Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema anayetujalia mpaka sasa hivi tukiwa tuko katika hali ya afya na uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nianze kwa kukupongeza wewe kwa kunipatia fursa ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. Aidha, nichukue fursa hii kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kaka yangu Nchemba pamoja na Naibu Waziri kaka yangu Masauni kwa hotuba nzuri ambayo kwa kweli inawagusa Watanzania wote. Vile vile, nichukue fursa hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote kwa ujumla wao kwa namna wanavyoendelea kujitoa kumsaidia mama yetu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassain, kwa kweli Waheshimiwa Mawaziri tunawaambia hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona jinsi mnavyofanya kazi ya kuhakikisha kwamba mnawatumikia Watanzania kwa lengo la kulipeleka mbele Taifa letu, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna anavyoendelea kuwasimamia Mawaziri na kuisimamia Serikali kuhakikisha kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pongezi za pekee nimpongeze sana sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassain, kwa namna anavyoendelea kuiongoza nchi yetu kwa mafanikio na ufanisi mkubwa kwa kweli Mama huyu ametuheshimisha sana Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nampongeza Mheshimiwa Rais wetu siku tunamuaga mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, pale Jamhuri alituahidi watanzania kwamba hakutoharibika kitu na kwakweli tumeshuhudia hakuna kitu kilichoharibaka wote ni mashahidi tunaona kwamba miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa, hakuna mradi hata mmoja ambao umesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile na mpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutumiza matarajio, matamanio ya mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Tunaona reli zinaendelea kujengwa, ndege zinaendelea kununuliwa, vituo vya afya vinajengwa, shule zinaendelea kujengwa, mradi wa umeme unaendelea kutelezwa, tunasema kwa kweli Mama yetu anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii, niwaombe watanzania wenzangu kwa umoja wetu bila kujali tofauti zetu tusimame pamoja kumuunga mkono Rais wetu. Kwani ameonesha nia ya dhati ya kulipeleka mbele Taifa letu, ameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia watanzania kwa hiyo tusimame pamoja kumpa support kiongozi wetu Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba sasa nichangie kwenye bajeti hii, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, bajeti ni bajeti nzuri sana kwa kweli ni bajeti ambayo imegusa maisha ya watanzania na kwakweli ni bajeti ya kwanza watangulizi wetu wanasema hapa, kwamba ni bajeti ambayo imesikiliza vilio vya Wabunge kwa asilimia kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona suala la TARURA Wabunge tulisimama hapa kwa umoja wetu kuzungumzia Sakata la TARURA na kwa kweli TARURA ilikuwa ipo katika hali mbaya, kwa sababu barabara za vijijini zilikuwa zipo katika hali mbaya. Ukizingatia athari mbalimbali zimeelezwa kutokana na ubovu wa barabara za vijijini ikiwemo kina mama kujifungulia njiani, watoto kufariki kutokana na kusombwa na maji kipindi cha mvua, lakini vilevile uzito na kupanda kwa gharama ya kusafirisha mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekisikia kilio hiki na kwenda kuweka fedha kwenye mfuko wa TARURA. Lakini vilevile Mama yetu Samia Suluhu Hassan amesikia kilio hiki kwa kuweka kila jimbo shilingi milioni 500 tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuongoza na kuongeza vianzio vipya vya mapato kwenye suala la mapato ya simu vilevile yanatokana na miala ya simu, lakini vilevile malipo ya line. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na kwenye tozo za mafuta kwa kweli umefanya jambo muhimu sana na umeandika historia na watanzania wataendelea kukumbuka kwa kazi yako kubwa uliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, tunafahamu kwamba Wizara ya Mawasiliano ni wizara ambayo haipo kwenye Muungano, lakini kuna sekta ambazo tuna-share pamoja, mfano Sekta ya Mawasiliano kama Posta, lakini vilevile kama TTCL, Air Tanzania na mambo mengine. Sasa kianzio hiki kipya cha mapato ambacho kinakwenda kukusanya mapato kutokana na line za simu na miamala ya simu, tunafahamu kwamba simu hizi wanaotumia ni watanzania wote wa pande zote mbili upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini miamala ya simu inafanywa na watanzania wote na sisi upande wa Zanzibar wananchi walio wengi mpaka vijijini wanatumia simu, ni watu wachache sana ambao hawamiliki simu. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba ukija uje utueleze kama Wanzibar na sisi mmetufikiria vipi, tunakwenda kufaidika vipi kutokana na fedha hii ambayo itakusanywa kutokana na makusanyo ambayo tunayachangia wote watanzania, tunaombeni sana na sisi kule Zanzibar kusema ukweli hali ni mbaya sana ya barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile nije suala la fedha hizi milioni 500 kama tulivyosema kwamba Mama amefanya jambo zuri sana, lakini kiukweli na sisi Zanzibar barabara zetu za vijijini hali ni mbaya sana. Na tunafahamu hatuna shaka Mama yetu atakisikia kilio hiki.

Nichukue fursa hii kwa niaba ya Wabunge wenzangu wa Zanzibar tunamuomba sana Mama yetu, tunamlilia na sisi atuangalie hali zetu za barabara Zanzibar kwakweli ni mbaya, tunamuomba sana atuangalie ili na sisi aweze kutupatia fedha hizi na wala hatuna shaka kutokana na usikivu wake nina imani yangu kwamba atatufikiria. Waswahili wanasema Mama ni Mama na anaye mdharau Mama hukumbwa na laana, hatupo tayari kukumbwa na laana, tunafahamu sana Mama yetu ni msikivu na ataendelea kutusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kumalizia nigusie Sekta ya Uvuvi mara nyingi tumekuwa tukipiga kelele kuhusu Sekta ya Uvuvi hususani kwenye kanuni zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba hadi sasa bado Serikali haijataka kuliangalia kwa ukaribu sana kuhusiana na changamoto ya kanuni ya uvuvi inayozuia ring net hadi sasa hivi ninavyoongea wavuvi wa Kigamboni na wa Mafia bado hawajapatiwa leseni, wanakaa hivi watu wanafamilia, wanakaa kila wakifika wanapigwa danadana hawapatiwi leseni kisingizio ni kanuni, tuambie, Mheshimiwa Waziri nikuombe au kwa Waziri Mkuu aliingilie kati wavuvi wanapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi wa ring net uliingia nchini mwaka 1984 mpaka 1985 Serikali iliwapatia kibali na ikauhalalisha uvuvi huu kwamba auharibu mazingira. Lakini kama haitoshi uvuvi wa ring net duniani nchi kama India, China, Norway, Dubai, Finland, Oman zinatumia uvuvi huu na uvuvi huu hata Shirika la Chakula Duniani unautambua uvuvi huu wa ring net kwamba hauharibu mazingira, iweje leo Tanzania tuseme kwamba uvuvi huu unaharibu mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali ituangalie ndugu zetu wanapata tabu wanategemea Sekta ya Uvuvi na Serikali inapiga kelele kwamba wananchi wajiajiri sasa wanapojiajiri tunapokwenda kuwawekea vikwazo tujue tunawasababishia mazingira magumu. Mtu anatoka ameacha watoto nyumbani anakwenda sehemu za Mafia au Kigamboni kufanya shughuli ya uvuvi akifika anazuiwa tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana Mwenyekiti kwa kunipatia fursa. (Makofi)