Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mgeni Jadi Kadika

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mwenye kunipa nguvu na afya njema nikaweza kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Maalim Seif Shariff Hamad kwa hekima yake na busara zake kuweza kuwatuliza Wazanzibari kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu. Kama si hekima zake basi sasa hivi tungekuwa tayari wengi wamekufa na wengi wamepata vilema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, sasa nakuja kwenye hoja. Mimi naanzia kuchangia hoja kwenye suala la UKIMWI. UKIMWI ni janga la Taifa na unapoteza nguvu kazi za vijana wetu katika Taifa hili. Pamoja na utafiti wa Serikali kusema kuwa UKIMWI umeshuka kuanzia asilimia 8.8 mpaka kufikia asilimia 5.1 lakini bado UKIMWI unaongoza. Utafiti unaonyesha mikoa mitano ya Tanzania ndiyo inaongoza kwa UKIMWI ambayo ni Mbeya, Iringa, Shinyanga, Dar es Salaam pamoja na Njombe. Mimi nataka kuzungumzia Mkoa wa Shinyanga kwa sababu ndiyo tulioutembelea na tukaona hali halisi ya wagojwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu wanasema, kuanzia Januari mpaka kufikia Disemba wagonjwa waliofika kwenye kituo cha afya na kupimwa wakaonekana ni waathirika katika Mkoa wa Shinyanga walikuwa ni wagonjwa 34,826, maambukizi mapya yalikuwa 953, hii ni asilimia kubwa. Nakuja kwa wajawazito, wajawazito waliofika kupimwa kati ya mwezi wa Januari mpaka Disemba walikuwa 81,509 na waliogundulika wameathirika ni wanawake 2,737, ni asilimia 3.4. Hii inaonyesha ni maambukizi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri alizungumzia kuwa ataongeza vituo na dawa lakini hakuzungumzia chakula. Wagonjwa hawa wa UKIMWI wanapokula dawa za ARV basi ni lazima wapatiwe chakula kwa sababu dawa zina nguvu na wanazidi kuathirika. Kwa hiyo, naomba Serikali itenge fungu maalum la kuwasaidia hawa waathirika walio katika mikoa hii iliyoambukizwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwa wakunga jadi. Wakunga wa jadi ni watu ambao wanatoa msaada mkubwa katika kuwasaidia akina mama wajawazito vijijini. Naiomba Serikali wawape mafunzo hawa waliokuwa hawajapata na waliopata mafunzo waajiriwe, Halmashauri ziwatazame, ziwape angalau posho za kupata sabuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya na zahanati ziboreshwe kwa sababu miundombinu yake ni mibovu. Hakuna maji, umeme na vitendea kazi na isitoshe vituo vya afya vinajengwa mbali na wananchi. Kwa hiyo, ni shida, mzazi akipakiwa kwenye baiskeli mpaka akifika kwenye kituo cha afya basi huyo hali yake ni taabani, hana nguvu za kusukuma mtoto inampelekea kufariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali ifanye juhudi za makusudi ili kuwapatia wanawake hawa gari angalau kila kata au kila kituo kipatiwe ambulance. Wenzangu wengi wamesema na mimi naomba hilo ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Mheshimiwa Spika, sasa nazungumzia watoto wa mitaani. Watoto wa mitaani ni wetu lakini inakuwa ni kero. Watoto hawa ni kweli maisha ni magumu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)