Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nianze kwa kusema kwamba binafsi sina mashaka na uwezo, dhamira na nia ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii. Ukimtazama usoni unaona kabisa huruma aliyonayo kwa Watanzania, kwa hiyo, sina mashaka kwamba anaweza kuitendea haki huko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo mtunzi mmoja wa vitabu maarufu sana, anaitwa Mudhihir Mohamed Mudhihir, aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo ninaloliongoza mimi sasa, ametunga kitabu kinaitwa Mwele Bin Taaban. Dibaji ya kitabu hiki imeandikwa na Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe. Maudhui yaliyopo ndani ya kitabu hiki ya Mwele Bin Taaban naona kama yanafanana na uhalisia uliopo katika nchi yetu hususan namna bajeti ya Wizara ya Afya mwaka huu ilivyopangiwa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 9 ya Katiba yetu (i), kinasema kwamba utajiri na rasilimali za nchi hii zitawekezwa kwenye kuhakikisha kwamba zinaondoa matatizo ya umaskini, maradhi na ujinga. Maradhi yanagusa Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa takwimu zinaonyesha kila mwaka Watanzania tunaongezeka kwa idadi ya watu 1,000,000, Wizara ya Afya badala ya kuongezewa pesa yenyewe ndiyo inapunguziwa. Mwaka huu imepunguziwa shilingi bilioni 18 kutoka kwenye bajeti ya mwaka jana wakati wale watu 1,000,000 wameendelea kuongezeka, matatizo ya afya yameendelea kuongezeka, uwezo wa kuyatatua kwa fedha hizi naamini hakuna. Dada yangu hapa ameongea vizuri na nilikuwa namtazama usoni nikiona kabisa dhamira yake, lakini fedha huna dada! Kwa bajeti hii inaashiria kabisa kwamba you are going to fail, business itakuwa vilevile, business as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano Hospitali ya Rufaa ya Mtwara ya Ligula, mwaka jana mlitenga shilingi bilioni mbili, mwaka huu tena mmetenga shilingi bilioni mbili, nikuulize shilingi bilioni mbili za mwaka jana umepeleka shilingi ngapi, aibu! Mwaka huu tena mmetenga shilingi bilioni 2, najua ni ku-copy na ku-paste tu, pesa hizi haziendi. Kama mwaka jana mlitenga na hamkupeleka, mwaka huu hiyohiyo tu, hamtapeleka fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mkoa ya Sokoine - Lindi, aibu! Hospitali ile haina chumba wala sehemu ya watu waliowasindikiza wagonjwa kuweza kupumzika. Kwa hiyo, kuna mtu anapeleka mgonjwa wake akifika pale akikaa yeye mwenyewe kesho anageuka kuwa mgonjwa kwa sababu ataugua malaria, atang‟atwa na mbu usiku kwa hiyo badala ya kusindikiza mgonjwa na mwenyewe anakuwa mgojwa, otherwise asimame usiku mzima. Hakuna sehemu ya kupumzika watu wanaopeleka wagonjwa Hospitali ya Mkoa ya Sokoine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la Kituo cha Afya Kitomanga kilichopo kwenye Jimbo la Mchinga. Ndiyo maana nasema this government is it serious? Pale Kitomanga kuna kituo cha afya, kwenye Jimbo langu la Mchinga, mmepeleka vifaa tiba kama X-ray, mashine za CT-Scan, mmepeleka vifaa vingi na kile kituo cha afya lengo lake ilikuwa mkifanye Hospitali ya Wilaya, huu ni mwaka wa nne, vifaa vile vinaharibika, vinaliwa na panya, ni aibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa tatu mwaka huu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya alitembelea pale badala ya kutoa majibu kwamba ni lini kituo hiki kitapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya amekwenda kufanya issue kuwa too much complicated watu wamekata tamaa. Ameongea na wananchi pale anawaambia kwa namna taratibu na sheria zilivyo, kituo hiki kuja kuwa hospitali itatuchukua muda mrefu, vifaa vile mlipeleka ili iweje? Pia katika maeneo yale watu hawana hospitali ya karibu kwa hiyo wanaendelea kuteseka. Namuomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha hoja yake hapa aje anipe majibu ni lini mtakipandisha Kituo cha Afya Kitomanga kuwa Hospitali ya Wilaya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la wazee. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri anasema kwamba Serikali ina mpango wa kuleta Bill of Right hapa ili Sheria ya Wazee iweze kupitishwa. Sera ya Wazee imepitishwa mwaka 2003 mpaka leo haina sheria. Kinachokuja kutokea Maafisa wa Maendeleo wa Jamii kwenye Wilaya huko kazi wanayoijua wao ni ku-deal na wanawake na vijana tu kundi la wazee limesahaulika, hii ndiyo reality.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata haya mambo yanayozungumzwa kwamba kutakuwa na fedha shilingi milioni 50 za Magufuli za kila kijiji, Maafisa wa Maendeleo ya Jamii wanahamasisha vijana, wanahamasisha wanawake waanzishe vikundi vya ujasiriamali wawapatie fedha, wazee wanaachwa. Ni kwa sababu hawana sheria, kungekuwa na sheria haya yasingetokea. Ukiangalia sera ya wazee ni sera nzuri, yenye lengo zuri la kuwatetea wazee, unfortunately kwa sababu hakuna sheria basi ndiyo hivyo mambo yanakwenda tu, business as usual, wazee wetu wanataabika. Lililo baya sisi wote ni wazee watarajiwa ikiwa tutafika, kwa hiyo, lazima tuhakikishe tunatengeneza mazingira na sisi miaka 20 mbele ikija tukiwa wazee mambo haya yawe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo suala la Mfuko wa CHF (Mfuko wa Afya ya Jamii). Mimi jimboni kwangu ndani ya Halmashauri yetu na Mheshimiwa Nape tuko Halmashauri moja, sisi tumekubaliana kwamba tutahamasisha wananchi wetu wote wajiunge na mkakati ilikuwa wakati huu wa msimu wa ufuta wananchi wote wakate kadi za Mfuko wa Afya ya Jamii. Unfortunately tumesitisha na nimewaambia wananchi wangu wasijiunge kwa sababu wanaibiwa bure tu. Mtu anakata kadi kwenye zahanati ya Kilolambwani akienda Mvuleni, kilometa tatu tu anaambiwa hutambuliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia dawa, Halmashauri wanatumia fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii kwenye matumizi yao. Kwa hiyo, mtu amekata kadi anakwenda hospitali hana dawa. Wanasema Mheshimiwa sasa hii haja ya kukata kadi inatokea wapi, bora twende tulipe shilingi 5,000. Kwa hiyo, kama kuna hoja ambayo Mheshimiwa Waziri anatakiwa ai-address ni hii issue ya Mfuko wa Afya ya Jamii. Wananchi wameitikia sana, mimi nimewasimamisha jimboni kwangu nimewaambia never, mpaka mimi niseme, msijiunge kwa sababu mnaibiwa na mnaibiwa kwa sababu mtu anakata hapa, kilometa tatu anaambiwa hutambuliki lakini pia dawa hakuna, kwa hiyo, anafanana na mtu ambaye hana kadi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala moja kwa haraka haraka sana linalohusu pia mambo ya wazee. Sera ya Wazee inasema wazi kwamba wazee na watoto watatibiwa bure, lakini kwa masikitiko makubwa sana, mwezi wa 12 nilipoteza wazee zaidi ya watatu kutoka Jimboni kwangu pale Sokoine. Wazee wale walifariki kwa sababu tu ya kukosa matibabu ya operesheni ya mshipa ngiri eti hawana fedha. Iliniuma sana na inaendelea kuniuma, kama sera inaweka wazi kwamba wazee wanatibiwa bure kwa nini mzee anakwenda hospitali hapati matibabu kwa kigezo tu kwamba hana fedha? Tuwe na huruma na wazee wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.