Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii. Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2021/2022 ambayo iliwasilishwa hap ana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kutujalia uzima na kuweza kukutana hapa. Lakini pili nichukue nafasi hii kwa dhati ya moyo wangu kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Jemadari wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiongoza nchi vizuri kwa muda huu ambao tukonae na kwa namna ambavyo amekuwa akisikiliza maoni ya Wabunge. Miongoni mwa sifa inayompamba kiongozi yeyote ni kusikiliza watu wake; Mama yetu anatusikiliza na anawasikiliza wananchi na anatuongoza vizuri, tunampongeza sana na tunamtakia afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushahidi ni huu ambao tumeuona tumeongea sana hapa wakati tunachangia bajeti za kisekta. Tulizungumza sana habari ya barabara zetu ziliziko vijijini na tukaeleza kiu yetu ya namna ambavyo tunatakiwa kutenga fedha nyingi za kutosha kwa ajili ya kujenga barabara za vijijini. Kama haitoshi ameweza kutoa milioni 500 kwa kila jimbo na hivi tunavyoongea ma-manager wetu wa TARURA wanaendelea kufanya kazi ya kufanya maandalizi ya kujenga barabara hizi. Maana yake barabara za vijijini zikiwa salama maana yake huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kusafirisha mazao zitaenda kufanikiwa katika vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada yamaneno hayo niseme nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Mchemba, kwa kuwasilisha vizuri bajeti hii ambayo tunaijadili. Kwa hakika bajeti hii imejikita katika kutatua kero za wananchi, bajeti hii imeonesha muelekeo wa Serikali kwa mwaka mmoja ujao; kwa kweli, nimpongeze yeye pamoja na watendaji wake akiwemo Naibu Waziri pamoja na katibu mkuu kwa kazi nzuri ya kutuandalia bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi nimeona maeneo mengi yamefanyiwa kazi, lakini ni vizuri nitoe ushauri wangu ili tuweze kubeba kwa pamoja bajeti hii ambayo inaenda kuboresha maisha ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwenye eneo la kilimo, wote wamezungumza hapa tumepongeza juhudi mbalimbali, lakini tumeangalia katika hili kwamba, bajeti ya Serikali inaeleza wazi kwamba, kilimo kinachangia fedha katika Serikali asilimia zaidi ya 26, lakini tunatenga fedha kidogo sana za maendeleo za kuhakikisha kwamba, tunapanga vizuri mipango ya kilimo cha nchi yetu, lakini wote tunajua kwamba, asilimia zaidi ya 65 ya wananchi wetu ndio wanafanya kilimo vijijini. Maana yake nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, shughuli kubwa inayofanywa na wananchi wetu wa Tanzania ni kilimo, lakini kilimo hiki kikitumika vizuri tukapata mazao ya kutosha tutaweza kupeleka malighafi nyingi kwenye viwanda. Maana yake tutakuwa na uwezo mkubwa wa kukuza viwanda na ambayo itatusaidia sana kuongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu nilikuwa nataka niseme tu kwamba, pamoja na kuwa nchi yetu imeingia kwenye kipato cha kati na kama tusipoangalia vizuri tutarudi tena nyuma, ombi langu ni kwamba, tuongeze nguvu sana kwenye kilimo cha nchi yetu. Wananchi wetu wasaidiwe walime kilimo cha kisasa. Ninajua juhudi zipo kubwa na kwenye hili nitaongelea zao la alizeti kwa asilimia kubwa kwa sababu, zao hili linalimwa sana katika mikoa 19 ya nchi yetu, pamoja na Mkoa wa Singida tunalima sana alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa. Tarehe 13 mwezi wa sita aliitisha kikao cha wadau wa alizeti katika Mkoa wa Singida na alionesha wazi kwamba, Serikali imedhamiria kuwekeza sana, ili kuondokana na kuagiza mafuta nje ya nchi. Tunatumia fedha zaidi ya bilioni 400 kuagiza mafuta kila mwaka ili kufidia gape lililopo la mafuta katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nieleze kwamba, tumepata mwanga mzuri juzi tulivyokaa na wadau. Na Mheshimiwa Waziri Mkuu ametumia muda wa saa nane amekaa kwenye kiti anasikiliza maoni ya wadau, ikiwemo sisi Wabunge. Niombe sana eneo ambalo limeelezwa sana ni sehemu ya kupata pembejeo ikiwemo mbegu bora zenye kutoa tija. Niombe sana kupitia bajeti hii tuongeze fedha za mbegu bora, ili wananchi wetu waweze kulima alizeti itakayoleta mafuta mengi, uzalishaji mwingi na kusaidia viwanda vyetu viweze kuzalisha mafuta mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea kwa sababu uzalishaji ni mdogo tumegundua kwamba, wanafanya miezi mitatu tu ya mwanzo, miezi iliyobakia yote hakuna uzalishaji wa mafuta kwa sababu, hakuna mbegu za mafuta za kukamua. Kwa hiyo, niombe sana kwenye eneo hili tumesema kwamba, tutahakikisha kwamba, miundombinu ya umwagiliaji tutaiongeza. Kwenye eneo hili ninaomba sana Serikali iongeze nguvu kwani kilimo hiki kikiwepo kitasaidia sana uzalishaji