Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nianze mchango wangu kwanza kwa kuipongeza Wizara ya Fedha katika eneo kubwa moja, Wizara ya Fedha sasa imeona umuhimu wa kupeleka walau fedha kwa kiwango kidogo kwenye sekta ya ardhi ili kusudi tuanze kufanya vizuri kwenye ardhi. Pia niipongeze Wizara ya Ardhi, wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti yake ya Wizara aliona umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika upangaji na upimaji wa nchi yetu. Kwenye eneo hilo nampongeza sana Waziri na Naibu Waziri na Wizara nzima ya Ardhi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee tu ardhi namna gani itatupa fedha, sigusi eneo lingine siku ya leo. Naomba nianze mfano wa Japan, Japan kabla hawajakwenda kwenye mapinduzi ya teknolojia waliwekeza kwenye ardhi pamoja na kuwa na ardhi ndogo, ukienda pake Tokyo idadi ya wakati wa Tokyo inakadiriwa kuwa takribani milioni 30, ni eneo dogo sana lakini ardhi ile ya Tokyo imepangwa vizuri na majengo yakajengwa kwenda juu. Walivyoona ardhi haitoshi wakaenda kwenye mapinduzi ya teknolojia, leo hii Japan ni nchi kati ya nchi saba zenye uchumi mkubwa duniani.

Mheshimiwa Spika, nirudi nchini hapa kwenye ardhi yetu, inakadiriwa watu waliomilikishwa viwanja, waliomilikishwa Tanzania ni watu 1,500,000 tu katika population ya watu milioni 60. Sasa nazungumzia tax base; watu 1,500,000 ndio wanaweza kulipa kodi ya ardhi lakini pia transactions ambazo zinatuletea fedha kwenye transfer kwa mfano wanauziana viwanja watu hawa hawa watu 1,500,000 hawa hawa tu nchi nzima katika idadi ya watu milioni 60. Tufanye hesabu ndogo tu, tukiweza kufikia lengo walau tupate watu milioni 10 tu Watanzania, tuache kwa sababu population karibu watu milioni 67, utaona kuna watoto, kuna wazee, kuna vijana ambao hawawezi kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Spika, tuseme tu, tufikie uwezo wa kumilikisha watu milioni 10, leo hii nchi hii itakuwa na fedha kiasi gani? Milioni kumi tu, tusiende mbali zaidi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba returns on investment ya ardhi ni ya muda mfupi sana kuliko uwekezaji wowote nchini. Hata mtu mmoja mmoja tu, wenye ardhi, wewe mwenyewe utaona tofauti ya mtu mwingine.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nasema neno moja hapa. Narejea tena, mfano nimetoka Japan narudia hapa Tanzania, Dodoma. Sizungumzii mambo makubwa sana, hapa hapa Dodoma. Natoa mfano halisi; wakati Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu inakwenda kuondolewa, walifanikiwa kupima viwanja takriban 69,000 kwa miaka yote 43, lakini Manispaa na Jiji baadaye ikapima viwanja 200,000; impact imeonekana ndani ya miaka mitatu. Niliwahi kusema hapa Bungeni, viwanja 200,000 vilivyopimwa na Jiji la Dodoma hatukwenda kukopa fedha benki, hatukupewa fedha ya Serikali Kuu. Sasa nimempongeza Waziri wa Ardhi kwa nini? Alivyokiri kwamba Serikali peke yake haiwezi ikapima ardhi ya nchi hii, nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, kwamba sasa sekta binafsi ikapime. Mfano, nafikiri Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi wanaweza wakakubaliana pamoja kwamba tuna Halmashauri 100 au takriban 84; Makampuni haya ya upimaji yakakabidhiwa hizi Halmashauri. Kuna maneno yalikuwa yakizungumzwa kwamba wale Makampuni ya Upimaji ni matapeli. Kuna sehemu tulikosea ndiyo maana wakapata nafasi ya kutapeli. Leo hii Mkurugenzi wa Halmashauri akienda akaingia mkataba na kampuni, Mkurugenzi wa Halmashauri, yeye ni answerable. Wananchi wao wanataka huduma tu.

