Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mwigulu na timu yake kwa bajeti nzuri sana waliyoiwasilisha. Kwa mara ya kwanza, mimi ni kipindi changu cha pili Bungeni hapa. Nimeona Wapinzani wakianza kuisifu Serikali. Hii ni dalili ya kwamba kwa kweli Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anafanya kazi nzuri. Muda mchache tu umemsikia Mheshimiwa Esther Matiko akizitaja Ibara, akitaja vifungu vya Katiba, akitaja Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi kwa vifungu, lakini amesifu mpaka ile tozo ya asilimia sita ya elimu ya juu. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Adam kuna Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu nimpe taarifa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, kwamba kazi ya Mbunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Ndio maana ukiapa haijalishi umetoka chama gani kwa sababu CCM ipo madarakani sasa hivi ina Ilani yao lazima tusome na niwaombe tu hizi Ilani msikae nazo kama mapambo. Kasomeni mfanye rejea muweze kuishauri na kusimamia Serikali vizuri. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakasaka unaipokea hiyo taarifa.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tena naipokea kwa mikono miwili, kwa sababu, narudia kwa mara ya kwanza, Ilani yetu kwanza inasifiwa na upinzani; lakini inasomwa. Kila miradi ambayo tulikuwa tunaipanga na inasomwa hapa. (Makofi)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kiongozi mzoefu wa kipindi cha pili. Upinzani sio uadui ni jicho la pili la Serikali. Kazi ya upinzani sio kukubali mambo yote ambayo Serikali inafanya vinginevyo wote tungekuwa chama kimoja. Kwa hiyo nampa taarifa, wajibu wetu sisi; sisi tunagonga muhuri sehemu ikifanywa vizuri, ikifanya vibaya tutapinga na nchi yetu itasonga mbele. Nampa taarifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakasaka.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado point iko pale pale, sasa hata taarifa zao tunazipokea kwa sababu zina mashiko. Miradi ile ya nyuma ambayo kila mradi ulikuwa ukiletwa Bungeni ilikuwa inapingwa. Naunga mkono hoja. (Makofi)

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ridhiwani una taarifa gani tena? Haya karibu.

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji hoja kwamba, shida iliyotokea hapa ni kwamba kuna mtu kasoma Biblia kuliko Mroma Mwenyewe. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakasaka.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mi taarifa za leo zote nazikubali. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoanza. Kwa kweli sasa hili Bunge tunakwenda vizuri, hata humu ndani sasa kumetulia, zile hoja tulizokuwa tunapingana pingana hazipo, lakini wakati tunasifia, tunamsifia Mheshimiwa Rais pia kwa teuzi mbalimbali.

