Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DANIEL N. NSANZUGWAKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja ya Mapendekezo ya Mpango, nikisoma pamoja na mwongozo wake wa kuandaa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema katika Bunge hili kwamba katika utamaduni wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola, Muswada kuwasilishwa mezani au na Waziri wa Serikali au na Mbunge na Muswada huu au hoja hii ikatolewa ni jambo la kawaida sana, ni jambo ambalo ni la kawaida kabisa na wala hakuna kitu ambacho ni cha ajabu. Nataka tuweke rekodi hizo kwa sababu yaliyotokea katika siku mbili ilionekana kama ni kitu kikubwa, lakini kumbe ni jambo la kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitajikita katika mambo makubwa matatu, nitajielekeza katika miradi ya Kitaifa ya kimkakati. Bila shaka huwezi kuzungumzia kukuza uchumi kama huwezi ukazungumzia miradi ya kimkakati. Miradi ya kimkakati tafsiri yake ni kwamba ni miradi ambayo ikitekelezwa itausukuma uchumi ule uweze kuzalisha mambo mengi zaidi na uweze kuzalisha fedha ziweze kutekeleza mambo mengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika miradi ya kimkakati, kabla sijaendelea na jambo hilo naomba ukurasa wa tisa wa Mpango, tufanye marekebisho kidogo. Katika yale maeneo yanayolima kahawa, nimeona yametajwa pale katika ukurasa wa tisa, wamesema katika Wilaya za Moshi, Mbinga, Bukoba, Mbozi na Tarime, kana kwamba ndiyo zinalima kahawa peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuweke rekodi sawasawa, kwa takwimu za Tanzania Coffee Board, Mkoa ambao unatoa kahawa ya arabika bora katika nchi za Afrika Mashariki ni pamoja na Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, naomba katika mpango ule katika ile miche ya kahawa, ijumuishe pia Wilaya ya Kigoma na Wilaya ya Kasulu ambako tunalima arabika ya kiwango cha juu kabisa na zaidi ya hapo hata TaCRI wana kitalu kikubwa sana cha kuzalisha miche zaidi ya 1,000,000 pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya kimkakati, niungane na wasemaji waliopita kuzungumzia suala la reli ya kati. Naona kuna confusion kidogo hapa, hivi tukisema reli ya kati maana yake nini? Reli ya kati maana yake ni kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora, Kigoma na unakuja branch ya Tabora kwenda Mwanza ndiyo reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha wa Mpango huu, reli ya kati ni pamoja na mchepuko kutoka Isaka pale Kahama kwenda Keza, Keza iko kwenye mpaka wetu na Rwanda na pia mchepuko wa kutoka Uvinza kwenda Msongati ya Burundi na pia mchepuko wa Kaliua, Mpanda kwenda Kalema bandarini na mchepuko wa Dodoma kwenda Singida, hiyo ndiyo reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka tuwe na uchumi wa viwanda, kama kweli tunataka nchi yetu ibadilike ingie katika uchumi wa kati, lazima tujenge reli. Sasa shida inakuwa pesa tunapata wapi, gharama ni kubwa kwa awamu kwanza tunahitaji takriba dola bilioni 7.6. Hii siyo fedha nyingi, nchi hii ni kubwa, tunakwenda kukopa, tuna marafiki wetu wa maendeleo, kuna Wachina na Wajapani wanatuamini na sisi tunawaamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwamba hatuna fedha za kujenga reli, hatutaki kuisikia katika Bunge hili. Tunataka Serikali ije na mkakati mahsusi, mkakati wa msingi kabisa wa kwenda kukopa fedha hizi kwa Serikali ya Watu wa China, kwa Serikali ya Wajapani tujenge reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, bila ya kuwa na reli, tunacheza ngoma. Haiwezekani mizigo yote, makontena yote, mafuta yote yapite kwenye barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, ni nchi yetu pekee ambayo mizigo mizito inapita kwenye barabara. Matokeo yake barabara hizi zinaharibika sana, inajengwa barabara ya kukaa miaka 30, uhai wake unakuwa ni miaka mitatu, minne, barabara inakuwa imeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tukubaliane, Waziri wa Fedha usipokuja na mkakati wa kujenga reli ya kati ikiwa na michepuko niliyoitaja, Isaka, Keza kwenda kubeba mzigo wa nickel, Uvinza - Msongati kwenda kwa ndugu zetu wa Burundi kuchukua mzigo wa Congo; mchepuko wa Kaliua, Mpanda - Kalema kwenda bandari ya Momba katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kuchukua mzigo wa Lumbumbashi.
Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, utakapokuja na Mpango huo bila hiyo reli ya kati hatuwezi kuelewana katika Bunge na nitaomba Waheshimiwa Wabunge tusimame kidete kumwambia arejeshe Mpango huo mpaka atuwekee reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani miaka zaidi ya ishirini tunazungumza reli ya kati, lakini haijengwi, haiwezekani? Wenzetu Kenya wameanza kujenga Mombasa kwenda Kigali, kwa nini sisi hatujengi, kwa nini hatuanzi, utasikia tumekarabati kilomita 176 za latiri 80, hatutaki kusikia lugha hiyo na nchi yetu si maskini, ina rasilimali za kutosha, tunaweza tukazikopea kujenga reli ya kati na michepuko niliyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati maana yake hizo reli zinakwenda kwenye mali, ukichepuka Isaka kwenda Keza, unakwenda kwenye nickel nyingi sana, tani milioni kwa mamilioni. Bandari ya Uvinza kwenda Msongati hiyo inapita Kasulu hiyo, Shunga - Kasulu, kwenda Burundi - Msongati maana yake ni madini ya nickel yaliyopo Burundi na mzigo ulioko Congo ya Mashariki. Isitoshe bila kujenga reli ya kati kwa standard gauge, tutaua bandari ya Dar es Salaam, bandari ya Dar es Salaam kwa miaka michache ijayo itakuwa haina mzigo, tutaua bandari ya Mwanza, tutaua bandari ya Kigoma na tutaua bandari ya Kalema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, Waziri wa Fedha, bila kuja na mkakati mahususi wa reli hii, kwa tafsiri hiyo, tutashawishiana Wabunge wote tukuombe urudi tena mpaka uje na hoja mahususi ya kujenga reli ya kati. Bila reli ya kati hakuna uchumi wa viwanda, bila reli ya kati hakuna nchi kwenda kwenye pato la kati, kwa nini tuendelee kujiharibia wenyewe, wakati tunaweza tukatenda haya na yakafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie ni maeneo wezeshi kwa maendeleo ya viwanda. Soma kwenye Mpango hapa, tumezungumzia juu ya nishati, reli na barabara. Nimefurahi kusikia kwamba washirika wetu wa Maendeleo wametupatia fedha kwa ajili ya kujenga gridi ya Taifa kutoka Geita sasa kuja Nyakanazi, Kwilingi na Kakonko, Mkoa wa Kigoma. Ningefikiri kupitia kwa Washirika wetu wa Maendeleo hao hao, tungeendeleza hiyo grid sasa, ile western grid, ile corridor kutoka Kakonko iende Kibondo, Kasulu, Kigoma na Katavi. Hatimaye iweze kuja ku-link na Tabora, tuweze kuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya maendeleo ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi sana na la kisera na liko kwenye Ilani yetu ni barabara ya Kigoma – Kidahwe - Nyakanazi. Hii barabara ni barabara ya kihistoria, imesemwa kwa miaka zaidi ya 20 sasa na bahati nzuri mkandarasi yuko site pale. Yule mkandarasi nimepata habari, alikuwa ananiambia Waziri wa Uchukuzi hapa kwamba wamempa fedha kidogo ili aendelee. Sasa tunaomba barabara hiyo ni barabara ya kimkakati kwa sababu inatuunganisha na mikoa mitano ya nchi hii; inatuunganisha Kigoma - Kagera, Kigoma - Mwanza, Kigoma - Geita, na Kigoma - Shinyanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo barabara ni muhimu sana. Tunamwomba Waziri wa Fedha, aje na mkakati sasa wa kuimalizia barabara hiyo. Na huyo mkandarasi ambaye yuko site, basi tunamwomba aendelee ili barabara hiyo ikamilike. Si hiyo tu, sisi tunaotoka Kigoma, hiyo barabara ndiyo siasa za Kigoma na tunasema barabara ya Nyakanazi kipindi hiki, ndio wakati wake na niseme tu kwamba tutaomba sana barabara hii ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)