Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii, ambayo ni bajeti ya kwanza ya awamu ya sita na vilevile ni bajeti ya kwanza katika mpango wa miaka mitano, wa 2021/2022 kwenda mpaka 2025/2026 ambayo dhima yake ni uchumi wa viwanda shindani na shirikishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linanigusa sana na nimeliongelea sana hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake pamoja na Naibu Waziri na timu yake kwa kutupa bajeti hii ambayo kwa kweli imegusa mioyo ya Watanzania. Sisi Wabunge ni mashahidi, mengi yaliyosemwa katika bajeti hii ni yale ambayo sisi kama Wabunge tuliomba Serikali iyashughulikie. Kwa hiyo tunamshukuru sana, na kwa vile hii ni Bajeti ya Taifa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais jemedari wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ndiye chachu kubwa ya bajeti hii, tunamshukuru sana. Mimi kibinafsi namshukuru kwanza kwa sababu ndani ya bajeti hii tunaona dhamira ya dhati ya kuishirikisha sekta binafsi katika kuendesha uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tupende tusipende sekta binafsi ndiyo sekta ambayo tunaitegemea kwa kupata mapato makubwa ya nchi. Lakini si hilo tu, ndani ya bajeti hii tunaona wazi kabisa kwamba Mheshimiwa Rais anatoa maono ya wazi na miongozo ya kuonesha kwamba miradi mbalimbali ambayo ilikuwa ni ya sekta binafsi ambayo imekwamba sasa ipate ufumbuzi na iweze kuendelea mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kwa kifupi kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kiukweli kabisa kwa kutoa muongozo kuhusiana na mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu umeongelewa kwa muda mrefu sana, na ulifikia mahali ukawa kama ni wimbo tu; unaimbwa unaisha. Lakini sasa tunaona dhamira ya dhati kabisa ya Mheshimiwa Rais, kwamba majadiliano yale ambayo yalikuwa yamekwama yaweze kuendelea na kukamilishwa; na kama hayawezekani basi tutafute alternative nyingine. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee sekta ya kilimo. Sekta hii ya kilimo wote tunafahamu kuwa ni sekta ambayo imetoa mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi; asilimia 26 ya Pato Ghafi la Taifa linatokana na sekta hii ya kilimo. Asilimia 65 ya waajiriwa ambao wanatoka katika maeneo ya vijijini Watanzania wanatoka katika sekta hii ya kilimo. Lakini siyo hilo tu mchango wa sekta hii kwa upande wa kuleta pesa ya kigeni ni takriban asilimia 24.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza ni kwamba sekta hii inatia huruma. Kwa sababu pamoja na hizo namba tunazoziongea hapa uwekezaji kwenye sekta hii bado ni mdogo sana, na wengi wameliongea hilo. Tunaongelea chini ya asilimia 0.8 wengine wanasema asilimia 1.9 lakini ukweli ni kwamba ni mdogo mno; na udogo wa uwekezaji huo si kwa Serikali peke yake kupitia bajeti bali hata kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, benki zetu bado hazijachangamkia fursa kubwa ambazo zipo katika sekta hii kubwa ya kilimo. Ukiangalia mgawanyo wa fedha ambazo zimekwenda kwenye sekta binafsi kwa ajili ya kilimo inasikitisha kuona kwamba takriban asilimia 35.8 ya mikopo ya benki imekwenda kwenye mambo binafsi tu ya watu. Asilimia 15.7 imekwenda kwenye biashara za kawaida, asilimia 10 kwenye viwanda, lakini kilimo ni asilimia nane tu. Kwa hiyo tuna tatizo kubwa la uwekezaji kwenye sekta hii upande wa Serikali kupitia bajeti lakini vile vile kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani sasa wote tuna kazi ya kufanya hapa, lakini la kwanza kabisa tuanze na maamuzi ya kibajeti. Naelewa hakuna kitu tunachoweza tukakifanya katika bajeti hii kwa sasa, lakini tunaiomba sana Serikali na tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri, wote tutambue kwamba lazima tuitendee haki Tanzania; na huwezi kuitendea haki Tanzania kama hautatoa pesa za kutosha kwenye sekta hiii ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka mitatu minne iliyopita sekta hii uwekezaji wake umeteremka. lakini huko nyuma angalau tulifikia asilimia tano ya total collection. Lakini tukiweza angalau tukafika angalau tufikie hata asilimia sita, tukiweza kufikia asilimia saba ambayo ndiyo declaration ya Maputo nadhani tutakuwa tayari tunaenda katika mlolongo mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nitoe ushauri; tunahitaji kuvutia uwekezaji kwa namna ya pekee kwenye sekta hii ya kilimo, na ninavyoona tunahitaji kuwa na special scheme za sekta ya kilimo pamoja na vivutio katika