Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya mwaka 2021/2022, bajeti ambayo ina mpango wa namna gani tunakwenda kukusanya mapato na matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni ya kwanza katika Mpango wa Miaka Mitano tuliyojiwekea, ni bajeti ya kwanza ya Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Awamu ya Sita yenye maelekezo mengi, yenye matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii inakwenda kujibu kero na vilio vya Watanzania wa aina mbalimbali. Kwa mfano inakwenda kuweka matumaini makubwa kwa watumishi kwa sababu tunaona kuna mpango wa kuwapandisha vyeo watumishi wapato 92,619 pamoja na kwenda kupunguza makali ya Maisha kwa sababu inakwenda kupunguza kodi kutoka asilimia tisa mpaka asilimia nane. Tunamshukuru sana mama, hongera sana. Pia itajenga mazingira mazuri kwa watendaji wa vijiji na makatibu tarafa kwa jinsi ambavyo itawarahisishia kazi zao, kwamba sasa wanakwenda kuwekewa laki moja ili iweze kuwarahisisha katika utendaji wao wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuwapa nguvu na confidence viongozi wetu wa siasa, Madiwani kwa kuwa sasa wanaweza wakasimamia miradi ya halmashauri bila kubabaishwa, bila ya kuwanyenyekea wakurugenzi wala wataalam. Wataweza kusimamia miradi ya Wakurugenzi kwa kuwawekea posho zao moja kwa moja kwenye akaunti inayotoka Hazina, hongera sana Mama. Lakini pia inampango mzima wa kuweza kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji waje wawekeze. Pia utaratibu mzuri kwa wafanya biashara kuweze kulipa kodi kwa hiyari yao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa Watanzania walio wengi matumaini ni makubwa kwa sababu bajeti hii imewaonesha jinsi ya kwenda kuboresha huduma za jamii. Kwa mfano itaendelea kutoa elimu bure kuanzia form one mpaka form four. Tunaipongeza sana, lakini mpango mzima wa kwenda kukamilisha vijiji ambavyo havijapata umeme katika mpango huu vijiji vyote Tanzania vinakwenda kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme ni kichocheo cha maendeleo, nimpango mzuri sana. Tunajua umeme umepunguzwa Rural-Urban Immigration ambapo vijana walikuwa hawapenda kukaa vijiji. kwamba ni afadhali akae Machinga Mjini kutokana na kukosa umeme, kwamba anaona ametengwa na dunia anashindwa kuingia internet. Lakini vile vile imeweza kuchochea viwanda vidogo vidogo kama saluni huko vijijini, viwanda vya ma-grill pamoja na pia kuwasaidia kina mama ambao walikuwa wanakwenda mbali kwa ajili ya kwenda kusaga mahidi wakifuata umeme mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile kuna mpango mzima wa kuboresha barabara, hasa hizi za TARURA pamoja na feeder roads; ni kichocheo kizuri sana miundombinu ya barabara. Hata hizi pembejeo tunazo sema zinafika kijijini kwa bei kubwa sana kutokana na miundombinu ya barabara ambapo ni mbovu. Kwa mfano Serikali inatoa bei elekezi kwa ajili ya mbolea, lakini mbolea mpaka ifike kijijini bei yake imekuwa mara dufu kutokana na matatizo ya barabara. kwa hiyo kuna umuhimu sana wa kuimarisha barabara, feeder roads pamoja barabara hizi za TARURA. naompongeza sana Mama yetu kwa kutoa top up licha ya bajeti ya TARURA lakini sasa imeongezwa milioni 500 kwa ajili ya kwenda kuboresha barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, ili kuweza kufikia ndoto hii sasa ya kutoa huduma bora kwa Watanzania pamoja na makundi mengine ni lazima sasa tuweke mkakati wa kupata mapato; kwa sababu bajeti yetu ni cash budget we expenditure kila ambacho tunaki-collect.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaompongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango kwa jinsi ambavyo amekuja na vyanzo mbalimbali vya kukusanya mapato. Kuna vyanzo vya zamani vinaendelea lakini pia nimeona vyanzo vipya. Vyanzo vingine kama jinsi utakapopata property tax, kodi ya majengo watu wamechangia najua ni msikivu atakwenda kuboresha kwa namna gani anakwenda kukusanya mapato hayo ambayo hayana kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ameweka vipaumbele, kwamba namna hii ya kwenda kukusanya mapato kipaumbele cha kwanza ni mapato yetu ya ndani na yanayotokana na kodi, tozo na ushuru, na sehemu nyingine ni mkopo wenye masharti nafuu na misaada. Sasa, kama kipaumbele cha kuendesha miradi yetu ni mapato ya ndani kwa hiyo sisi hatuna budi