Mheshimiwa Spika, hapo awali tulikuwa tunasema Kamati za Ardhi, ngazi ya mitaa ziingie mkataba. Haiwezekani, ndiyo maana tuliona imeshindikana mpaka wakaanza kutapeli wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba na ni rai yangu, kwa dhati kabisa, model itakayotusaidia nchi hii kupata fedha nyingi ni ardhi. Tuache kote, tukiipima nchi yetu vizuri, kuna zile neighborhood zinazochangamka, Halmashauri za mijini mijini; ukienda pale na uzuri Waziri ameshatoa bei elekezi ya kulipia shilingi 150,000/=. Mwananchi wa kawaida akipimiwa kiwanja chake, shilingi 150,000 atalipa. Kwa sababu anaamini akipimiwa kiwanja ardhi yake inapanda thamani, atakopesheka, kama ni shamba atapata mkopo, atalima vizuri. Pia kama ni kiwanja, anaweza kukiuza kikawa na thamani ya juu zaidi, akawekeza kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, pia kwa faida ya Serikali; kiwanja kilichopimwa na chenye hati faida yake ya kwanza, Serikali inapata kodi ya ardhi ya kila mwaka. Sasa chukua kodi ya ardhi ya kila mwaka na hii ni kodi endelevu, huna haja ya kufanya mapitio tena. Kwa hiyo, ndani ya miaka yote wewe kodi ya ardhi unalipa tu. Kwa hiyo, niseme tu kwa dhati, ardhi ni sekta muhimu…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Ndiyo, taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri Ardhi.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji ya kwamba nia njema ya Serikali kushirikisha taasisi binafsi katika upimaji, nadhani tumeiona. Tume-engage makampuni Zaidi ya 163, lakini matokeo yake katika utekelezaji wao, zaidi ya asilimia 60 kama haifiki 70 kati ya 60 na 70 wote wameshindwa kufanya kazi yao vizuri na Serikali iliwaamini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika suala zima lile analolizungumzia, Serikali tayari ilishachukua hatua, lakini tunachohitaji sasa ni Halmashauri ambazo zinahusika kule kuweza kukaa na ile mikataba na wale watu kuweza kuwatambua badala ya kuwaachia wananchi. Ukiwaachi wananchi peke yake, zoezi haliendi. Kwa hiyo, tunahitaji commitment ya Halmashauri ambazo ndiyo Mamlaka za Upangaji, nasi ni Waheshimiwa Madiwani. Nadhani tukiweza kulisimamia kasi ya upimaji itaongezeka.

SPIKA: Mheshimiwa Kunambi unapokea taarifa?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimepongeza Wizara. Anachokisema Mheshimiwa Naibu Waziri ni cha msingi kabisa. Hapo mwanzo walipitisha Wizara ya Ardhi mwongozo unaosema, Kamati za Ardhi ngazi ya Vitongoji na Vijiji ndiyo viingie mikataba na ndiyo maana wananchi wakaanza kutapeliwa. Sasa Serikali imekwenda imepiga U-turn na ni jambo jema sana kwamba turudi sasa, kumbe tulikosea. Unaona!

Kwa hiyo, anachoeleza Naibu Waziri ni jambo la msingi kabisa kwamba sasa Halmashauri ndiyo ziingie mikataba kwa kupitia Wakurugenzi na siyo Kamati za Ardhi ngazi ya Vijiji au Mitaa. Huko tulikosea. Kwa hiyo, model hii mpya waliyokuja nayo, ndiyo maana nimepongeza Wizara ya Ardhi, ni nzuri kabisa kwa maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema nini hapa? Ninachoomba, Wizara ya Fedha iiongeze fedha Wizara ya Ardhi ili kusudi sasa kazi ya Wizara ya Ardhi isimamie upatikanaji wa hati kwa wakati. Kuna mfumo mmoja unaitwa ILMS (Integrated Land Management System). Mfumo huu ni mzuri sana. Tuliwahi kupata ufadhili tukapeleka pale Kinondoni, Kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla, umefanya vizuri. Leo hii nampongeza pia Waziri wa Ardhi, wameuleta hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu uzuri wake, Afisa Ardhi mmoja anaweza kutengeneza hati 300 kwa siku moja tu. Leo hii Afisa Ardhi mmoja anaweza kutengeneza hati tatu kwa siku, tena huyo ni mwadilifu sana. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, tupeleke fedha Wizara ya Ardhi waka- integrate huu mfumo nchi nzima. Kila Halmashauri, wakati sekta binafsi inakwenda kupima, viwanja vinapatikana, basi wananchi wapate uhakika wa kupata hati. Kwa hiyo, maana yake nini? Mfumo huu ukiwa kwenye kila Halmashauri nchini, maana yake hati itapatikana kwa wakati; na kwa sababu tunataka tupate hati, na Land Rent itapatikana na tozo ya ardhi itapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachokiomba kwa Waziri wa Fedha, kuna shilingi bilioni 50 nimesikia inaenda huko. Kwa hiyo, waone namna ya kuboresha boresha huko ili kusudi Wizara ya Ardhi isiishie Dodoma tu kuleta huo mfumo wa ILMS (integrate Land Management System), upelekwe nchi nzima ili kusudi Watanzania tupate hati na tulipe kodi na hii ni tax base kubwa.

Mheshimiwa Spika, nasema mathalan, tukipata watu milioni 10 tu wanaweza kukulipa kodi ya ardhi kwa mwaka, sisi bajeti yetu inakwenda ku-double na transaction za ardhi ni nyingi. Kwenye transfer tu kuna 10% ya bei ya kiwanja. Ten percent ya shilingi milioni 60 ni shilingi ngapi jamani? Hela iko huko. Nami sitachoka kusema, nitasema mpaka namaliza Bunge langu, mpaka nione Serikali imesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ardhi ni ardhi-mtaji kwetu Watanzania. Nitaendelea kusema mpaka nione Serikali imenisikia ili tupate fedha tukajenge madaraja, tupate fedha tumalizie miradi mikubwa ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema, nakushukuru sana, sana, sana. Naendelea kupongeza Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi. Sisi Wabunge kazi yetu, naomba tuchukuliwe positive.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante.