Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Suleiman Haroub Suleiman

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kutoa mchango wangu katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2021 - 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nakushukuru wewe kwa kuongoza kikao hiki kwa uweledi na Ufanisi. Nampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania kwa uongozi wake imara na wenye matokeo chanya kwa Taifa letu. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu wa Wizara na Watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani na pongezi hizo, nina michango, ushauri na maswali yenye lengo la kujenga, siyo kubomoa. Naishauri Wizara kushirikiana na Serikali za Mikoa, Wilaya na Mitaa. Lengo kuu ni kushajiisha utalii wa ndani, kwani wananchi wengi hawana uelewa juu ya dhana nzima ya utalii. Hivyo basi, Serikali hizo zitasaidia kushajiisha, kuhamasisha na kuelimisha dhana nzima ya utalii. Pia Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio Wenyeviti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa sehemu zao. Amani na utulivu ndio kitu muhimu sana kwa ustawi wa utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii ni sekta mtambuka, hivyo basi, naishauri Wizara kuendelea kushirikiana na baadhi ya taasisi ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya TAMISEMI, Kilimo na Ardhi, kwani itasaidia kufikisha huduma stahiki kwa watalii wa ndani na wa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara kuboresha miundombinu tofauti ikiwemo mawasiliano ya simu, barabara kwa baadhi ya hifadhi sambamba na sehemu za vivutio vya utalii. Kwani ukosefu wa Mawasiliano kutazorotesha uongezekaji wa watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na janga lililoikabili dunia, Covid 19, nashauri Serikali kuboresha utalii wa ndani kwa ushirikiano baina ya SMZ na SMT kwani kuna vivutio vipo Zanzibar ambavyo Tanzania Bara hakuna, pia vipo vivutio Tanzania Bara ambavyo Zanzibar havipo. Tubuni vivutio ziada vya Utalii, mfano ngoma za jadi ili kuhifadhi utamaduni, silka, mila na desturi, kuendeleza miradi kwa kiwango kizuri na kwa muda stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri nilioainisha hapo juu, napenda kutoa pongezi za dhati tena kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara. Nimefarajika kuona kunaanzishwa aina tofauti za utalii, ukiwemo utalii wa michezo, utalii wa fukwe na utalii wa meli. Swali langu ni: Je, meli kwa ajili ya utalii huo ipo wapi sasa hivi; na je, ina hadhi ya watalii wa kiwango gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hamwoni haja ya kuanzisha utalii wa tiba asili? Je, Wizara imejiandaa vipi kukuza utalii wa ndani kwa vitendo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawatakia kazi njema kwa maslahi ya uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.