Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa ruhusa yako nami nisiwe mchoyo wa kushukuru, kwa kunichagua katika kuwasilisha mchango wa bajeti yetu ya Serikali, ambao ni mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia kwanza napenda kumpongeza pamoja na timu yake, Waziri wa Fedha na Mipango, kwa hotuba yake nzuri na mtiririko wake mzuri katika kuwasilisha katika hadhira yetu hii ya Bunge. Pia, nampongeza Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kutufikisha hapa tulipo na kwa kuweza kuweka maelekezo yake mazuri sana kama ambavyo katika bajeti zetu hizi tunavyokwenda nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchangiaji wangu, nitajaribu kugusa mambo matatu. Cha mwanzo, nitajaribu kuangalia suala la uchumi wa nchi yetu. Unajua kukua kwa uchumi maana yake wakati mwingine watu wanajaribu kutafuta, ile tafsiri ya uchumi. Kwa nini uchumi unaambiwa kwamba umekua kwa asilimia nne au asilimia ngapi. Mwananchi wa chini mara nyingi huwa hawezi kujua uchumi namna unavyokua, lakini kwa namna ambavyo maendeleo ya nchi yetu yanavyopiga hatua, hasa katika masuala ya ujenzi wa miundombinu yetu, maana yake ile ni dhahiri kwamba uchumi wa nchi yetu unakua. Kigezo cha mwanzo ni kuona ile miradi mikubwa iko katika hali ya uendelevu, kwamba, tangu ilivyoanza miradi hiyo maana yake iko katika hali ya uendelevu. Sasa uendelevu ule maana yake ni kigezo dhahiri kwamba nchi yetu ya Tanzania inakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tukizungumzia suala la bajeti, bajeti yetu hii tutasema kwamba ni ya ushirikishwaji wa watu kulipa kodi bila ya hiari. Kwa nini nazungumza kwamba ni bajeti ya shirikishi ya watu kulipa kodi bila ya hiari, kutokana na kwamba kwa namna ya zile kodi zilivyowekwa. Wabunge wengi wanajaribu ku-question suala la kodi ya nyumba kwamba, labda pengine litampa mzigo mwenye nyumba au mpangaji katika nyumba. Suala lile kiukweli na kiundani kabisa maana yake ile ni dhahiri kwamba, tunashirikisha ile jamii iliyokuwepo katika makazi yetu katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusijaribu kulaumu au kujaribu kulalamika kwa Sh.1,000/= ambayo inalipwa kwa kila mwezi kwamba, ikawa ni suala ambalo ni kubwa sana kwa kushirikishwa wananchi wetu kulipa katika tozo ya nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nasema kwamba bajeti yetu ni uendelezaji wa kazi za Awamu ya Tano ambayo imeziacha. Nasema kwa mujibu wa bajeti ambayo iliyokuwepo, ni dhahiri kwamba mfumo wa bajeti uliokuwepo, haya mambo yote ambayo yameachwa, kwa upande wa Serikali ya Awamu ya Tano, maana yake ni dhahiri kwamba kodi inalenga hasa kumalizia yale yote ambayo yameachwa. Kwa imani yetu, tuna uhakika kwa uongozi tuliokuwa nao kwamba, yale yote ambayo yameachwa na Hayati Dkt. Pombe Magufuli, mambo yale yote yataweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina wasiwasi kwa mujibu wa timu tuliyokuwa nayo na kwa uongozi wetu wa mama na kwa namna ambavyo, yeye mwenyewe binafsi anavyofanya kazi katika kuishirikisha jamii. Kaanza kuishirikisha jamii ya wanawake, akaweza kuwaeleza namna ya uchumi wa nchi tunaokusudia kwenda nao. Tangu juzi tunamwona Rais wetu akiwa kule Mwanza, nako vile vile akishajihisha masuala haya haya ya ulipaji kodi. Ni dhahiri anaweka ile picha ya namna ya mfumo wa Serikali ya Awamu ya Sita namna ilivyo, leo tumemuona akiwashirikisha vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akawaeleza vizuri sana kuhusu kuwaundia Mabaraza yao ya Vijana kwamba, huku upande wa Tanzania Bara hakuna Baraza la Vijana, lakini kutokana na hotuba yake ile, nasema kwamba vijana wamepata moyo mkubwa sana. Kutokana na maneno yake ni dhahiri kwamba vijana wamepata mwamko na hasa katika masuala ya hii bajeti yetu, vijana wataleta mchango mkubwa sana na wanaweza kusababisha kuleta maendeleo makubwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija suala la bajeti iliyoletwa, maana yake imekidhi mapendekezo yote yaliyokuwa yamependekezwa na Wabunge katika Bunge letu hili. Wabunge wengi walikuwa na vilio vingi kabisa, walikuwa wanalia kuhusiana