Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi jioni hii ili nichangie mchango kidogo. Mimi ni Mjumbe kwenye Kamati ya Bajeti, nimepata fursa ya kuchangia mengi kuishauri Serikali, lakini kwa jioni ya leo naomba niongelee maeneo mawili.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea suala la TRA, kwanza naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote na Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake.

Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Wajumbe wengine ambao wamepata fursa ya kuchangia wakiomba TRA iwezeshwe kwa maana ya kuwa na watumishi wa kutosha. Tutakubaliana kwamba suala la kutoza kodi ni suala la kitaaluma, linahitaji mtu ambaye amebobea amesomea na yupo vizuri ili anayetozwa kodi awe comfortable kwamba natoa kodi katika mikono salama. Sasa kama tunataka kuongeza mapato ya kutosha ni vizuri tukahakikisha kwamba TRA inakuwa na watumishi wa kutosha wenye weledi ambao wamewezeshwa kibajeti ili wafanye kazi zao vile inavyotakiwa. Haiwezekani tukiwa tunataka ng’ombe atoe maziwa, lakini ng’ombe huyu tunasahau kumlisha. Ni wakati muafaka tuhakikishe kwamba TRA inakuwa na staff wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Benki kuu kwa maana BOT wamefanya kazi nzuri sana. Kila Mtanzania anajua jinsi ambavyo shilingi yetu imekuwa imara kwa kipindi kirefu. Kwa hiyo juhudi ambazo zimefanywa na BOT pamoja na Wizara ya Fedha katika kuhakikisha kwamba shilingi yetu ni imara ni jambo la kupongeza. Kuna baadhi ya jitihada ambazo zimefanyika zikaonekana kama vile zinaumiza, lakini malengo yake ni mazuri ilikuwa na uhimilivu katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunamaliza kwenye Kamati ya Wizara ya Kilimo, ulisema kwamba kama Bunge hili ili likumbukwe kama ambavyo Bunge la Kumi na Moja litakumbukwa kwa kufanya kazi nzuri kuhusiana na suala zima la Madini, Bunge la Kumi na Mbili lina wajibu wa kufanya mapinduzi katika suala zima la kilimo ambalo hakika linaajiri Watanzania wengi.

Mheshimiwa Spika, vile vile ukasema ni vizuri tukasubiri katika bajeti inayokuja, lakini nikawa nafikiria kwa sauti kidogo, kwamba hivi hapa tulipofika hakuna ambacho kinaweza kikafanyika ili fedha zikapatikana kwa ajili ya kwenda kufanya mapinduzi kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikasema nilishauri Bunge, kwa kupitia Benki kuu kwa maelekezo ya kisera, ukawa na incentive kwa mabenki ya biashara; mosi, kuhakikisha kwamba interest rate kwa wale wanaokwenda kukopa kwa ajili ya shughuli za kilimo zinashushwa kwa makusudi mazima ili watu wawe na appetite ya kwenda kukopa kwa ajili ya shughuli za kilimo. Pia ili mtu umkopeshe kwenye kilimo sio suala la mwaka mmoja, kwa hiyo ndani ya Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu waweke utaratibu ambao kutakuwa na appetite ya kukopesha hawa watu wanaokwenda kufanya shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka kwamba Wizara ya Kilimo wamekuja wakasema kwamba, sasa hivi Watanzania tuna quota ya kuuza soya beans China kwa miaka mitatu. Sasa kama tukaacha na hiki kipindi kikapita, maana yake tutakua tumebakia na mwaka mmoja. Wataalam wa Wizara ya Fedha na BOT waje na utaratibu ambao utahakikisha mabenki yaamue, kwa hili kwa dhati kabisa twende tukakopeshe watu ili wa-engage kwenye kilimo ukijua kwamba hakika zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wako kwenye kilimo. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Taasisi zake wachukue kama changamoto waifanyie kazi ndani ya muda mfupi ili msimu wa mvua tuanze kuona fedha zina-flow kwenda kwenye shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa leo nilisema niseme hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)