sekta hii. Tunajua sekta hii iko katika maeneo ya vijijini huko mikoani. Wengine walisema na mimi nalisisitiza, kwamba iko haja ya kuwa na vivutio vya kikodi na vya kisera ambavyo vita-focus kwenye sekta ya kilimo na kwenye viwanda ambavyo vitakua na vitajengwa katika maeneo ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaloliona sasa hivi kiwanda kinachojengwa eneo la kilimo mikoani na kinachojengwa mikoa ambayo haina kilimo vinakuwa treated sawa; hatuwezi kufika katika utaratibu huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejitahidi kuweka vivutio vya aina fulani katika bajeti hii kwa upande wa cold rooms na vifungashio. Lakini mimi nasema kwamba, pamoja na hilo tunawashukuru lakini bado tutatakiwa tuangalie wapi hasa panahitaji kuwekewa hivyo vivutio. Tuangalie mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo. Mimi nasema, vifungashio sawa, cold rooms sawa, lakini twende tukaangalie pale ambapo kunafanyika uzalishaji wa mazao yetu ya kilimo ndipo hasa tuweke hivyo vivutio. Tuangalie maeneo ambayo kama kuna viwanda vya madawa, tuangalie viwanda vya mbolea, tuangalie vilevile pale ambapo tunahitaji utaalam na utaalamu hatuwezi kuupata hapa basi tulegeze masharti ya vibali kwa watu ambao watakwenda kufanya kazi kama wataalamu kwenye sekta ya kilimo. Tunahitaji kufanya kazi kimkakati ili tuweze kuifunua hii sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu zao la avocado, kwa kifupi tu. Nchi hii ina uwezo mkubwa sana wa kuongeza mapato makubwa sana kama tukiweza ku-focus kwenye zao la avocado. Zao hili linaweza kui-transform Tanzania. Ukichukua nchi kama ya Mexico ambayo eneo lake ni dogo, hata ukubwa wa mkoa wa Njombe Mexico ni ndogo lakini kwa mwaka 2018/2019 Mexico kwa avocado peke yake wameingiza 2.7 billion dollars. Hayo ni mapato yanayofikia mapato yetu yote ya dhahabu. Kwa hiyo iko haja ya kuliangalia hili jambo kwa umakini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa sasa watafiti wanasema katika miaka mitano ijayo Tanzania inaweza ikawa nchi ya uzalishaji mkubwa wa avocado kuliko hata Kenya. Lakini tuna kilio hapa ndani, kwamba avocado zetu sisi tunazi-register kama zinatoka Kenya, na kwa hiyo kuna upotevu wa mapato, lakini vilevile nchi yetu inakosa fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba tatizo hili litaendelea kama tusipoweka mikakati mahiri sasa hivi. Ukiangalia kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam ambayo ndiyo port of exit kubwa tunayoitegemea uwekezaji unaoendelea ni mkubwa lakini bado hauja focus kwenye perishables. Nchi hii inategemewa kuwa projected kuzalisha takriban laki sita za avocado.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukilinganisha na Mombasa watu wanakwenda Mombasa kwa sababu slot za cold rooms Mombasa ziko 1800, unakwenda na container una slot unangojea meli Tanzania TICTS Pamoja na TPA slot zipo 120. Kwa hiyo hakuna uwezo wowote utakaotufanya sisi tuende kwenye huo ushindani na tukashinda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuongea kidogo sekta ya Madini, ukiangalia utakuta kwamba tumelegalega na nchi yetu kwa kiasi kikubwa sana sekta ya utalii ime-collapse, lakini sekta ya Madini imeweza ku-balance na imenyanyua kwa kufanya shilingi yetu i-stabilize kwa sababu ya dhahabu. Tunamshukuru Mungu kwamba tunaiyo dhahabu, lakini kwa kiasi kikubwa dhahabu yote hiyo imetoka kwenye migodi kama miwili pamoja na wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwamba, tunatakiwa tuendelee kuvuta wawekezaji kwenye Sekta hii ya Madini ili tuweze kupata mapato makubwa. Pia tunatakiwa tu-identify, twende kwenye sekta nyingine au sub- sector nyingine ambazo ndiyo sasa hivi dunia inakwenda na huko tuna wawekezaji kuna maeneo kama ya helium gas, kuna maeneo kama ya rare earth. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo haya tayari tuna wawekezaji, lakini wawekezaji hawa wanagombea mitaji na nchi nyingine na kama hatutafanya maamuzi haraka ina maana hiyo opportunity haitakuwepo na hatutaweza kukua na kupata mapato makubwa ambayo kama tungekuwa na migodi kila mahali inafanya kazi, kila mahali inazalisha, tungekuwa na uchumi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba, mambo mengi yamefanyika ya kikodi hapa ambayo yanataka kusisimua uchumi, lakini tukiwa na utendaji na uzalishaji na migodi na huku wewe unalima uchumi huu siyo kwamba utasisimuka lakini utazimuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)