wa kutosha bila kutegemea mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye hili niseme kwenye eneo moja tumekuwa tukitengewa fedha, lakini hazitoki kwenye skimu ya umwagiliaji katika kata yangu moja inaitwa Mang’onyi. Skimu ya umwagiliaji hii ikikamilika itasaidia wakulima wengi kupata kilimo cha umwagiliaji na kuongeza tija katika kilimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi tumeongelea habari ya upimaji wa udongo. Kuna maeneo mengi wakulima wanalima tu ilimradi wanalima, lakini hawajui ardhi yao ina uwezo gani wa kuzalisha mazao. Tumeomba sana watafiti wetu wafanye kazi hiyo kuhakikisha kwamba, ardhi ambayo tunalima inakuwa ni ardhi inayojulikana wazi; kama inahitaji mbolea ijulikane ni mbolea kiasi gani, ili wakulima wetu waweze kulima kwa uhakika. Na kwenye hili Waziri Mkuu ameelekeza kwamba, wenzetu wataalamu wa kilimo waweze kufanya kazi yao vizuri, washauri kwenye halmashauri zetu ili tuweze kuhakikisha tunalima kilimo cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kilimo hiki ni pamoja na kuhakikisha kwamba, tunaongeza kilimo cha chakula kwa maana ya mazao mbalimbali yanayotokea huku, ili tuwe na usalama wa chakula. Niseme tu, nieleze tu kwamba, pamoja na kwamba, tunaongelea kilimo, lakini nishukuru sana Mheshimiwa Rais ameonesha wazi kwamba, bajeti hii ni kweli ni bajeti ya kazi iendelee. Kwa sababu, miradi yote ya kimkakati amesema itaendelea na juzi akiwa Mwanza amezindua tena ujenzi wa reli ya SGR kutoka Mwanza kwenda Isaka maana yake sasa inakutana katikati iweze kukamilika ianze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imeeleza waziwazi usafiri wa anga pamoja na ununuzi wa meli ambao amesaini juzi meli tano zinaenda kujengwa pamoja na uboreshaji wa bandari. Hili ni jambo jema kabisa, tuendelee kuiomba Wizara, tuendelee kutoa fedha ambazo zimetengwa ili miradi hii isikwame njiani ili tuweze kupata matokeo ambayo tunayatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo hili nitaongelea kidogo kwenye eneo la wilaya yangu. Wilaya ya Ikungi tulikuwa na maombi ya muda mrefu, tunaomba tuwe na mradi wa kimkakati na sisi tuwe na stendi ya wilaya; hatuna stendi ya mabasi ambayo inaweza kukidhi haja iliyoko pale katika wilaya yetu. Lakini kwenye eneo hili pia nilikuwa naomba tupate soko la kisasa katika eneo lile katika wilaya yetu, ili kuongeza mapato ya halmashauri ili yasaidiane na bajeti ya Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi wetu katika vijiji vyetu pamoja na wilaya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niongelee jambo la tatu ni jambo la maslahi ya watumishi. Hili eneo niipongeze sana Serikali kwa kuamua sasa kwamba, wafanyakazi wapatoa 94,000 wanaenda kupandishwa madaraja na fedha zipo katika bajeti hii. ni jambo jema sana pamoja na kuwa tunasema waongezewe mshahara, lakini ukipandishwa daraja una uhakika na kulipwa mshahara katika daraja lako. Wengine wanajiendeleza katika elimu, lakini wanakuwa wanabaki hawapandishwi madaraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara husika ihakikishe inasimamia vizuri wafanyakazi hawa wapate haki yao ya kuhakikisha wanapanda madaraja. Nimeona zimetengwa karibia bilioni 400 zinaenda kufanya kazi hii ni jambo jema sana tunamshukuru sana Rais, tunamshukuru sana Waziri kwa kuwasilisha jambo hili; lakini niendelee kuomba tuendelee kuendelea kuwaza kuongeza mapato, ili tuweze kuongeza mishahara ya watumishi ambayo kwa kweli, wameendelea kuomba kila mara na dhamira ya Mheshimiwa Rais tunaiona atawaongezea kama alivyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo hili tumeongelea pale Madiwani, Madiwani wanafanya kazi nzuri sana kule. Nipongeze kwamba, fedha zile ambazo walikuwa wanalipwa posho yao itaenda moja kwa moja kutoka kwenye Serikali kuu ni jambo jema. Lakini niombe sana Mheshimiwa hii ilikuwa ni hiyo fedha wanalipwa huko nyuma kwa hiyo, wamekuwa na maombi ya kuda mrefu tunaomba posho ziongezwe za Madiwani ili wafanye kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika maeneo yetu. Sisi tukiwa huku wao wanafanya kazi vijijini kule kukaa karibu na wananchi katika kusimamia maendeleo, tukiwaongezea wataongeza motisha, wataongeza nguvu kubwa ya kusimamia maendeleo na fedha hizi tunazozipeleka kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo tumeongelea habari ya suala la Madiwani, lakini kuna namna ambavyo tunadhani kule kwenye vijiji tuone namna ambavyo tutaongeza fedha kwa ajili ya kuwasaidia viongozi wetu wa vijiji ili waweze kufanya kazi kwa tija.

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga. Ahsante sana.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ninaunga mkono asilimia 100 bajeti hii. Nawatakia kila la heri, ahsante sana. (Makofi)