na suala la TARURA na mambo mengi ambayo walikuwa wanaeleza au wanatoa vilio vyao yameweza kupatiwa muarobaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nasema kwamba mama kaja, kwa ajili ya kutatua muarobaini kama lilivyo jina lake Mama Samia Suluhu kweli kaja kuleta suluhu ya uchumi wa nchi yetu. Kwa muktadha huo maana yake kitu cha mwanzo kabla ya bajeti, mama alianza kutatua tatizo la TARURA, akazungumza suala la Mfuko wa kila Jimbo kuwapatia shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuzungumza suala hili, nadhani kwamba, nijaribu kumuuliza Waziri tu kwamba huu Mfuko ambao tayari mama kausema, kuhusiana na shilingi milioni 500 kwenye majimbo. Huu Mfuko, je, sisi wa upande wa Zanzibar unatuhusu? Najaribu kuuliza hivyo kwa sababu, kuna Mfuko ule wa Jimbo ambao unatuhusu sote, lakini sasa je, hizi shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo kwa sababu zimezungumzwa kwa kila Jimbo, sasa je, kwa upande wa kule Tanzania Visiwani au Tanzania Zanzibar, je, watapata kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nitazungumzia suala la VAT. Pia katika hili nalo nashukuru kwamba, Waziri kajaribu kuzungumiza suala vizuri sana kuhusuana na VAT kwamba, upande wa Zanzibar na kwa upande wa Tanzania Bara. Alisema kwamba, kutakuwa na ule unafuu wa kusameheana, kwamba kutakuwa hakuna ulipaji; bidhaa itakayolipiwa Zanzibar ikija Bara maana yake haitotozwa VAT. Hata hivyo, tatizo bado linabaki kwa upande wa bidhaa nyingine, hasa kwa upande wa zile bidhaa ambazo ni kubwa, kwa mfano, kama magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali zote mbili zikae pamoja, maana yake wawe na ushuru wa aina moja, kuliko kwamba kuna bidhaa ambayo inatozwa Zanzibar, ikija huku unaambiwa kwamba ulipe different. Serikali yetu ni moja, Tanzania yetu ni moja, Watanzania ni wamoja. Kwa hivyo, tusijaribu kujenga kitu ambacho kitaleta hitilafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuhusiana kwa upande wa VAT, kuna suala la vitu ambavyo ni tangible na vitu ambavyo ni intangible. Tangible havina tatizo kwa sababu vinajulikana kwamba kama ni bidhaa zenye kushikika, lakini kuna bidhaa ambazo ni intangible, kama suala la mawasiliano, hili suala hili sijui tutalifanyaje katika ugawanaji wa mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kuna Mbunge wetu mmoja, aliwahi kulizungumza suala hili kwamba, Zanzibar wana asilimia 18 kwa upande wa Tanzania Bara kuna asilimia 15. Je, katika utozwaji huu ile different maana yake itakuwaje? Nadhani kwamba viongozi wote wawili kwa upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara, wangekaa pamoja kujaribu kulijadili suala hilo. Suala hili pia lipo hata kwa upande wa miamala na nadhani kwamba nalo litaweza likaja likaleta hitilafu hiyo. Kwa hivyo, nashauri Waziri suala hilo aweze kuliangalia vizuri, ili lisije kuleta hitilafu yoyote kwa pande zetu zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitazungumzia suala la upande wa kilimo. Tanzania ili kuweza kukua kwa uchumi ni vizuri zaidi tukajaribu kuangalia sekta ya uchumi katika hali bora kabisa. Kilimo chetu hiki nadhani kinaweza kikakua na Serikali ina nia kabisa kabisa na ndiyo maana ikaweza kupeleka hizi fedha, kwa ajili ya kutengeneza njia au barabara vijijini kwa ajili ya kurahisisha watu kuweza kusafirisha mazao yao kwa njia ya urahisi. Hata hivyo, ni vizuri zaidi kwa upande wa kilimo tukajaribu kuangalia na miundombinu. Je, miundombinu ambayo iliyokuwepo katika sekta ya kilimo, inaweza kukidhi haja ya uchumi wetu wa Tanzania kuweza kukua? Maana yake hilo lote tujaribu kuliangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napongeza sana bajeti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia, kwa jitihada yake kubwa anayoifanya na kwa mwelekeo wote ambao anauonyesha. Kwa namna ambavyo nchi yetu ya Tanzania kama ulivyokuwa msemo wa Rais wetu wa Zanzibar kule “yajayo yanafurahisha” kwa maana hiyo tutegemee kwamba Tanzania “yajayo yatakuwa yanafurahisha”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja ya bajeti yetu hii. (Makofi)