Nakumbuka Mheshimiwa Mwigulu wakati anasoma bajeti yake alituambia kuhusu kadi ya njano na nyekundu; kwamba mama anazo zote mbili na tumeziona. Moja imetumika juzi juzi tu na kwenye mpira kuna kadi unapewa moja kwa moja nyekundu bila kuonywa, lakini nyingine unaonywa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwenyekiti wa Maadili kama alivyokuwa anasema Mheshimiwa Matiko, ninapoona maadili yanamomonyoka huwa najisikia vibaya na hasa ya viongozi. Kwa sababu sisi moja ya kazi yetu ni kuishauri Serikali kama Bunge na sisi Kamati ya Maadili tupo pia kwa niaba ya Bunge zima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia kwa kuonesha kadi nyekundu kwa Kiongozi mmoja wa Serikali ambaye ametumia ulimi wake vibaya. Moja ya maadili ya kiongozi ni pamoja na kutumia lugha ya staha. Sasa huyu mwenzetu mmoja aliweka comedy akazidisha akatumia lugha ambayo si ya staha, mama alimwonesha kadi nyekundu moja kwa moja. Mimi nampongeza sana na hiyo italeta heshima kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu kwenye eneo ambalo alilizungumza Mheshimiwa Munde, ameongea vizuri sana kuhusu lile suala la land rent. Tunahitaji kodi, kodi lazima ikusanywe na ni kweli kila nchi inaendelea duniani kwa kukusanya kodi. Naomba kuna vipengele kama viwili hebu Mheshimiwa Mwigulu akaviangalie au hata atakapoanza kuhitimisha hoja yake aje atufafanulie kidogo ni kweli kuna mkanganyiko kwenye eneo fulani. Kwa mfano, kuna wazee ambao walipata msamaha wa jumla kwenye kodi. Sasa itakapoingia ile tunalipa kwenye LUKU moja kwa moja wale wazee ule msamaha sijui itakuwaje. Pia na lile eneo ambalo utakuta kwa mfano mtu kwenye kiwanja kimoja ana mita tatu ambazo zote zipo kwenye kiwanja kimoja sasa wakati analipia LUKU ile sijui kama hakutakuwa na contradiction nyingine yoyote, basi hiyo Mheshimiwa Mwigulu atatufafanulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa upande wa TRA. Wananchi wengi wangependa kuwa na kampuni wanapotaka kufanya biashara, lakini mlolongo wa namna ya kufungua kampuni, mimi ni mjasiriamali na-declare interest. Kwa mtu wa kawaida kufungua kampuni kuna shida. Ile milolongo ya kuanzia kujaza fomu huko, ukishamaliza uende kwa Mtendaji, uende kwa Bibi Afya, uende kwa watu wa Chakula wa TFDA, sehemu mbalimbali haina shida. Hata hivyo, kuna eneo moja ambalo kabla hujaanza process yoyote unatakiwa ufanyiwe hesabu na mtaalam wa mahesabu. Sasa wengi unakuta kwamba hawawezi kutoa ile fedha kumpa Mhasibu ambaye unakuta gharama yake ni kubwa labda Sh.600,000 au Sh.700,000 na mtu ndio anataka kufungua kampuni. Naomba aliangalie eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sehemu ya uhakiki. Tulishawahi kuzungumza huku, sehemu ya uhakiki wa madeni ni kichaka kabisa cha kuficha vitu mbalimbali. Maeneo yale kwa mfano, natolea mfano wa mwananchi mmoja wa jimbo langu ambaye anadai toka mwaka 2014/2015 madeni yake mpaka 2020 niliambiwa kwamba ameshahakikiwa. Nikawapigia mpaka Hazina wakasema wamekudanganya, hakuna katika majina hayo, huyo hawajaleta jina lake na huyu alihudumia Ofisi ya RPC na maandishi yao yapo, uhakiki sasa hivi una miaka karibu saba. Wanaendelea kuhakiki kwa hiyo ni kichaka cha watu kuficha haki za watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la sensa, namshukuru Mheshimiwa Mwigulu, amezungumzia suala la sensa. Naomba kwenye suala hili waje kutoa elimu ya kutosha, Tabora limetuponza. Ukiangalia kwa mfano Jimbo la Tabora Mjini alisema hapa Mheshimiwa wa Viti Maalum kuhusu ukubwa wa jimbo lile na idadi ya watu, ni tofauti kabisa. Tabora Mjini ina watu wasiopungua 500,000 inaenda 600,000 huko. Ni jimbo kubwa nilisema hapa wakati nachangia asubuhi, lina kata 29, lakini kutokana na baadhi ya watu kutojitokeza kwenye sensa, ile iliyopita hawakuweza kukidhi mahitaji ya sensa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu, huwezi kupanga maendeleo bila kujua una idadi ya watu kiasi gani. Kwa hiyo, naomba sana waje kutoa elimu ya kutosha, Jimbo la Tabora Mjini ni kubwa na pale itakapofika kugawa majimbo, Tabora Mjini wasije wakaisahau ni kubwa ina kata 29, vijiji 41, ni jimbo ambalo sehemu nyingine ukienda ni masaa mawili kwenye jimbo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la urasimishaji kwa kumalizia. Wako watu ambao waliaminiwa, kampuni mbalimbali kwa ajili ya urasimishaji kwenye ardhi. Wamekusanya fedha za wananchi; wananchi wanasubiri kupimiwa na zile kampuni zimechukua muda mrefu na sehemu nyingi hazijarasimishwa rasmi. Hizi kampuni zinaonekana nyingine za kitapeli. Serikali iangalie kama kuna uwezekano wakizigundua wazifute kabisa ili kampuni zingine ziweze kuchukua hiyo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)