kuwekeza katika sekta hizi za kiuchumi, ikiwepo kilimo, mifugo, maliasili na madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naipongeza sana Serikali kwa sababu hata bajeti, kwa mfano nikichukulia mfano wa kilimo; tumeongeza bajeti ya kilimo kwa asilimia 22 lakini bado bajeti hii inaonekana haitoshi kwa sababu ukiangalia kwenye gross budget, bajeti yote ya Nchi nzima bado kilimo inakwenda kwenye asilimia 0.8 kwamba iko chini ya asilimia moja. Tunavyoweza kuboresha kilimo; kwa sababu tatizo kubwa kwenye kilimo ni uzalishaji mdogo. Kwa mfano tungeweza kuboresha uzalishaji katika kilimo, faida moja wapo tunayopata ni uhakika wa chakula. Tunapokuwa na uhakika wa chakula basi tunakwenda kumudu inflation, na vile vile tunakwenda kufanya serving, kwamba sasa vyakula ambavyo tulikuwa tunategemea kuagiza kutoka nje ikiwemo mafuta, watu wengi wamechangia, ngano na sukari. Tunatumia hizi fedha kupeleka kwenye miradi ya vitu vingine; kwa hiyo ni faida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunajua kwamba kilimo kinatoa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. Kwenye viwanda tutapata ajira, tutakusanya kodi, tutakwenda kuongeza mnyororo wa thamani na hivyo tutapata fedha. Kwa hiyo hatuna budi kuwekeza katika sekta hizo ikiwemo kilimo pamoja na sekta nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mazao ya kilimo yanakuwa hayajafikia malengo kwa sababu, kwanza kuna upungufu mkubwa wa huduma za ugani. Tumeona kwamba sera ya nchi ilikuwa kila ni kijiji kupata Afisa Ugani mmoja wa kilimo na mmoja wa mifugo. Lakini tukiangalia kuna upungufu mkubwa sana kwa maafisa kilimo, tuna maafisa kilimo takriban 6,700 ilhali wanaotakiwa ni 21,288. Hii inaonesha kwamba ratio ya Afisa Kilimo mmoja ni kuwahudua wakulima 600. Hatuwezi kufanya maajabu au mapinduzi makubwa kwenye kilimo kama tupo hivi.

Mheshimiwa Naibu Waziri, japo naipongeza sana Wizara kwa sababu pia imetenga fedha kwa ajili kuboresha huduma ya ugani, imeweke bilioni 11.5 kwa ajili ya kununua pikipiki 1,500 kwa ajili pia ya kuwapa maafisa kilimo extension kit pamoja na soil test kit lakini bado hizi 1,500 hata si robo bado vitendea kazi vinatakiwa kwa maafisa ugani. Mimi nilikuwa naomba kama kuna uwezekano kitengo hiki kiongezewe bajeti kutoka kokote itakavyopatikana ili Watanzania walio wengi ambao ni wakulima waweze kufikiwa na huduma za ugani. Lakini vile vile Maafisa Ugani waajiriwe. Kuna halmashauri nyingine hali yao ni mbaya sana kwa ajili ya upungufu wa huduma hizi za ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na tatizo la pembejeo, mimi naisifu sana Serikali kwa sababu imeongeza bajeti ya kituo cha utafiti ili waje na mbegu bora ambazo zitakuja kuzalishwa na ASA, hata ASA imeongezewa bajeti. Bajeti ya utafiti imeongezwa kutoka bilioni 7.5 hadi bilioni 9.9. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Utafiti vina kazi nyingi tunahItaji utafiti kwenye kilimo. Kwa mfano licha ya mbegu pia wanatakiwa kutufanyia utafiti wa agroecological zone, tujue ni mazao yapi yanatakiwa kuzalishwa wapi, tunatakiwa kufahamu hali ya rutuba ya udongo. Wakati mwingine tunamshauri mkulima apande na dup, nani anayefahamu kwamba pale kulikuwa shida ya phosphorus, ndio maana mkulima anaingia gharama kubwa, anatumia hiyo dup lakini at the end of the day bado matokeo ni madogo. Kwa hiyo tunahitaji utafiti tusibahatishe hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo imeongeza maradufu bajeti ya Wakala wa Kuzalisha Mbegu (ASA), kutoka bilioni 5.4 hadi bilioni 10.5. Tunaiomba ASA sasa isimamiwe, izalishe ile mbegu inayohitajika. Kuna mbegu kwa mfano za alizeti, mkulima atahangaika atavuna alizeti, lakini gunia zima la alizeti akienda kukamua anaenda kupata lita ishirini, ndoo moja. Kwa hiyo tunahitaji wazalishe mbegu chotara ambazo kweli zinakwenda kukidhi. Mtu anavyotoa jasho kwamba anaenda kufanya kile kilicho bora, pamoja na mbegu ya ngano nashairi, mbegu ya mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu Watanzania wengi kwa mfano Kanda ya Kusini kule wanatumia mbegu za mahindi za Zambia, ambazo ni za Kampuni za SEEDCO na Mosanto pamoja na watu wa Kanda ya Kaskazini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshalia Mheshimiwa.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga hoja mkono. (Makofi)