemu ya Buhigwe, lakini ile mashine moja mpaka sasa haifanyi kazi iseme imekufa. Kwa hiyo, imebidi sasa TANESCO wachukue sehemu ya Buhigwe wairudishe Kigoma Mji mpaka dakika ya sasa wananchi wa Kigoma wananusishwa umeme. Jana umeme umekatika saa kumi na mbili wanarudishiwa asubuhi na imekuwa ni trend ambayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali hii iliyopo kuna minong’ono mingi sana huko kwanini umeme uanze kukatika sasa na kwanini haukuwa una katika hapo nyuma najua mlengo wa Serikali ni kwamba hakuna mgao wa umeme, lakini lazima tuzungumzie uhalisia kabisa ya kwamba upo umeme una katika na wananchi kila siku lazima umeme ukatike na shughuli zinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo ningeomba wizara iweze kulichukulia umaanani wake, ukija Kibondo kadhalika hivyo hivyo ina uwezo wa kuzalisha megawatt 2.5 hiki kituo cha Kibondo kinalisha Kankoko, kinalisha na Kibondo, lakini kinahitaji zaidi ya megawatt 3.2 ili kiweze kulisha hizi wilaya mbili nacho kinauwezo wa kulisha hii 2.5.

Mheshimiwa Spika,kwa hiyo, niiombe Serikali najua kuna namna ambavyo inataka kufanya kwa ajili ya kutoa mashine kutoka Loliondo kuja kuisimika pale kituo cha Kasulu, hilo ni zuri kabisa na ningeomba sana wizara iweze kuharakisha kwa sababu sisi Kigoma tumekuwa kwenye hii hali wakati ilihali wenzetu wananufaika na umeme grid sasa ningeomba hii bajeti iweze kuangalia a quick solution ya kuitoa Kigoma mahala ilipo mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuoneshe tu jambo dogo ambalo mpaka sasa ukija ukaangalia Serikali inatumia pesa za watu masikini kutumia kwa ajili ya kutumia haya ma- generator na kama ikiweza kuharakisha kwa mfano; grid ya Taifa wamesema kufikia Kigoma itakuwa imefika mwaka 2023 jambo ambalo ikifika mpaka huo mwaka tutakuwa tumesha hangaika vya kutosha. Ningeiomba Serikali ina uwezo kulingana na hii hatua tuliyonayo iweze ku-speedup huu mradi wa umeme wa grid ya Taifa angalau hata tufike 2022 uwe umeweza kufika ili kuweza kuwa na permanent solution katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka dakika ya sasa katika Mkoa wa Kigoma unit moja ya umeme inazalishwa kwa shilingi za kitanzania 645, lakini unit moja hiyo hiyo ya umeme ukienda Singida inazalishwa kwa shilingi za kitanzania 36 mpaka 50 na Serikali hii hii inaweza kutumia bilioni 1.6 kwa mwezi kwa ajili ya kuzalisha umeme katika Mkoa wetu wa Kigoma hizi ni pesa nyingi sana, kwa nini tusiharakishe sana ili umeme wa grid uweze kufika tuweze kuokoa pesa hizi na hatimaye mwananchi aweze kuona ya kwamba ana unafuu wa kuweza ku-utilize umeme katika mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri mambo machache sana katika wizara hii ili iweze kuyachukulia kwa uharaka sana ambayo moja itakuwa ni permanent Solution, lakini nyingine itakuwa a quick solution kwa ajili ya kuokoa hii hali inayotokana, inayojitokeza kila muda katika mkoa wetu wa Kigoma. Moja kabisa, ni kama nilivyosema ni kuharakisha huu mradi wa umeme wa grid ya Taifa ili uweze kufika kwa haraka sana hiyo ndiyo permanent Solution sisi watu wa Kigoma tutakayoiona ya kwamba mmetutoa kwenye giza, lakini jambo la pili ni kuweza kuharakisha hiyo mashine kutoka Loliondo iweze kufungwa pale katika kituo cha Kasulu ili tuweze kuepukana na hii hali ya umeme kukatika kila iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, na jambo la tatu kabisa na la mwisho, nimuombe Waziri pale kwetu Kigoma kuna muwekezaji ambaye anaitwa the next Solar Wazi Limited amewekeza pale Kigoma anauwezo wa kuzalisha megawatt 4 mpaka 5, lakini anazalisha chini ya megawatt hizo ambapo vilevile tumejaribu kumuona hapo miezi ya nyuma anasema ndio anaweza, lakini Serikali iweze kumpa ushirikiano ili aweze kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niombe Waziri uweze kuongea na muwekezaji ili aweze kuzalisha zaidi ya hicho kiwango ili tuweze kuepukana na hali ya mgao huu wa umeme katika mkoa wetu wa Kigoma.

SPIKA: Mheshimiwa!

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, kwa machache hayo naona muda umekimbia, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)